13 – Mwanamke atapunguza nywele za kichwani mwake kwa ajili ya hajj na ´umrah kwa kiasi cha ncha ya kidole. Haijuzu kwake kunyoa. Ncha ya kidole ni kichwa cha kidole katika tindi yake ya juu. Mtunzi wa “al-Mughniy” amesema:

“Kilichosuniwa kwa mwanamke ni kupunguza nywele na si kunyoa na hakuna tofauti juu ya hilo. Ibn-ul-Mundhir amesema: “Wanachuoni wameafikiana juu ya hilo kwa sababu kunyoa juu yao ni kukatwakatwa. Ibn ´Abbaas amepokea kwa kusema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanawake hawana kunyoa. Kilichoko kwa wanawake ni kupunguza.”

Ameipokea Abu Daawuud.

´Aliy amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mwanamke kunyoa kichwa chake.”

Ameipokea Abu Daawuud.

Ahmad alikuwa akisema:

“Apunguze kwa kila fundo kiasi cha tindi ya juu ya kidole.”

Hayo pia ndio maoni ya Ibn ´Umar, ash-Shaafi´iy, Ishaaq na Abu Thawr.

Abu Daawuud amesema:

“Nimemsikia Ahmad akiulizwa kama mwanamke apunguze nywele zake zote?” Akajibu: “Ndio. Atazikusanya nywele zake mpaka mbele ya kichwa chake kisha atakata katika ncha ya nywele zake kiasi cha tindi ya juu ya kidole.”[1]

Imaam an-Nawawiy amesema katika “al-Majmuu´”:

“Wanachuoni wameafikiana kwamba mwanamke hakuamrishwa kunyoa. Bali kazi yake ni yeye kupunguza nywele za kichwani mwake. Kwa sababu ni Bid´ah juu yao na kukatwakatwa.”[2]

[1] (05/310).

[2] (08/150-154).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 94-95
  • Imechapishwa: 14/11/2019