39. I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya Hodhi na Njia

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika kiwanja cha Qiyaamah kutakuwa hodhi iliyotajwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maji yake ni meupe kuliko maziwa na matamu kuliko asali. Vikombe vyake ni wingi wa idadi ya nyota mbinguni na urefu na upana wake ni sawa na mwendo wa mwezi. Anayekunywa humo mara moja, hatopata kiu baada yake kamwe.

Njia imewekwa juu ya Jahannam na ni daraja iliyo baina ya Pepo na Moto. Watu watapita juu yake kadiri ya matendo yao. Kuna ambao watapita kama kufumba na kufumbua, wengine kama umeme, wengine kama upepo, wengine kama mpanda farasi, wengine kama mwenye kusafiri kwa ngamia, wengine kama mkimbiaji, wengine kama watembeaji, wengine kama mtambaaji na wengine watashikwa na kutupwa Motoni. Yule atakayevuka Njia ataingia Peponi. Watapoivuka watasimama kwenye daraja baina ya Pepo na Moto na kulipizana kisasi wao kwa wao. Baada ya kusafishwa, watapewa idhini ya kuingia Peponi.

MAELEZO

Katika kiwanja cha Qiyaamah kutakuwa hodhi… – Huu ni utafiti wenye kuzungumzia kuhusu Hodhi na Njia. Hodhi hii itakuwa ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ndio ile inayoitwa al-Kawthar:

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ

“Hakika Sisi Tumekupa [mto wa] al-Kawthar.” (108:01)

al-Kawthar ni mto uliopo Peponi. Hodhi hii ina mifereji miwili ya al-Kawthar. Hodhi hii iko duniani ardhini. Ni Hodhi itaendewa na waumini ambao ni wafuasi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Urefu na upana wake ni mwezi. Vikombe vyake ni sawa na idadi ya nyota mbinguni. Maji yake ni meupe sana kushinda maziwa na ladha yake ni matamu zaidi kushinda asali. Mwenye kunywa humo basi hatohisi kiu kamwe mpaka pale atapoingia Peponi. Waumini wataufikia na kunywa ndani yake. Hili linahusiana na wale wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna watu ambao watafukuzwa. Kisha ataulizwa Mola ambapo atasema:

“Hakika hawa walibaki ni wenye kuritadi tangu ulipofarakana nao.”

Kwa hivyo watazuia kuifikia. Baada ya hapo aseme (´alayhis-Swalaatu was-Salaam):

“Atokomee! Atokomee yule aliyebadilisha baada yangu!”[1]

Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa Hodhi hii itaendewa tu na waumini ambao wamekufa na hali ya kuwa wanamfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanafuata dini yake.

Kuhusu walioritadi baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au wakati mwingine wowote hawa hawatoifikia Hodhi hii. Vilevile inahusiana na makafiri wengine wote hawatoweza kuifikia Hodhi hii. Wataifikia tu waumini miongoni mwa wafuasi wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mitume wengine (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam) nao pia watakuwa na Hodhi zao[2]. Lakini hata hivyo Hodhi yake yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio kamilifu na yenye kutimia zaidi. Watafukuzwa kwenye Hodhi yake wasiokuwa katika kizazi chake kama inavyofukuzwa ngamia geni. Hakuna watayoifikia isipokuwa tu wale waumini ambao ni wakweli. Ama walioritadi hawana fungu kwayo. Hakuna nguvu wala uwezo isipokuwa kwa Allaah. Tunamuomba Allaah sote atujaalie kuwa miongoni mwa wataoifikia.

Njia imewekwa juu ya Jahannam… – Njia itawekwa juu ya Moto wa Jahannam. Atayeanguka kwenye Njia hii anatumbukia Motoni. Njia hii itapitiwa juu yake na kila mwenye kuingia Peponi. Amesema (Ta´ala):

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا

“Na hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ataufikia. Hiyo kwa Mola wako ni hukumu ya lazima kutimizwa. Kisha Tutawaokoa wale waliokuwa na taqwa na Tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.” (19:71-72)

Waumini watapita na kuokoka. Wasiokuwa waumini hawatopita. Kinyume chake wataanguka Motoni.

