Swali 43: Ni ipi hukumu ya kuswali swalah ya ijumaa sehemu mbili au zaidi katika mji au mtaa mmoja pamoja na kutubainishia dalili za ash-Shaafi´iy[1]?

Jibu: Tambua – Allaah akuwafikishe – kwamba maoni ya kikosi kikubwa cha wanazuoni ni kwamba ni haramu kuswali swalah nyingi za ijumaa katika mji mmoja isipokuwa kukiwa kuna haja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akisimamisha al-Muadiynah al-Munawwarah kipindi cha uhai wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa ijumaa moja. Vivyo hivyo kipindi cha makhaliyfah wake waongofu; Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Kadhalika katika miji mingine yote ya Kiislamu mwanzoni mwa Uislamu. Hayo ni kwa sababu mkusanyiko ni jambo limekokotezwa kwa upande wa Shari´ah takasifu. Waislamu wanapata kukusanyika mahali pamoja wakati wanaposimamisha swalah ya ijumaa na swalah ya ´iyd ambapo wanasaidiana juu ya wema na kumcha Allaah na kusimamisha nembo za Kiislamu. Faida nyingine ni kwamba wanaungana baina yao, wanapendana, wanajuana, kuwa na uelewa juu ya Uislamu na kuigizana katika kheri. Jengine ni fadhilah zaidi na ujira wa wingi wa mkusanyiko na kuwakasirisha maadui wa Uislamu ambao ni wanafiki na wengine kuwa neno lao kuwa moja na kutofarikiana.

Yapo maandiko mengi katika Qur-aan na Sunnah yanayohimiza juu ya umoja na kuungana na kutahadhari kutokamana na mfarakano na kutofautiana. Miongoni mwayo ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[2]

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ

“Wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakatofautiana baada ya kuwajia hoja ubainifu.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Hakika Allaah anaridhia kwenu mambo matatu: mumuabudu na wala msimshirikishe na chochote, mshikamane na kamba ya Allaah na wala msifarakane na muwanasihi wale ambao Allaah amewapatia utawala.”[4]

Kutokana na yaliyotangulia jambo linapata kuwa wazi kwamba lililo la lazima ni kukusanyika watu wa mji au kijiji kimoja katika ijumaa moja kama ambavo wanakusanyika kuswali ´iyd moja ikiwa hilo litawezekana pasi na uzito kutokana na dalili na sababu zilizotangulia na manufaa makubwa katika kukusanyika.

Lakini ikiwa kuna haja kubwa ya kufanya mikusanyiko miwili au zaidi katika mji au mtaa mkubwa hapana neno kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanazuoni. Mfano wa hilo kama pande za mji ziko mbalimbali na inakuwa vigumu kwa watu wake kukusanyika katika msikiti mmoja, basi hapana neno kutekeleza swalah ya ijumaa katika misikiti miwili au zaidi kutegemea na haja. Vivyo hivyo endapo mitaa iko mbalimbali na haiwezekani watu wake wakakusanyika katika msikiti mmoja, basi hapana vibaya watakeleza ijumaa mbili kama katika mji. Kwa ajili hii wakati ilipojengwa Baghdaad na ikawa na mitaa mipana kulifanywa mikusanyiko miwili; mkusanyiko mmoja ulikuwa upande wa mashariki na mkusanyiko mwingine upande wa magharibi. Hayo halifanyika katikati ya karne ya pili mbele ya wanazuoni wanaotambulika na hawakukemea jambo hilo kwa sababu haja ndio imepelekea kufanya hivo. Wakati ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) kipindi cha uongozi wake alipoambiwa kwamba Kuufah kuna wanyonge na inakuwa vigumu kwao kutoka kwenda jangwani kwa ajili ya kuhudhuria swalah ya ´iyd alimwamrisha mtu ambaye atawaswalisha swalah ya ´iyd ndani ya mji na yeye (Radhiya Allaahu ´anh) akaswalisha jopo kubwa la watu waliokwenda jangwani.

