42. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya imani

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuwa:

Dini na Imani ni kauli na matendo. Kauli ya moyo na ulimi, na matendo ya moyo na ulimi na viungo vya mwili. Imani inazidi kwa utiifu na inashuka kwa maasi. Pamoja na hivyo, wao hawawakufurishi waislamu kwa kutenda maasi na madhambi makubwa, kama wanavyofanya Khawaarij, bali udugu wa Imani bado upo pamoja na kuwa kwa maasi. Kama Alivyosema (Subhaanahu wa Ta´ala) katika Aayah ya kisasi:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ

”Na anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema naye alipe kwa wema.” (02:178)

Na Akasema (Subhaanah):

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ

”Na mataifa [au makundi] mawili ya Waumini yakipigana, basi suluhisheni baina yao. [Lakini] mojawapo likikandamiza jengine, basi lipigeni [vita] lile linalokandamiza mpaka lielemee kwenye amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu na fanyeni haki – hakika Allaah Anapenda wafanyao haki. Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.” (49:09-10)

Hawapingi Imani ya Muislamu mtenda madhambi moja kwa moja na wala hawasemi kuwa atadumishwa Motoni milele, kama wanavyosema Mu´tazilah, bali Muislamu mtenda madhambi anaingia pia katika Imani. Kama ilivyo katika Kauli Yake (Ta´ala):

فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

”Basi [aliyeua] aachilie huru mtumwa muumini.” (04:92)

Na wakati mwingine yawezekana akawa haingii katika Imani kamilifu. Kama ilivyo katika Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

”Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu [na hushtuka] na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia iymaan.” (08:02)

Na kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, na wala hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini, na hapori mwenye kupora pindi anapopora kitu chenye thamani, jambo ambapo linafanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[1]

Tunasema: “Ni muumini mwenye Imani pungufu” au “Ni muumini akiwa na Imani yake, mtenda dhambi kwa dhambi yake kubwa.” Kwa hali hiyo hapewi Imani kamilifu na wala haikanushwi moja kwa moja.

MAELEZO

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni… – Utafiti huu ni mkubwa na ni miongoni mwa I´tiqaad za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wanasema kuwa imani ni maneno na vitendo. Maneno ya moyo na ulimi, matendo ya moyo na viungo vya mwili. Haya ndio wanayoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hili ni tofauti na Murji-ah, Mu´tazilah na Khawaarij. Khawaarij wanayakubali haya, lakini wanasema kuwa imani haizidi wala haipungui. Kadhalika Mu´tazilah wanasema kuwa imani haizidi wala haipungui. Wanasema kuhusu imani ima iwepo yote na ikibidi kuondoka inaondoka yote. Kwa ajili hii ndio maana wamemkufurisha mtenda madhambi na kuonelea kuwa ni mwenye kudumishwa Motoni milele. Mu´tazilah pia wamekubaliana nao juu ya hilo inapokuja katika hukumu ya Aakhirah na kwamba mtenda madhambi atadumishwa Motoni milele. Murji-ah wao wameyandosha matendo katika imani na kusema kuwa imani ni kutamka au kusadikisha peke yake. Mapote yote haya yaliyotajwa yamekosea na kupotea kutoka kwenye Njia.

Sahihi ni yale waliyomo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambapo wanasema kuwa imani ni maneno na vitendo, maneno ya moyo na ulimi, vitendo vya moyo na viungo vya mwili.

Mfano wa matendo ya moyo ni kama kumpenda Allaah, kumuogopa, kumtakasia ´ibaadah, kusadikisha, kusadikisha kwa maneno, Tasbiyh, Tahliyl na Dhikr.

Mfano wa matendo ya viungo vya mwili ni kama swalah, zakaah, swawm, hajj na Jihaad. Namna hii ndivyo wanavyoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ya kwamba imani ni maneno na matendo, inazidi kwa kufanya mambo ya utiifu na inapungua kwa kufanya mambo ya maasi. Msemo wenye kusema:

“Imani ni maneno na matendo.”

wanaingia ndani yake Khawaarij na Mu´tazilah. Msemo wenye kusema:

“Imani inazidi kwa kufanya mambo ya utiifu na inapungua kwa kufanya mambo ya maasi.”

Mu´tazilah na Khawaarij wanatoka. Ni Radd kwao. Msemo wenye kusema:

“Imani ni maneno na matendo.”

Murji-ah vilevile wanatoka.

Ni wajibu kwa muumini aamini ´Aqiydah hii na atendee kazi muqtadha yake.

