Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Maana yake ni kwamba hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah. “Hapana mungu” ni kukanusha kila kinachoabudiwa badala ya Allaah, ilihali “isipokuwa Allaah” ni kuthibitisha ya kwamba ´ibaadah afanyiwa Allaah pekee. Hana mshirika katika ´ibaadah Yake, kama ambavyo hana mshirika katika ufalma Wake.

MAELEZO

Maana ya “hapana mungu isipokuwa Allaah” ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Shahaadah hii ni mtu atambue kwa mdomo wake na kwa moyo wake ya kwamba hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall). Neno “hapana mungu isipokuwa Allaah” limekusanya ukanushaji na uthibitishaji.

Neno “hapana mungu” kuna ukanushaji ilihali uthibitishaji upo katika neno “isipokuwa Allaah”. Kwa msaada wa maelezo ya maunganisho haya “kwa haki” kutakuwa kumebainika jawabu juu ya utatizi unaosema “Vipi mtu atasema ya kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah ilihali kuna wangu wengi wanaoabudiwa badala ya Allaah na sivyo tu, bali Allaah amewaita kuwa ni “waungu” na wale waabudiwa wao? Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

فَمَا أَغْنَتْ عَنْهُمْ آلِهَتُهُمُ الَّتِي يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ لَّمَّا جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ

“Basi hawakuwafaa kitu chochote waungu wao waliyokuwa wakiiomba badala ya Allaah ilipokuja amri ya Mola wako.” (Huud 11 : 101)

Na vipi tunaweza kuthibitisha uungu wa mtu mwingine, mbali na uungu wa Allaah,  ilihali Mitume walikuwa wakiwaambia watu wao:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika nyinyi hamna mungu mwengine badala Yake!”? (al-A´raaf 07 : 59)

Jibu la utatizi huu linabainika kwa kile kielezi kinachosema “hapana mungu isipokuwa Allaah”. Miungu hii inayoabudiwa badala ya Allaah ni miungu ya batili. Sio miungu ya kikweli na haina haki yoyote ya kuabudiwa. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

”Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye Mwenye haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.” (al-Hajj 22 : 62)

Dalili nyingine ni maneno Yake (Ta´ala):

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ تِلْكَ إِذًا قِسْمَةٌ ضِيزَىٰ إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَمَا تَهْوَى الْأَنفُسُ ۖ وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّن رَّبِّهِمُ الْهُدَىٰ

“Je, mmeona al-Laat na al-‘Uzzaa na Manaat, mwengine wa tatu? Je, nyinyi mna wana wa kiume Naye ana wana wa kike? Huo ni mgawanyo si wa uadilifu! Hayo si chochote isipokuwa ni majina mmeyaita nyinyi na baba zenu; wala Allaah hakuyateremshia madaraka yoyote. Hawafuati isipokuwa dhana na yale yanayotamani nafsi zao na hali   imekwishawajia kutoka kwa Mola wao uongofu.” (an-Najm 53 : 19-23)

Amesema (Ta´ala) ya kwamba Yuusuf (´alayhis-Salaam) amesema:

مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ

“Hamwabudu pasi Naye isipokuwa majina mmeyaita nyinyi na baba zenu; hakuyateremshia Allaah kwayo mamlaka yoyote.” (Yuusuf 12 : 40)

Kwa hivyo “hapana mungu isipokuwa Allaah” maana yake ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall). Ama kuhusiana na vyengine vyote vinavyoabudiwa badala ya Allaah, uungu wao unaodaiwa ni wa batili. Kwa msemo mwingine ni uungu wa batili.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 70-73
  • Imechapishwa: 28/05/2020