Ikifaa kufanya hivo katika ´iyd kutokana na haja basi ijumaa ni mfano wake ili kukusanya ule uzito na kuwanyia urafiki waislamu. Wanazuoni wengi wameonelea kufaa kuwepo swalah nyingi za ijumaa kukiwa kuna haja ya kufanya hivo. Muwaffaq-ud-Diyn Abu Muhammad ´Abdillaah bin Ahmad bin Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema kwa mnasaba wa maneno ya Abul-Qaasim al-Kharqiy (Rahimahu Allaah):

“Mji ukiwa mkubwa ambapo kukahitajika misikiti [ya kuwakusanya watu] basi itafaa kuswali swalah ya ijumaa katika misikiti yote hiyo. Ujumla wake ni kwamba pindi mji utakuwa mkubwa na inakuwa vigumu kuwakusanya watu wake katika msikiti mmoja na hilo likawa haliwezekani kwa sababu ya kuwepo mbalimbali pande zake au msikiti ukawa mdogo kwa watu wake – kama Baghdaad, Aswbahaan na mfano wake katika miji mingine mikubwa – basi itafaa kuswali ijumaa katika misikiti mingine itayohitajia. Haya ndio maoni ya ´Atwaa´ na ameyaidhinisha Abu Yuusuf Baghdaad pasi na kwengine. Kwa sababu adhabu za ki-Shari´ah zinatekelezwa humo maeneo mawili tofauti na ijumaa inatekelezwa pale ambapo kunasimamishwa adhabu za ki-Shari´ah. Maneno yake yanapelekea kwamba endapo kutakuweko mji mwingine ambapo unasimamisha adhabu za ki-Shari´ah maeneo mawili tofauti, basi itafaa kuswaliwa swalah ya ijumaa katika maeneo yake hayo mawili. Kwa sababu swalah ya ijumaa inakuwepo pale ambapo kunatekelezwa adhabu za ki-Shari´ah. Haya ndio maoni ya Ibn-ul-Mubaarak. Abu Haniyfah, Maalik na ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) wamesema kwamba haifai katika mji mmoja kuswali swalah ya ijumaa zaidi ya sehemu moja. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akikusanyika isipokuwa katika msikiti mmoja. Vivyo hivyo ndivo walivofanya makhaliyfah wake baada yake. Endapo itafaa basi haitofaa kuitelekeza misikiti mingine. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema: “Swalah ya ijumaa haifai kuswaliwa isipokuwa katika msikiti mkubwa ambao kiongozi anaswali ndani yake.”[5]

al-Muwaffaq (Rahimahu Allaah) amesema tena:

“Sisi tunaona kuwa swalah iliowekwa katika Shari´ah malengo yake ni kuwakusanya watu na kuwatolea Khutbah. Kwa hiyo maeneo mengine yatafaa kwa kiasi cha haja kama ilivyo katika swalah ya ´iyd. Imethibiti kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) siku ua ´iyd alikuwa akitoka kwenda kiwanjani na wanyonge akiwateulia Abu Mas´uud ambaye anawaswalisha.

Kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuacha kufanya ijumaa mbili na akiwatosheleza moja ni kwa sababu Maswahabah walikuwa wakichunga kupenda kusikiliza Khutbah yake na kuona ijumaa yake ijapo nyumba zao zitakuwa mbali. Kwa sababu yeye ndiye mfikishaji kutoka kwa Allaah na kuziwekea Shari´ah hukumu mbalimbali. Wakati haja ilipopelekea kufanya hivo katika miji mbalimbali swalah ya ijumaa iliswaliwa maeneo mbalimbali na hakupinga. Hivyo ikawa ni maafikiano (إجماعا). Maneno ya Ibn ´Umar maana yake ni kwamba swalah ya ijumaa isiswaliwe katika misikiti midogo na ukaachwa ule mkubwa. Kuyazingatia hayo kwa kuiwekea mpaka ni jambo halina wajihi. Abu Daawuud amesema kuwa amemsikia Ahmad (Rahimahu Allaah) akisema:

