42. Du´aa wakati wa kikao


177- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayekaa katika kikao na kuzungumza sana na akasema kabla ya kusimama katika kikao hicho:

سُبْحانَكَ اللهُمَّ وَبِحَمْدِكَ أَشْهَدُ أَنْ لا إِله إِلا أَنْتَ أَسْتَغْفِرُكَ وَأَتُوبُ إِلَيْكَ

“Kutakasika ni Kwako na himdi ni Zako. Nashuhudia kwamba hakuna mola anayeabudiwa kwa haki ila Wewe. Ninakuomba msamaha na kutubia Kwako.”

isipokuwa Allaah Humsamehe yaliyokuwa katika kikao hicho.”

178- Katika Hadiyth nyingine:

“Ikiwa ni kikao kizuri inakuwa ni kama muhuri chake. Na ikiwa ni kikao cha kuchanganyika inakuwa ni kafara kwake.”

179- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna watu ambao wanasimama kutoka kwenye kikao pasina kumdhukuru Allaah (Ta´ala) hapo isipokuwa ni kama wamesimama kutoka kwenye mzoga wa punda. Ni khasara kwao.”

180- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Ni nadra Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anasimama kutoka kwenye kikao isipokuwa anawaombea Maswahabah zake Du´aa hii:

اللهُمَّ اقسم لَنَا من خَشْيَتِكَ ما تَحولُ به بيننا وبينَ مَعَاصيك وَمن طَاعَتكَ ما تُبَلِّغُنَا به جَنَّتَك وَمِنَ الْيقين ما تَهُوِّن به عَلَيْنَا مصائِبَ الدُّنْيا اللهُمَّ مُتَّعْنَا بِأَسْمَاعِنَا وأَبْصَارِنَا وَقُوَّتِنَا مَا أَحْيَيْتَنَا واجْعَلْهُ الوارثَ مِنَّا واجْعَلْ ثَأْرَنَا على مَنْ ظَلَمَنَا وانْصُرْنَا على منْ عَادَانا وَلاَ تَجْعَل مُصِيبتنَا في ديننا وَلاَ تَجْعَل الدُّنْيَا أَكْبَرَ هَمِّنَا وَلا مبلَغَ عِلْمِنَا وَلا تُسَلِّطْ عَلَيْنَا من لا يَرْحَمُنَا

“Ee Allaah! Tugawie kukuogopa ambako kutatuzuia baina yetu sisi na kukuasi, kukutii ambako kutatufikisha sisi katika Pepo Yako na yakini ambayo itaturahisishia matatizo ya dunia. Ee Allaah! Tupe ladha katika usikizi wetu, uoni wetu na nguvu zetu maadamu ni Mwenye kutufanya bado tuhai. Vifanye ni vyenye kubaki na sisi[1]. Tufanye ni wenye kulipiza kisasi kwa wale wenye kutudhulumu. Tunusuru dhidi ya maadui zetu. Usifanye msiba wetu ukawa katika Dini yetu. Usiifanye dunia ikawa ndio hamu yetu kubwa wala kubwa katika elimu yetu. Usitutawalishie wale wasiokuwa na huruma juu yetu.”

[1] Yaani salama na afya mpaka tutapokufa.

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 109-111
  • Imechapishwa: 21/03/2017