47. Tofauti iliyopo kuhusu ni nani bora kati ya ´Uthmaan na ´Aliy


Tumetangulia kuzungumza juu ya fadhila za Maswahabah na kwamba wanatofautiana katika fadhila baina yao. Hata hivyo wanashirikiana katika fadhila za uswahabah. Hakuna yeyote anayeshirikiana nao katika fadhila hii. Hakuna yeyote anayewafikia katika hili. Kuhusu wao kati yao wanashindana. Baadhi ni wabora zaidi kuliko wengine. Tukisema kuwa baadhi ni wabora zaidi kuliko wengine haina maana kwamba tuwatukane wale wenye kushindwa ubora. Haijuzu kumtukana yule anayeshindwa ubora ilihali ni Swahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kadhalika tumetangulia kubainisha kuwa Maswahabah bora ni wale makhaliyfah wane. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangofu baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu.”

Ambaye amewaita kuwa ni makhaliyfah waongofu ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pia akaamrisha kushikamana na Sunnah zao kwa kuwa wanapita juu ya Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanazithibitisha na kuzitawanya kutokana na ile elimu, nguvu na uongozi aliyowapa Allaah.

Mbora zaidi katika makhaliyfah wanne ni Abu Bakr na kisha ´Umar. Haya ni kwa maafikiano ya waislamu. Walitafautiana kwa ´Aliy na ´Uthmaan ni nani ambaye ni bora zaidi. Kuna kundi lilimfadhilisha ´Uthmaan. Kundi lingine likamfadhilisha ´Aliy. Kundi lingine likasimama. Yote haya yanahusiana na ubora/fadhila. Kuhusu uongozi Ummah mzima umeafikiana juu ya kwamba uongozi baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wa Abu Bakr, kisha wa ´Umar, halafu wa ´Uthmaan na kisha wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Huu ndio mpangilio wa uongozi kwa maafikiano. Shaykh-ul-Islaam (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”:

“Mwenye kutukana uongozi wa mmoja katika hawa ni mpotevu kuliko punda wa kufugwa.”[1]

Kuna tofauti kati ya masuala ya ubora na masuala ya uongozi. Kuhusu masuala ya ubora waislamu wameafikiana juu ya kwamba mbora ni Abu Bakr na kisha ´Umar. Wakatafautiana ni nani bora kati ya ´Aliy na ´Uthmaan. Maoni sahihi ni kwamba ´Uthmaan ndiye bora zaidi. Kwa mtazamo wa kuwepo tofauti inatajwa. Vinginevyo ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ndiye bora zaidi. Dalili ni kuwa watu wa mashauriano walimtanguliza ´Uthmaan juu ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) katika uongozi.

Masuala ya ubora kati ya ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ni kitu chepesi. Kutukana uongozi ndio upotevu. Kwa sababu Raafidhwah wanasema kuwa khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ´Aliy na ndiye muusiwa. Wanasema kuwa Maswahabah walimdhulumu na wakampokonya uongozi. Isitoshe wanamlaani Abu Bakr na ´Umar na wanawaita kuwa ni masanamu mawili ya ki-Quraysh. Hili bila ya shaka yoyote ni upotevu, ukafiri na ni kwenda kinyume na maafikiano. Khaliyfah baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, halafu ´Umar, halafu ´Uthmaan na halafu ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum).

[1] Tazama “al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah”, uk. 193 Sharh ya mwandishi (Hafidhwahu Allaah).