40. Mwenye busara na kuvipa kisogo vya watu


1 – Sahl bin Sa´d amesema:

”Kuna bwana mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nifunze kitendo ambacho nikikifanya basi Allaah atanipenda na watu watanipenda.” Akasema: ”Ipe nyongo dunia Allaah atakupenda. Vipe nyongo vile vilivyoko mikononi mwa watu watu watakupenda.”

2 – Ni lazima kwa yule mwenye busara kuacha kutamani vilivyoko kwa watu kikamilifu na kuwakatia tamaa. Ni ufukara kutazama kitu ambacho hakuna mashaka yoyote juu ya uwepo wake. Mtu aseme nini juu ya kile ambacho kuna mashaka juu ya kuwepo kwake?

3 – Sa´d bin ´Amaarah amesema:

”Ee mwanangu kipenzi! Onyesha kukata tamaa, kwani ni utajiri. Nakutadharisha kutazama vya watu. Ni ufukara.”

4 – Jitihada tukufu zaidi ni kule kuacha kutamani vya watu. Hana utajiri yule anayetamani vitu vya watu.  Yule mwenye kuacha kutamani vya watu amekusanya utukufu na heshima ya juu kabisa. Pepo kwa yule ambaye nembo ya moyo wake ni uchaji na macho yake hayakupofoka kwa kuangalia vya watu!

5 – Yule anayependa kuwa huru basi asitamani kisicho chake. Kwani kutamani ni umasikini kama ambavo kukata tamaa ni utajiri. Anayetamani hudhalilishwa na kutwezwa kama ambavo anayekinai hujizuia na akajitosheleza.

6 – Ahmad bin Hanbal alimsikia Ibn-us-Simaak akisema:

”Matarajio ni kamba moyoni mwako na minyororo mguuni mwako. Hivyo basi, ondosha matarajio moyoni mwako itafunguka minyororo mguuni mwako.”

7 – Mwenye busara hatamani yale walionayo marafiki zake. Ni udhalilishaji. Mwenye busara anataka tamaa juu ya adui. Ni uokozi.

8 – Ukataji tamaa ni jeraha la raha na utukufu. Tamaa ni jeraha la uchovu na udhalilishaji. Ni wangapi waliotamani wamechoka na kujidhalilisha pasi na kufikia malengo yao? Ni wangapi waliokata tamaa walipumzika na kutukuzwa na aidha wakapata yale waliyoyataka na ambayo hawakuyataka?

9 – Abu Ja´far amesema:

”Kukata tamaa juu ya vile vilivyoko kwa watu ni utukufu.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 141-144
  • Imechapishwa: 08/08/2021