Kuna ambao watapita kama kufumba na kufumbua… – Wale wataopita juu ya Njia hii kuna waumini ambao watapita kama kufumba na kufumbua. Wengine watapita kama umeme, wengine kama mpanda farasi, wengine kama upepo na wengine kama ngamia. Kila mmoja atapita juu yake kutegemea na vile matendo yake yalivyo. Vilevile kuna wengine watapita kwa kujikongoja; mara amesimama na wakati mwingine anajikwaa. Kuna wengine watapita na kutumbukizwa Motoni. Kila mmoja atapita kutegemea na matendo aliokuwa juu yake. Waumini wakweli tu ndio wataokoka. Waliosalia watatupwa Motoni. Kuna ambao utawaonja kidogo lakini hatimaye watasalimika. Kuna wengine watatumbukia humo na kuadhibiwa kwa kiwango cha madhambi yao na halafu baadaye Allaah awatoe Motoni na kuwaingiza Motoni. Hakuna atayedumishwa Motoni milele isipokuwa makafiri peke yao.

Kuhusiana na waislamu watenda madhambi wataotumbukia humo wataadhibiwa kwa muda fulani kila mmoja kwa kiasi cha madhambi yake. Kisha Allaah atawapa idhini waombezi wawaombee. Miongoni mwa watu hao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye atawaombea halafu watolewe Motoni. Ataombea nyombezi nne. Kila uombezi Allaah atampa idadi ya watu maalum ambao watatolewa Motoni. Baada ya hapo Motoni kutabaki watu katika Ummah huu ambao hawakupata uombezi wowote. Pamoja na hivyo Allaah atawatoa humo kutokana na fadhila na huruma Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Atawatoa Motoni na kuwaingiza Peponi. Watawekwa kwenye mto wa uhai. Mto huo unaitwa “mto wa uhai”. Wakiwekwa humo watachipuka kama inavyochipuka punje kwenye kijiwavu cha kokwa. Umbile lao likitimia ndipo wataidhinishwa sasa kuingia Peponi.

Uwajibu wa kujibidisha na njia za salama na uokovu

Kwa haya muumini anapata kujua kuwa ni wajibu kwake kupupia juu ya kutafuta sababu za usalama na kwamba hili ni khatari kubwa, sawa yanayohusu Hodhi na Njia. Ni wajibu kwake kumuomba Allaah mwisho mwema. Vilevile ajitahidi kuwa na uthabiti katika haki na awe na msimamo juu yake. Sambamba na hilo atahadhari na kumuasi Allaah (´Azza wa Jall) na akimbilie kutubia. Kila mwenye kutekeleza akimbilie kutubu. Hakuna yeyote aliyekingwa na kukosea. Lakini pamoja na hivyo ni lazima kuleta tawbah. Kila atapofanya mapungufu au dhambi akimbilie kufanya tawbah.

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ

“Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao, humdhukuru Allaah wakaomba msamaha kwa madhambi yao. Na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua. Hao jazaa yao ni msamaha kutoka kwa Mola wao na Pepo zipitazo chini yake mito – ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje ujira wa watendaji wema!” (03:135-136)

Muumini anatakiwa kuihesabu nafsi yake siku zote, aichunge na kuipeleleza. Matendo yasimtie jeuri na kumfanya akajiaminisha. Badala yake anatakiwa kuihesabu nafsi yake na kupambana nayo. Huenda kwa kufanya hayo akasalimika.

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

“Na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika kwa Mola wao ni wenye kurejea. Hao wanakimbilia katika kufanya kheri nyingi; nao wao katika hayo watawatangulia [wengine].” (23:60-61)

Ibn Abiy Mulaykah amesema:

“Nilikutana na Maswahabah thelathini wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wote walikuwa wanachelea unafiki juu ya nafsi zao. Hakukuwa miongoni mwao mwenye kusema kwamba ana imani kama ya Jibriyl na Mikaaiyl.”[3]

Ibraahiym bin Yaziyd at-Taymiymiy amesema:

“Sikufanya kitendo chochote isipokuwa nilichelea nisije kuwa mwongo.”[4]

Lililo wajibu ni kuhadhari na mtu asijiamini na kujiona kutokana na matendo. Hakika Allaah anakubali tu kutoka kwa wachaji Allaah. Mtu apambane na nafsi yake. Atambue mapungufu na kasoro zake ili aweze kujitahidi, aijue haki na alazimiane na tawbah mpaka pale atapokutana na Mola Wake.

[1] al-Bukhaariy (4625) na Muslim (2860)

[2] at-Tirmidhiy (2443). Ni nzuri kwa mujibu wa Imaam al-Albaaniy katika “as-Swahiyh” (1589).

[3] Ameipokea al-Bukhaariy na kuiwekea taaliki (47-48)

[4] Ameipokea al-Bukhaariy na kuiwekea taaliki (47-48)

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com