42. Mume anatakiwa awe na wivu kwa mke


Miongoni mwa haki za mke juu ya mume wake ni yeye awe na wivu kwa mke wake. Anatakiwa kuona yeye ni mwenye wivu kwake. Lakini hata hivyo inatakiwa iwe ni wivu wenye kudhibitiwa ili uweze kuleta yaliyo na kheri na kuzuia yaliyo na shari.

Anatakiwa awe na wivu kwa mke wake kukionekana kitu katika mwili wake. Anatakiwa awe na wivu kwa mke wake akiwaangalia wanaume wasio Mahram zake. Anatakiwa awe na wivu kwa mke wake akichanganyika na wanaume wasio Mahram zake. Anatakiwa awe na wivu kwa mke wake akizungumza na wanaume wasio Mahram zake pasipo haja.

Ama kuhusu wivu wa sampuli ya shaka na tuhuma zisizo na maana, hili ni haramu. Baadhi ya wanaume wanasema kuwa wana wivu na wanaanza kuwapeleleza wake zao pasina mashaka yoyote. Pale tu anapoingia nyumbani kitu cha kwanza ni kuanza kuangalia simu yake na orodha ya namba zilizopiga. Simu yake ikipiga anajongea karibu ili aweze kusikia anazungumza na nani. Anapeleleza kila kitu na kumshakia. Anapomsikia anazungumza anamuuliza:

“Unamkusudia nani?”

Anapowasikia watu wanaashiria kitu, anapata mawazo ya kwamba wanamkusudia mke wake. Yeye anamshakia tu mke wake. Anasema kuwa yeye ana wivu, lakini wivu kama huu ni haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna wivu unaopendwa na Allaah na kuna wivu unaochukiwa na Allaah. Ama kuhusu wivu unaopendwa na Allaah, ni ule wivu unaotokamana na mashaka. Kuhusu wivu unaochukiwa na Allaah, ni ule wivu unaokuwa pasina mashaka yoyote.”[1]

[1] Abu Daawuud (2659), an-Nasaaiy (2558), Ibn Hibbaan (11/4762), Ahmad (5/445) na wengine. Ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (7/2388). Mhakiki wa ”al-Musnad” [ya Ahmad] amesema:

”Nzuri kupitia zingine.” (19/156)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 24/03/2017