Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ

”Wakasema: “Haya sisi chochote isipokuwa ni maisha yetu dunia. Tunakufa na tunahuika na hakuna cha kutuangamiza isipokuwa zama tu.” (al-Jaathiyah 45:24)

2- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Mwanadamu ananiudhi. Anatukana wakati – ilihali Mimi ni wakati; Nageuza usiku na mchana.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Msitukane wakati. Kwani hakika ya Allaah ndiye wakati.[2]

MAELEZO

Alichokusudia mwandishi kwa kichwa cha khabari hiki ni kubainisha kwamba kutukana wakati na madhambi mengine ni miongoni mwa mambo yanayopunguza na kudhoofisha Tawhiyd na kupunguza ukamilifu wake. Kwa hivyo ni wajibu kutahadhari na madhambi yote yanayoidhoofisha imani kukiwemo vilevile kutukana wakati, upepo na vyengine vyote visivyostahiki kutukanwa. Ni wajibu kutahadhari na yale yote yanayomkasirisha Allaah.

Wakati umeumbwa na unaendeshwa. Hauwezi kufanya kitu peke yake. Allaah (Ta´ala) ndiye mwenye kuuendesha. Wakati ndani yake kuna nyusiku na michana. Mwenye kutukana wakati anamuudhi Allaah. Hakuna chochote kiwezacho kumdhuru Allaah, lakini maasi yanamuudhi kwa sababu yanamughadhibisha. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا

“Hakika wale wanaomuudhi Allaah na Mtume wake, Allaah amewalaani duniani na Aakhirah na amewaandalia adhabu ya kutweza.” (al-Ahzaab 33:57)

Kutukana wakati maana yake ni kutukana zama kutokana na yale yanayopitika ndani ya usiku na mchana.  Mfano wa hayo ni kama mtu kumuomba Allaah alaani saa au akamuomba Allaah alaani siku fulani au akamuomba Allaah asiibariki siku fulani na mfano wa hayo. Kutukana wakati maana yake ni kuuapiza, kuulani au kuomba du´aa dhidi yake.

Hata hivyo sio matusi kuelezea kwamba wakati ni mzito. Mfano wa hilo ni kama mtu kusema kwamba siku hii ni nzito, ngumu, yenye huzuni, yenye baridi au yenye joto kali.

2- Imesihi kupokelewa kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Mwanadamu ananiudhi. Anatukana wakati – ilihali Mimi ni wakati; Nageuza usiku na mchana.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Msitukane wakati. Kwani hakika ya Allaah ndiye wakati.”

Hapa kumebainishwa maana ya wakati na kwamba ni usiku na mchana. Allaah ndiye mwenye kugeuza usiku na mchana. Mwenye kutukana wakati anamtukana Yule aliyeuumba na kuugeuza. Jambo hilo halijuzu.

Amekosea yule aliyesema kuwa ad-Dahr, wakati, ni katika majina ya Allaah. Mmoja katika wao ni Ibn Hazm. Hadiyth inafahamisha kwamba Allaah ndiye ambaye kaumba wakati na kuutunuku yale yote yanayotokea. Miongoni mwa hayo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msitukane upepo.”[3]

Vivyo hivyo kumtukana ngamia, mbuzi, kondoo, ng´ombe na vyengine vyote visivyostahiki kutukanwa. Kutukana huku kunaipunguza imani na Tawhiyd ya mtu.

[1] al-Bukhaariy (4826) na Muslim (2246).

[2] Muslim (2246).

[3] at-Tirmidhiy (2252), Ibn Maajah (3727), Ahmad (7407), al-Haakim (3075) na al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (719). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (3003).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 140
  • Imechapishwa: 02/11/2018