50. Baadhi ya fadhila za ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh)

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

وقل إنَّ خير النَّاسِ بعد محمَّدٍ

15 – Sema “Watu bora baada ya Muhammad

وزيراهُ قدماً ثم عثمانُ الارجَحُ

    ni mawaziri wake wawili wa tangu zamani, kisha ´Uthmaan [ndio maoni] yenye nguvu zaidi

MAELEZO

Watatu inapokuja katika ubora ni ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh). Yeye ni miongoni mwa wa awali waliotangulia katika Uislamu. Alihajiri mara mbili; alihajiri kwenda Habeshi na akahajiri kwenda al-Madiynah. Akajitolea mali tele katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall) na akanunua kisima cha warumi kwa ajili ya waislamu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni nani atayenunua kisima hichi na yuko na Pepo?”[1]

Akakinunua ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) na akakifanya ni Waqf kwa waislamu. Akaandaa jeshi la ´Usrah kikamilifu kutokana na mali yake. Yeye ndiye ambaye alishika uongozi baada ya ´Umar kwa maafikiano ya watu wa mashauriano ambao aliwateulia ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). Wakampa kiapo cha usikivu na utiifu na waislamu kadhalika wakafanya hivo.

Isitoshe yeye ni mume wa wasichana wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambao ni Ruqayyah na Umm Kulthuum. Ndio maana akaitwa Dhun-Nurayn (aliye na nuru mbili) kwa kuwa alioa wasichana wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Makkah kuzungumza na washirikina na kukaenezwa uvumi kwamba ameuawa, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamlia kiapo kwa mkono wake na kusema:

“Hii ni kwa ajili ya ´Uthmaan.”[2]

Kiapo kikatimia pasi na yeye kuwepo kwa kuwa wakati huo alikuwa Makkah.

Kadhalika yeye ndiye ambaye aliandika msahafu unaoitwa “msahafu wa ´Uthmaan” kwa hati ya ´Uthmaan. Hati yake ndio hii misahafu tulionayo hii leo. Fadhilah zake ni nyingi (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] al-Bukhaariy (2778)

[2] al-Bukhaariy (3698) na (4066)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 118-119
  • Imechapishwa: 10/01/2024