40. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya maombezi

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Mtu wa kwanza ambaye atafunguliwa mlango wa Pepo ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wa kwanza ambao wataingia Peponi ni Ummah wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Atakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah na nyombezi tatu. Ama uombezi wa kwanza atawaombea waliosimamishwa na kusubiri wahukumiwe baada ya Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysa bin Maryam kutoa udhuru wa kuombea, mpaka itaishia kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama uombezi wa pili atawaombea watu wa Peponi waingie Peponi – na nyombezi hizi mbili ni maalum kwake. Ama uombezi wa tatu atawaombea wale waliostahiki kuingia Motoni. Na uombezi huu ni kwake na kwa Mitume wengine, wakweli na wengineo. Atawaombea wale waliostahiki kuingia Motoni wasiingizwe na awaombee wale walioingia watolewe humo. Allaah (Ta´ala) Atawatoa ndani ya Moto watu si kwa sababu ya uombezi, bali ni kwa sababu ya fadhila na huruma Wake. Kutabaki Peponi nafasi baada ya watu walioingia na Allaah Ataumba watu maalum kwa ajili yake kisha Awaingize Peponi. Hatua hizi mbali mbali zinazokuja kuhusu Nyumba ya ´Aakhirah, hesabu na thawabu, Pepo na Moto.

Ufafanuzi zaidi wa hilo umetajwa katika Vitabu vilivyoteremshwa kutoka mbinguni na Aathaar ya elimu iliyopokelewa kutoka kwa Mitume. Na katika elimu iliyorithiwa kutoka kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), katika hayo kuna yanayokinaisha na kutosheleza, yule mwenye kutafuta atapata.

MAELEZO

Mwandishi (Rahimahu Allaah) anasema:

Mtu wa kwanza ambaye atafunguliwa mlango wa Pepo ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ndiye Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameamrisha asifunguliwe yeyote kabla yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye mtu wa kwanza atayefunguliwa mlango wake na kubisha hodi. Mlinzi wa Pepo atamwambia kwamba niliamrishwa nisimfungulie yeyote kabla yako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtu wa kwanza ambaye atafunguliwa mlango wa Pepo ni Muhammad… – Ummah wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio utakuwa wa kwanza kuingia Peponi. Baada ya Mitume Ummah bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ummah wa kwanza miongoni mwa nyumati utaoingia Peponi na ulio bora baada ya Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) ni Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Nyombezi tatu za Mtume (´alayis-Salaam)

Atakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Qiyaamah na nyombezi tatu… – Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakuwa na nyombezi tatu:

Mosi: Uombezi mkubwa juu ya wataokuwa wamesimamishwa uwanjani ili wahukumiwe na kufanyiwa hesabu. Haya yatakuwa baada ya Mitume wengine kuomba udhuru; Aadam, Nuuh, Ibraahiym, Muusa na ´Iysaa mwana wa Maryam. Pindi kisimamo kitakuwa kizito kwa watu watamwendea Aadam (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Watasema kumwambia:

“Ee Aadam! Hakika wewe ndiye kiumbe cha kwanza. Allaah amekuumba kwa Mkono Wake, akakupulizia roho, Malaika wakakusujudia na akakufunza majina ya kila kitu. Hivyo tunakuomba utuombee kwa Mola Wako. Hivi kweli huoni tuliyomo? Hivi kweli huoni hali ilipofikia?”

Bi maana matatizo na magumu.

Aseme (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Mimi siistahiki. Hakika Mola Wangu ameghadhibika leo ghadhabu ambayo hajapatapo kughadhibika kabla yake na hatoghadhibika mfano wake baada ya leo.”

Baada ya hapo atataja makosa yake ya kwamba alikula kwenye mti. Alitubu kwa kosa hili, lakini hata hivyo haya ni kutokana na unyenyekevu wa hali ya juu walionao Mitume, khofu na imani yao kamilifu (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Atawaambia:

“Nendeni kwa Nuuh.”

Halafu wataenda kwa Nuuh (´alayhimis-Swalaatu was-Salaam) na kumwambia:

“Wewe ndiye Mtume wa kwanza uliyetumwa katika ardhi.”

Bi maana Mtume wa kwanza baada ya kutokea shirki kati yao. Watamwambia:

“Hakika Allaah amekwita kuwa ni “mja mwenye kushukuru. Hivi kweli huoni hali tuliyomo? Tuombee kwa Mola Wako. Hakika Mola Wangu ameghadhibika leo ghadhabu ambayo hajapatapo kughadhibika kabla yake na hatoghadhibika mfano wake baada ya leo.”

Atawaambia jinsi alivyoomba du´aa dhidi ya Ummah wake ambapo awaambie:

“Nendeni kwa Ibraahiym. Watapoenda kwa Ibraahiym awaambie vivyo hivyo. Hakika Mola Wangu ameghadhibika leo ghadhabu ambayo hajapatapo kughadhibika kabla yake na hatoghadhibika mfano wake baada ya leo.” Awaambia jinsi alivyosema uongo mara tatu:

إِنِّي سَقِيمٌ

“Hakika mimi ni mgonjwa.” (37:89)

بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَـٰذَا

“Bali amefanya hayo hili [sanamu] kubwa lao.” (21:63)