Hawapingi Imani ya Muislamu mtenda madhambi… – Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamoja vilevile na kutompokonya imani muislamu mtenda dhambi ambaye anajinasibisha na Uislamu. Hawaonelei vilevile kuwa atadumishwa Motoni milele. Khawaarij ndio wanampokonya imani yote. Mu´tazilah wanaonelea kuwa atadumishwa Motoni milele. Muislamu mtenda dhambi anaingia katika imani. Kwa mfano Kauli Yake (Ta´ala):

فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

”Basi [aliyeua] aachilie huru mtumwa muumini.” (04:92)

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا حَتَّىٰ إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّوا أَن لَّا مَلْجَأَ مِنَ اللَّـهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ

“Na [pia Allaah Akapokea tawbah] ya wale watatu waliobaki nyuma [kutokwenda vita vya Tabuwk wakajuta mno] mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana na zikadhikika nafsi zao, na wakatambua kwamba hakuna pa kumkimbia Allaah isipokuwa Kwake; kisha [Allaah] Akapokea tawbah yao ili watubie. Hakika Allaah Yeye Ndiye Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli.” (09:119)

Anaingia ndani ya wito huu ambao wanazungumzishwa wale walioamini. Ama sehemu za matapo na sifa hawi mwenye kuingia. Kauli Yake (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا

”Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu [na hushtuka] na wanaposomewa Aayah Zake huwazidishia iymaan.”(08:02)

Kadhalika haingii katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba pindi anapoiba hali ya kuwa ni muumini, na wala hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini, na hapori mwenye kupora pindi anapopora kitu chenye thamani, jambo ambapo linafanya watu kumwangalia kwa ajili ya hilo, hali ya kuwa ni muumini.”[2]

Vilevile dalili nyenginezo mfano wa hizo.

Kwa haya inapata kujulikana ya kwamba muumini mwenye imani kamilifu haingii katika mkumbo wenye kulaumiwa. Upande mwingine muumini mwenye imani pungufu anaingia katika mkumbo wenye kulaumiwa:

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba… “

Kwa sababu imani yake ni pungufu. Tunapozungumzia waumini wenye imani kamilifu waislamu watenda madhambi wanatoka humo.

Wasifu wa imani ni yule muislamu ambaye anazungumzishwa kutokana na imani yake. Hivyo muislamu mtenda dhambi kuna uwezekano akaingia katika Kauli Yake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا

“Enyi mlioamini.” (02:104)

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

“Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.” (03:19)

Vivyo hivyo akaingia katika maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muislamu ni ndugu ya Muislamu mwenzake.”[3]

Anaingia humu muislamu mtenda dhambi na asiyekuwa mtenda dhambi. Lakini kunapotajwa imani kamilifu yenye kuambatana na matapo muislamu mtenda dhambi haingii humo. Lakini kunapotajwa imani isiyofungamanishwa muislamu mtenda dhambi anaingia humo. Kama ilivyotangulia hapo mbele kwa mfano Kauli Yake:

فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ

“… na anayesamehewa na nduguye kwa lolote… ” (02:178)

Muuaji ameitwa kuwa ni ndugu.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

“Hakika Waumini ni ndugu.” (49:10)

Wameitwa kuwa ni ndugu pamoja na kuwa wamepigana vita.

Kwa ufupi ni kwamba muislamu mtenda dhambi anaingia katika imani isiyofungamanishwa:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا

“Enyi mlioamini!” (49:11)

وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ

“Na atakayemuua muumini kwa kukosea basi aachilie huru mtumwa Muumin.” (04:92)

Kuna Aayah nyenginezo mfano wa hizi.

Sambamba na hilo haingii katika imani kamilifu ambayo watu wake wamesifiwa. Kwa mfano Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

“Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao, zinajaa khofu [na kushtuka] wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan na kwa Mola wao wanategemea. Ambao wanasimamisha Swalah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa.” (08:02-03)

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hazini mwenye kuzini pindi anapozini hali ya kuwa ni muumini, na wala haibi mwenye kuimba… “

Utenda dhambi wake umefanya akakosa imani kamilifu. Mtu sampuli hii huitwa muislamu, muumini mwenye imani pungufu au pia mtu anaweza kusema kuwa ni muumini kutokana na imani alionayo na ni mtenda dhambi kutokana na dhambi yake kubwa. Hivyo anawakuwa hakupewa jina la muumini isiyofungamanishwa na wala anakuwa hakupokonywa nalo. Mtu kama huyu mtu hafai kusema kuwa ni muumini mwenye imani kamilifu kama ambavyo haitakikani vilevile kusema kuwa sio muumini. Isipokuwa ikiwa kama mtu anakusudia kuwa sio muumini mwenye imani kamilifu.

Kwa haya wanaraddiwa Mu´tazilah na Khawaarij na mtu anabaki kuwa ni muumini kwa mujibu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah inapokuja katika mlango huu mkubwa ambao wasomi wengi wamepotea kwao.

[1] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[2] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[3] al-Bukhaariy (2442) na Muslim (2580)

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com