“Madiynah kulikuwa kumewekwa mpaka gani? Musw´ab bin ´Umayr aliiswali kipindi ambapo walikuwa wamejificha katika nyumba ambapo akawakusanya wakiwa arobaini. Ama pasi na haja haifai kuiswali zaidi [ya sehemu] moja. Kukipatikana kutosheka kwa [sehemu mbili] haitosihi kufanya [sehemu nyingine ya] tatu na zenye kuzidi hapo. Hatumjui yeyote anayeona kinyume na hivo. ´Atwaa´ aliambiwa kwamba watu wa Baswrah hauwatoshi msikiti mkubwa. Akasema: “Kila watu wawe na msikiti wao wanapokusanyikia na hilo litawatosheleza kutokamana na kukusanyika katika msikiti mkubwa. Yale wanayoonelea jopo la wanazuoni wengi ndio yenye haki zaidi kwa sababu haikunakiliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makhaliyfah wake kwamba walikusanya zaidi ya ijumaa moja. Hakukuwa na haja ya kufanya hivo. Haijuzu kuthibitisha hukumu kwa kuhukumu bila ya dalili.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) aliulizwa kuhusu swalah ya ijumaa katika msikiti wa al-Qal´ah Dameski kama inafaa kwa sababu ndani ya mji kuna Khutbah nyingine?

Jibu: Ndio, inafaa kukaswali hapo swalah ya ijumaa. Kwa sababu ni kama mji mwingine kama Misri na Cairo. Hata ikiwa sio kama mji mwingine, kutekeleza swalah ya ijumaa maeneo mawili tofauti katika mji mkubwa kutokana na haja inafaa kwa mtazamo wa wanazuoni wengi. Kutokana na haya kulipojengwa Baghdaad na ikawa na pande mbili kulitekelezwa humo swalah ya ijumaa upande wa mashariki na swalah ya ijumaa nyingine upande wa magharibi. Wanazuoni wengi wamejuzisha jambo hilo.”

Kutokana na tuliyoyataja itakuwa wazi kwa muulizaji juu ya kufaa kutekeleza ijumaa mbili na zaidi katika mji mmoja ikiwa haja imepelekea kufanya hivo. Watu watafanya hivo kutokana na ufinyo wa nafasi na kutopata nafasi watu wote wa mji au kutokana na upana wa mji na kuwa mbalimbali pande zake na ugumu mkubwa juu yao katika kukusanyika kwenye msikiti mmoja. Mfano wa hilo ikiwa katika mji kuna makabila mawili na kati yao kuna migogoro na magomvi na kukakhofiwa ikiwa watakusanyika basi kutatokea fitina kati yao na mapigano, basi itafaa kwa kila kabila kukusanya wao wenyewe muda wa kuwa fitina ni yenye kuendelea. Vivyo hivyo sababu nyenginezo zinazofanana na hizo.

Hapa kuna suala jengine ambalo ni lazima kulizindua; baadhi ya watu hivi katika zama zilizokuja nyuma ikiwa katika mji mmoja kuna mikusanyiko miwili na zaidi basi wanaswali Dhuhr baada ya swalah ya ijumaa na wanadai kwamba kufanya hivo kuna kuchukua tahadhari kwa kuchelea kutosihi moja kati ya ijumaa mbili hizo. Ukweli wa mambo ni kwamba haya ni maovu ya wazi na uzushi katika Uislamu ambao kuukubali. Wamelikemea waliokutana nalo katika wale wanazuoni wakaguzi. Kwa sababu Allaah (Subhaanah) amewawajibishia waislamu katika siku ya ijumaa na nyenginezo swalah tano ilihali watu wanawawajibishia watu siku ya ijumaa kuswali swalah sita. Haijalishi kitu hata kama hawatowajibisha jambo hilo bali wamelipendekeza au kuliruhusu. Yote hayo hayajuzu. Kwa sababu ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba alikuwa akisema katika Khutbah ya ijumaa:

“Mazungumzo bora ni Kitabu cha Allaah, uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa na kila Bid´ah ni upotofu.”[6]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”[7]

Muslim ameipokea kwa tamko lisemalo:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[8]

Swalah na amani zimwendee mja na Mtume Wake Muhammad, kizazi chake, Maswahabah zake na wale watakaowafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz

Raisi wa chuo kikuu cha al-Madiynah an-Munawwarah.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/351-357).

[2] 03:103

[3] 03:105

[4] Ahmad (8444) na Maalik katika ”al-Muwattwa´” (1572).

[5] al-Mughniy (02/184).

[6] Muslim (1435) na Ibn Maajah (44).

[7] al-Bukhaariy (2499) na Muslim (3242).

[8] Muslim (3243).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 83-90
  • Imechapishwa: 06/12/2021