Halafu atawaambia waende kwa Muusa. Waende kwa Muusa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) ambapo atawaambia vivyo hivyo. Hakika Mola Wangu ameghadhibika leo ghadhabu ambayo hajapatapo kughadhibika kabla yake na hatoghadhibika mfano wake baada ya leo. Mimi niliua nafsi ambayo sikuamrishwa kuiua. Hivyo nendeni kwa ´Iysaa (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Waende kwa ´Iysaa na kumwambia: “Tuombee kwa Mola Wako ambapo atawataka udhuru na kuwaambia kama walivyosema wa kabla yake. Hakika Mola Wangu ameghadhibika leo ghadhabu ambayo hajapatapo kughadhibika kabla yake na hatoghadhibika mfano wake baada ya leo. Hivyo nendeni kwa Muhammad, kwani yeye ni mja ambaye amesamehewa madhambi aliyoyatanguliza na yaliyoko mbele. Wataenda kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo atasema:

“Mimi ndiye mwenye kuistahiki. Mimi ndiye mwenye kuistahiki. Baada ya hapo aende kwa Mola Wake asujudu chini ya ´Arshi mbele ya Mola Wake. Amsifu kwa himdi kubwa ili Allaah amruhusu. Kisha baada ya hapo aambiwe:

“Ee Muhammad! Inua kichwa chako, sema utasikizwa, omba utapewa na shufaia utapewa uombezi. Halafu awaombee waliosimamishwa uwanjani ili wahukumiwe”.”

Pili: Atawaombea watu wa Peponi ili waingizwe Peponi.

Tatu: Atawaombea watu walioingia Motoni kwa sababu ya madhambi na maasi yao baada ya Allaah kuwaadhibu awaondoshe Motoni. Atawaombea mara nne (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kila mara atapoombea watatolewa kundi la watu. Haya yametajwa katika “as-Swahiyh”[1].

Ama uombezi wa tatu atawaombea wale waliostahiki kuingia Motoni… Mitume, waumini na watu wa kawaida na wao pia wataombea, kama alivyosema mwandishi. Ufafanuzi juu ya yatayopitika siku ya Qiyaamah ni mambo mazito.

Allaah (Ta´ala) Atawatoa ndani ya Moto watu si kwa sababu ya uombezi… – Watabaki Motoni baadhi ya wapwekeshaji ambao hawakupata uombezi. Hawa ni wale watenda madhambi waliokuwa wakimuabudu Allaah peke yake ambao wameingia Motoni kwa sababu ya madhambi yao. Hata hivyo Allaah (Jalla wa ´Alaa) atawatoa Motoni kwa fadhila na huruma Wake pasi na uombezi wa yeyote. Hawa ndio wataokuwa wamebaki Motoni na watakuwa wameungua na Moto. Baada ya hapo watawekwa kwenye mto wa uhai na wachipuke kama inavyochipuka punje kwenye kokwa lake. Litapotimia umbile lao Allaah atawaingiza Peponi kwa fadhila na huruma Wake (Subhnaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote ambaye alikuwa anamuabudu Allaah peke yake ambaye atabaki Motoni. Wataobaki tu ni makafiri ambao Allaah amewafaradhishia kudumu humo milele. Amesema (Ta´ala):

كَذَٰلِكَ يُرِيهِمُ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ حَسَرَاتٍ عَلَيْهِمْ ۖ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنَ النَّارِ

“Hivyo ndivyo Allaah Atakavyowaonyesha ‘amali zao kuwa ni majuto juu yao na wala hawatokuwa wenye kutoka Motoni.” (02:167)

كُلَّمَا خَبَتْ زِدْنَاهُمْ سَعِيرًا

“Kila ukififia Tunawazidishia [Moto wa] Sa’iyraa.” (17:97)

فَذُوقُوا فَلَن نَّزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا

“Basi onjeni [malipo yenu], kwani Hatutokuzidishieni chochote isipokuwa adhabu.” (78:30)

يُرِيدُونَ أَن يَخْرُجُوا مِنَ النَّارِ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنْهَا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ

“Watataka kutoka katika Moto lakini wao si wenye kutoka kamwe humo, na watapata adhabu ya kudumu.” (05:37)

وَهُمْ يَصْطَرِخُونَ فِيهَا رَبَّنَا أَخْرِجْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا غَيْرَ الَّذِي كُنَّا نَعْمَلُ

“Nao watapiga mayowe humo [watasema]: “Mola wetu! Tutoe tutende mema mbali na ya yale tulokuwa tukitenda… ”

Bi maana duniani. Allaah (´Azza wa Jall) awaambie:

أَوَلَمْ نُعَمِّرْكُم مَّا يَتَذَكَّرُ فِيهِ مَن تَذَكَّرَ وَجَاءَكُمُ النَّذِيرُ ۖ فَذُوقُوا فَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ

“Je, kwani Hatukukupeni umri wa kukumbuka mwenye kukumbuka humo? Na alikujieni mwonyaji. Basi onjeni [adhabu], kwani madhalimu hawana yeyote yule wa kuwanusuru.” (35:37)

Hii ndio itakuwa hali yao na mwisho wao. Ni adhabu kali – tunamuomba Allaah afya. Wataadhibiwa milele kwenye Moto usiokatika na hawatotolewa humo na ni Moto ambao hautozima.

Ufafanuzi zaidi wa hilo umetajwa katika Vitabu vilivyoteremshwa… – Kuhusiana na ufafanuzi juu ya siku ya Qiyaamah, mizani, hali za mizani na uzito wake, namna ambavyo madaftari pia yatapimwa na mengineyo yote haya yametajwa katika Qur-aan na katika Hadiyth ambazo ni Swahiyh. Mwenye kuyataka kwa kina anaweza kuyapata. Tunamuomba Allaah usalama. Hakuna uwezo wala nguvu isipokuwa kwa Allaah.

[1] al-Bukhaariy (6565) na Muslim (192).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com