Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”[1]

“Pindi waislamu wawili watapokutana na silaha zao yule muuaji na yule muuliwaji Motoni.”[2]

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumuua ni ukafiri.”[3]

“Yule mwenye kumwambia nduguye “ee kafiri”, basi imemgusa mmoja wao.”[4]

“Ni kumkufuru Allaah mtu kuikana nasabu yake hata kama imefichikana.”[5]

Hizi na Hadiyth mfano wake ambazo ni Swahiyh na zimehifadhiwa tunajisalimisha nazo ijapokuwa hatuzielewi. Hatuzizungumzii, hatujadiliani nazo na wala hatuzifasiri kwa njia inayopingana na uinje wake. Hatuzirudishi isipokuwa kwa kitu kilicho na haki zaidi ya kukipokea.”

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ametoa baadhi ya mifano kuonyesha kufuru ndogo isiyomtoa mtu katika Uislamu. Hadiyth hizi zimetaja kufuru na hakukukusudiwa kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu. Mambo haya yameitwa kuwa ni “kufuru” kwa sababu kunazingatiwa ni kukanusha mambo maalum. Kwa mfano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msirudi baada yangu kuwa makafiri wapotevu baadhi wakizikata shingo za wengine.”

Hapa ni kutupilia mbali ule udugu wa Kiislamu ambao Allaah (´Azza wa Jall) amesema juu yake:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ

“Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu. Na Mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.”[6]

Yule mwenye kumpiga vita ndugu yake ametupilia mbali ule udugu wa kiimani. Kadhalika:

“Pindi waislamu wawili watapokutana na silaha zao yule muuaji na yule muuliwaji Motoni.”

Haina maana kwamba watadumishwa Motoni milele. Kunasemwa hayohayo juu ya hizo Hadiyth zengine mfano wake.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema juu ya Hadiyth zilizotangulia kutajwa:

“Hizi na Hadiyth mfano wake ambazo ni Swahiyh na zimehifadhiwa tunajisalimisha nazo ijapokuwa hatuzielewi. Hatuzizungumzii, hatujadiliani nazo na wala hatuzifasiri kwa njia inayopingana na uinje wake. Hatuzirudishi isipokuwa kwa kitu kilicho na haki zaidi ya kukipokea.”

Hata hivyo hapana ubaya kuzizungumzia kwa njia ya inayobainisha maana yake ya sawa pamoja na kubainisha kwamba wale ambao wataadhibiwa Motoni kisha baadaye kutolewa na kuingizwa Peponi watafanya hivo baada ya kuadhibiwa kwa muda mrefu na Allaah ndiye mwenye kujua zaidi.

Sasa tumejua kuwa makusudio ya kufuru iliyotajwa ni kufuru ndogo. Huenda baadhi ya watu wakaelewa kwamba ni kufuru inayomtoa mtu katika Uislamu. Hayo ndio yaliyowatokea Khawaarij. Ni ujinga. Muislamu anapaswa kuwarejelea wanachuoni katika mambo haya. Wanachuoni namaanisha wale wenye utambuzi juu ya Hadiyth na wenye kufuata mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.”[7]

Tunatambua kuwa Khawaarij na wengineo wamepotea kwa sababu ya kufasiri kwao Qur-aan na Sunnah kwa matamanio yao. Hawakurejea kwa wanachuoni juu ya Hadiyth. Hiyo ikawa ndio sababu ya wao kupotea; wao kwa wao walikuwa wakifasiriana na wakaongozana katika ujinga na upotevu huu na matokeo yake wakaangamia na wakasababisha wengine kuangamia.

[1] al-Bukhaariy (121) na Muslim (65).

[2] al-Bukhaariy (31) na Muslim (2888).

[3] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

[4] al-Bukhaariy (6104) na Muslim (60).

[5] Ahmad (2/215). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (4485).

[6] 49:10

[7] 16:43

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 171-172
  • Imechapishwa: 06/06/2019