Kuna aina tatu ya waja wema:

1 – Waliotangulia na waliokurubishwa. Hawa ni wale waliotekeleza mambo ya faradhi na mambo ya wajibu na wakajikurubisha kwa Allaah kwa kufanya mambo ya kujitolea na yaliyopendekezwa. Sambamba na hayo wakajiepusha na mambo ya haramu na mambo yaliyochukizwa ambayo sio ya haramu. Aidha wakajiepusha kupindukia katika yale mambo yaliyoruhusiwa (المباحات) kwa kuchelea wasije kuingia ndani ya mambo yaliyochukizwa.

2 – Wa kati na kati. Hawa ni wale watu wa kuliani. Ni wale waliofanya mambo ya wajibu peke yake na wakasimama katika mpaka huu. Hakuwa na uchangamfu wa kufanya mambo ya kujitolea na mambo yaliyopendekezwa. Aidha wakajiepusha na mambo yaliyoharamishwa na wakasimama katika mpaka huu na hawakujiepusha na mambo yaliyochukizwa ambayo sio ya haramu. Pengine wakapindukia katika yale mambo yaliyoruhusiwa (المباحات).

Aina zote mbili wataingia Peponi pale mwanzoni – hiyo ni fadhilah na ihsaan kutoka kwa Allaah.

3 – Waliojidhulumu nafsi zao. Hawa ni wale waumini na wenye kumwabudu Allaah pekee na hawakutumubukia ndani ya shirki. Lakini wamejidhulumu nafsi zao kwa kufanya mapungufu katika baadhi ya mambo ambayo ni wajibu au wamefanya baadhi ya mambo ambayo ni haramu. Hawa kuna khatari juu yao wakaadhibiwa ndani ya kaburi kutokana na maasi yao. Pia kuna khatari wakaingia Motoni. Lakini huenda Allaah akawasamehe na pengine wakafanyiwa uombezi na hivyo wasiingie Motoni. Pengine vilevile wakaadhibiwa Motoni kwa kitambo fulani lakini hata hivyo hawatodumishwa ndani yake milele. Wakishasafika Allaah atawatoa nje ya Moto kwa uombezi wa waombezi na huruma ya Mwingi wa huruma. Amesema (Ta´ala) juu ya aina tatu za watu hawa:

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَذْهَبَ عَنَّا الْحَزَنَ ۖ إِنَّ رَبَّنَا لَغَفُورٌ شَكُورٌ الَّذِي أَحَلَّنَا دَارَ الْمُقَامَةِ مِن فَضْلِهِ لَا يَمَسُّنَا فِيهَا نَصَبٌ وَلَا يَمَسُّنَا فِيهَا لُغُوبٌ

“Kisha Tukawarithisha Kitabu wale tuliowateuwa miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni aliyedhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa kati na kati na miongoni mwao aliyetangulia kwa mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah – hiyo ndio fadhilah kubwa. Mabustani ya kudumu milele wataziingia, watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri na watasema: “Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye ametuondoshea huzuni. Hakika Mola wetu bila shaka ni Mwingi wa kughufuria,  Mwingi wa kupokea shukurani; ambaye ametuweka Nyumba yenye kudumu kwa fadhilah Zake, hatutopatwa humo mashaka na wala hatutopatwa humo na machovu.”[1]

[1] 35:32-35

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 81
  • Imechapishwa: 20/06/2022