42. Mambo yenye kufanya imani ikazidi

Imani inazidi kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

1- Kujua majina na sifa za Allaah. Kadri ambavyo mtu atazidi kuyatambua, akajua yale inapelekea na athari yake, basi ndivyo jinsi imani na mapenzi na kumuadhimisha Mola kutakavyozidi.

2- Kuzitafakari ishara za Allaah za kilimwengu na Aayah za Kishari´ah. Kadri ambavyo mtu atazidi kuzitafakari na kuzingatia ile nguvu kubwa na hekima kubwa inayopatikana ndani yake, ndivyo jinsi imani na yakini yake itakavyozidi.

3- Kutenda matendo mema kwa kujikurubisha kwa Allaah (Ta´ala). Imani inazidi kutegemea na ule uzuri, sampuli na wingi wa matendo. Kadri ambavyo kitendo kitakuwa kizuri zaidi, ndivyo jinsi imani itavyozidi. Uzuri wa kitendo unatokana na Ikhlaasw na kule kuafikiana na Shari´ah.

Kuhusu sampuli ya kitendo, hakika cha wajibu ni bora zaidi kuliko kilichopendekezwa. Baadhi ya vitendo vimekokotezwa na ni bora zaidi kuliko vyengine. Kadri jinsi kitendo kitakuwa bora zaidi, ndivyo jinsi imani inavyozidi.

Kuhusiana na wingi wa matendo, imani inazidi kadri jinsi matendo ni mengi. Kwa sababu matendo yanaingia katika imani, si ajabu ikazidi pale ambapo mtu anazidisha matendo.

 4- Kuacha maasi kwa ajili ya kumuogopa Allaah (´Azaa wa Jall). Kila ambavyo hima ya mtu inakuwa ni yenye nguvu zaidi kufanya maasi fulani, basi ndivyo jinsi imani ya mtu inazidi kuwa na nguvu zaidi kwa kuyaacha. Mtu kuyaacha ilihali ana hima ya hali ya juu, ni dalili inayojulisha kuwa imani yake ina nguvu kabisa na kuwa anatanguliza yale anayoyapenda Allaah na Mtume Wake mbele ya yale ambayo nafsi yake inatamani.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 95
  • Imechapishwa: 15/05/2020