44. Hekima ya Allaah kuweka ´ibaadah mbalimbali

Waja wa Allaah! Tambueni – Allaah akurehemuni – kwamba Allaah ana hukumu kamilifu na hekima kubwa katika vile alivyoumba na vile anavoweka katika Shari´ah. Hakika Yeye ni mwingi wa hekima juu ya viumbe na Shari´ah Yake. Hakuwaumba waja Wake kwa ajili ya mchezo na wala hakuwaacha burebure pasi na malengo. Hakuwawekea Shari´ah kwa njia ya mchezo. Bali amewaumba kwa lengo kubwa na akawabainishia njia iliyonyooka. Allaah amewawekea Shari´ah mbalimbali zinazowazidishia imani zao na kuwakamilishia ´ibaadah zao. Hakuna ´ibaadah yoyote ambayo Allaah amewawekea waja Wake isipokuwa ni kutokana na hekima kubwa – ameijua yule mwenye kuijua na ameijahili mwenye kuijahili. Ujinga wetu wa kutojua kitu katika ´ibaadah sio dalili inayoonyesha kuwa kitu hicho hakina hekima. Bali hiyo ni dalili juu ya kushindwa kwetu na upungufu wetu wa kutojua hekima ya Allaah (Subhaanah):

وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا

”Hamkupewa elimu isipokuwa kidogo tu.”[1]

Allaah ameweka Shari´ah ya ´ibaadah  na akapanga miamala mbalimbali kwa ajili ya majaribio na kuwatahini waja Wake ili ipate kubainika yule ambaye ni mwenye kumwabudu Mola Wake na yule mwenye kuabudu matamanio yake. Ambaye atakubali Shari´ah hizi na mpangilio huo kwa kifua kikunjufu na nafsi yenye utulivu basi huyo ni mwenye kumwabudu Mola Wake, mwenye kuridhia Shari´ah Zake, anayetanguliza utiifu wa Mola Wake juu ya matamanio ya nafsi. Na yule asiyekubali ´ibaadah na hafuati mpangilio isipokuwa kwa yale yanayoendana na matakwa yake na yakaafikiana na makusudio yake, basi huyo ni mwenye kuabudu matamanio yake, mwenye kuchukia Shari´ah ya Allaah, mwenye kuipa mgongo Shari´ah ya Mola Wake ambaye ameyafanya matamanio yake ni yenye kufuatwa na si yenye kufuata na ambaye anataka Shari´ah ya Allaah iwe ni yenye kufuata matakwa yake licha ya upungufu wa elimu yake na uchache wa hekima yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ

“Lau kama haki ingelifuata matamanio yao, basi zingelibomoka mbingu na ardhi na waliokuwemo humo. Bali Tumewaletea ukumbusho wao lakini hata hivyo wao ni wenye kupuuza ukumbusho wao.”[2]

Miongoni mwa hekima za Allaah ni kufanya ´ibaadah aina mbalimbali zenye kutofautiana ili kupambanuke kukubali, kuridhia na Allaah apate kuwapambanua wale walioamini. Miongoni mwa watu wako ambao wanaweza kufurahia aina fulani ya ´ibaadah na wakaishikilia na wakachukia aina nyingine na wakazembea kwayo. Ndipo Allaah akafanya ´ibaadah zinazohusiana na mwili kama mfano wa swalah. Miongoni mwazo ni zile zinazohusiana na utoaji wa mali inayopendwa zaidi na nafsi kama mfano wa zakaah. Miongoni mwazo ziko zinazohusiana na kitendo cha mwili na utoaji wa mali vyote miwili kama mfano wa hajj na jihaad. Miongoni mwazo ziko ambazo zinahusiana na kuizuia nafsi kutokamana na vile inavopenda na kutamani kama mfano wa swawm.

Mja anaposimama kutekeleza ´ibaadah hizi aina mbalimbali na akazikamilisha kwa njia inayotakikana pasi na kuchukia wala kuzembea ambapo akachoka, akafanya kazi, akajitolea yale yanayopendwa kwake na akaizuia nafsi kutokana na vile inavopenda. Akayafanya yote hayo hali ya kuwa ni mwenye kumtii Mola Wake, kutekeleza amri Yake na kuridhia Shari´ah Yake basi hiyo inakuwa ni dalili juu ya ukamilifu wa uja Wake, ukamilifu wa kunyenyekea Kwake, kumpenda Mola Wake na kumtukuza. Hivyo kunahakikika juu yake sifa ya uja wake kwa Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] 17:85

[2] 23:71

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 61-63
  • Imechapishwa: 12/05/2020