48. Uwajibu wa kutulizana katika Rukuu´


Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitulizana katika Rukuu´ na akamwamrisha hivo yule mtu aliyeswali kimakosa, kama tulivyotangulia kutaja.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Timizeni Rukuu´ na Sujuud zenu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake ya kwamba mimi naweza kukuoneni nyuma yangu[1] pindi mnaporukuu na mnaposujudu.”[2]

Alimuona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwanamume mmoja haitimizi Rukuu´ yake na anadonoa katika Sujuud yake akasema:

“Lau mtu huyu angelikufa katika hali hii basi angelikuwa amekufa katika dini isiyokuwa ya Muhammad. Anadonoa swalah yake kama adonoavyo kunguru damu. Mfano wa ambaye haitimizi Rukuu´ yake na anadonoa katika Sujuud yake ni kama mfano wa mtu ambaye anakula tende moja au mbili; hazimnufaishi kwa chochote.”[3]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kipenzi wangu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amenikataza kuidonoa swalah yangu kama jogoo, kugeukageuka kama mbweha na kuchuchumaa kama ngedere.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwizi mbaya kabisa ni yule anayeiba katika swalah yake.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi ataiba katika swalah yake?” Wakasema: “Hatimizi Rukuu´ wala Sujuud yake.”[5]

Wakati mmoja alipokuwa akiswali mara akamtupia jicho kupitia kwenye pembe ya jicho lake mtu ambaye alikuwa hanyooshi uti wa mgongo wake katika Rukuu´ na Sujuud. Alipomaliza akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi waislamu! Haisihi swalah ya yule ambaye hasawazishi uti wa mgongo wake katika Rukuu´ na Sujuud.”[6]

Amesema katika Hadiyth nyingine:

“Swalah ya mtu haisihi mpaka asawazishe uti wa mgongo wake katika Rukuu´ na Sujuud.”[7]

[1] Kuona huku ni kwa hakika na ni moja katika miujiza yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo ni jambo linahusiana katika swalah peke yake. Hakuna dalili ya kuona kwa ujumla.

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

[3] Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” (1/349), al-Aajurriy katika ”al-Arba´iyn”, al-Bayhaqiy , at-Twabaraaniy (1/192/1), adh-Dhwiyaa’ katika ”al-Muntaqaa” (1/276) na Ibn ´Asaakir (2/226/2) kwa mlolongo wa wapokezi mzuri. Imesahihishwa na Ibn Khuzaymah (1/82/1). Sehemu ya kwanza ya sentesi ina upokezi wenye kuutilia nguvu katika ”al-Ibaanah” (1/43/5) ya Ibn Battwah hata hivyo ni usimulizi ambao ni Mursal.

[4] at-Twayaalisiy, Ahmad na Ibn Abiy Shaybah. Hadiyth ni nzuri, kama nilivyoieleza katika taaliki zangu ya ”al-Ahkaam” (1348) ya Haafidhw ´Abdul-Haqq al-Ishbiyliy.

[5] Ibn Abiy Shaybah (2/89/1), at-Twabaraaniy na al-Haakim aliyeisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[6] Ibn Abiy Shaybah (1/89/1), Ibn Maajah na Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. Tazama ”as-Swahiyhah” (2536).

[7] Abu ´Awaanah, Abu Daawuud na as-Sahmiy (61). ad-Daaraqutwniy ameisahihisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 113-114
  • Imechapishwa: 17/02/2017