43. Kufaradhishwa kwa Shari´ah zengine zilizobaki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hijrah ni kutoka katika mji wa kikafiri na kwenda katika mji wa Kiislamu. Ummah huu umefaradhishiwa kufanya Hijrah kutoka katika mji wa kikafiri na kwenda katika mji wa Kiislamu na itaendelea kubaki mpaka Qiyaamah kitaposimama. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚقَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا

“Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali wamejidhulumu nafsi zao, wataulizwa: “Mlikuwa katika hali gani?” Watasema: “Tulikuwa tukikandamizwa katika ardhi”, [Malaika] watasema: “Je, kwani ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahajiri?” Basi hao makazi yao yatakuwa ni Motoni – na ubaya ulioje mahali pa kurejea! Isipokuwa wale waliokandamizwa – kati ya wanaume na wanawake na watoto – ambao hawakuweza kupata namna yoyote wala hawawezi kuongoza njia. Basi hao huenda Allaah akawasamehe – Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufiria.” (an-Nisaa´ 04:97-99)

Kauli Yake (Ta´ala):

يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ

“Enyi waja Wangu ambao mmeamini! Hakika ardhi Yangu ni pana, basi Mimi Pekee niabuduni.” (al-´Ankabuut 29:56)

al-Baghawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sababu ya kuteremka Aayah hii kwa baadhi ya waislamu Makkah ambao hawakufanya Hijrah. Hivyo Allaah amewazungumzisha kwa jina la imani.”

Dalili juu ya Hijrah kutoka katika Sunnah, ni kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hijrah haitosimama mpaka Tawbah isimamishwe. Na Tawbah haitosimamishwa mpaka jua lichomoze kutoka magharibi.”

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotulia al-Madiynah, alifaradhishiwa Shari´ah zingine za Kiislamu. Kwa mfano zakaah, swawm, hajj, adhaana, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu na Shari´ah zingine za Kiislamu. Aliyafanya haya kwa miaka kumi. Baada ya hapo akafa, lakini Dini yake imebaki.

Hii ndio Dini yake. Hakuna kheri yoyote isipokuwa amewaonesha nayo Ummah wake, na hakuna shari yoyote isipokuwa amewatahadharisha nayo. Kheri [kubwa] Aliyowaonesha nayo ni Tawhiyd na kila anachokipenda Allaah na kukiridhia. Na shari [kubwa] Aliyowatahadharisha nayo ni shirki na kila anachokichukia Allaah na kukikataa.

Allaah amemtuma kwa watu wote na Allaah akafaradhisha kwa viumbe wote – majini na watu – kumtii. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”” (al-A´raaf 07:158)

Allaah kupitia kwake ameikamilisha Dini. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni Dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio Dini yenu.” (al-Maa-idah 05:03)

Dalili ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ

“Hakika wewe ni utakufa na wao pia ni watakufa. Kisha hakika nyinyi siku ya Qiyaamah mbele ya Mola wenumtagombana.” (az-Zumar 39:30-31)

Baada ya watu kufa, watafufuliwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.” (Twaaha 20:55)

وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا

”Na Allaah amekuotesheni kutoka katika ardhi mimea; kisha atakurudisheni humo [ardhini] na atakutoeni [tena upya] mtoke.” (Nuuh 71:17-18)

Baada ya kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa matendo yao. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.” (an-Najm 53:31)

Yule mwenye kukanusha kufufuliwa anakufuru. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.” (at-Taghaabuun 64:07)

MAELEZO

Baada ya yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhajiri na kutulia al-Madiynah, ndipo akafaradhishiwa Shari´ah zengine kukiwemo zakaah, kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwa kuwa wakati huo al-Madiynah ilikuwa tayari imeshakuwa nchi ya Kiislamu na ndio makao makuu ya kwanza ya waislamu. Ndio maana wakaamrishwa hizo Shari´ah zengine zilizobaki. Huko walikuwa wanaweza kuamrisha mema na kukataza maovu. Haya ilikuwa ni huruma kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) kwamba mambo haya ya wajibu yakaanza kufanya kazi punde tu alipohamia al-Madiynah. Lakini msingi wa zakaah ulikuwa tayari umeshawekwa Makkah. Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-An´aam” iliyoteremshwa Makkah:

وَآتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

“… na mpeni haki yake [yule muhitaji] siku ya kuvunwa kwake.” (06:141)

Mipaka yake, wanaoistahiki na upambanuzi wa hukumu zake yote haya yaliteremshwa al-Madiynah. Kadhalika kufunga Ramadhaan kuliwekwa mwaka wa pili baada ya kuhajiri. Hajj iliwekwa mwaka wa tisa au wa kumi baada ya kuhajiri. Ndipo Allaah akateremsha:

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا

”Kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo wa kuiendea.” (03:97)

Aayah ipo katika Suurah “Aal ´Imraan” iliyoteremshwa al-Madiynah.

Vivyo hivyo Jihaad iliamrishwa al-Madiynah. Mwanzoni ilikuwa mtu anapambana kwa ajili tu ya kujihami. Baadaye akaamrishwa kuanza kuwapiga vita makafiri na kupambana na makafiri hata kama wao hawakumuanza. Akawalingania katika dini ya Allaah; ima waingie katika Uislamu au wanapigwa mpaka wasilimu.

Hata hivyo watu wa Kitabu walikuwa wakitaamiliwa kinyume. Walikuwa wanaweza kutozwa kodi (Jizyah) iwapo hawaingii katika Uislamu. Hata waabudu moto walikuwa wakitaamiliwa hivo; ima waingie katika Uislamu au watozwe kodi. Ama makafiri wengine wote ima waingie katika Uislamu au wapigwe vita kukiwepo uwezo.

Baada ya Allaah kuikamilisha dini kupitia kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ndipo Allaah akamfisha baada ya miaka 10 tangu kuhajiri. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni Dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio Dini yenu.” (05:03)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عِندَ رَبِّكُمْ تَخْتَصِمُونَ

Hakika wewe ni utakufa na wao pia ni watakufa. Kisha hakika nyinyi siku ya Qiyaamah mbele ya Mola wenu mtagombana.” (39:30-31)

Watu baada ya kufa watafufuliwa. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَاللَّـهُ أَنبَتَكُم مِّنَ الْأَرْضِ نَبَاتًا ثُمَّ يُعِيدُكُمْ فِيهَا وَيُخْرِجُكُمْ إِخْرَاجًا

”Na Allaah amekuotesheni kutoka katika ardhi mimea; kisha atakurudisheni humo [ardhini] na atakutoeni [tena upya] mtoke.” (71:17-18)

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.” (64:07)

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.” (53:31)

Watu watafanyiwa hesabu na kulipwa siku ya Qiyaamah. Watapewa vitabu vyao ima kwa mikono yao ya kuume au kwa mikono yao ya kushoto. Mwenye furaha atapewa kitabu chake katika mkono wake wa kulia, mwangamivu atapewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto.

Mwenye furaha mizani yake itakuwa mizito, mwangamivu mizani yake itakuwa khafifu. Watenda maasi wako katika khatari. Mizani yao inaweza kuwa na uzito ikiwa watatubia au Allaah (Subhaanah) akawasamehe au wakifanya matendo mema. Mizani yao inaweza vilevile ikawa khafifu na wakatumbukia Motoni na Allaah humo akawaadhibu kwa ule muda Allaah atataka. Halafu Allaah awatoe Motoni kwa sababu ya kufa kwao hali ya kuwa ni waislamu. Kwa hivyo ni wajibu kwa kila yule ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia ajiepushe na maasi, atubie daima na awe na msimamo wa sawa. Kwa kuwa hajui ni lini mauti yatamjia. Kwa ajili hiyo ni muhimu sana kwa muislamu kuchukua maazimio ya kweli na apambane na nafsi yake mpaka iweze kushika njia iliyonyooka na atubie kikweli juu ya madhambi yake yote. Lengo ni kuwa mauti yamjie akiwa katika hali nzuri na katika njia iliyonyooka ambapo aweze kufuzu furaha na uokozi siku ya Qiyaamah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 51-54
  • Imechapishwa: 10/02/2017