38. Haiyumkiniki kuelezea namna alivyo Allaah


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Maelezo hayawezi kuelezea namna zilivyo sifa Zake.

MAELEZO

Bi maana hakuna yeyote anayetambua namna zilivyo sifa Zake. Hata hivyo maana yake ni yenye kutambulika. Kwa msemo mwingine maneno, usikizi, uoni na sifa nyenginezo hazitakiwi kufanyiwa namna. Tunaziamini na kuzithibitisha pasi na kutambua namna yake. Majina na sifa maana yake ni yenye kutambulika. Lakini namna yake hakuna yeyote anayejua zilivyo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee. Kwa hiyo usiulize ni namna gani alivyolingana, kwani hatujui namna yake. Bwana mmoja alimuuliza Imaam Maalik (Rahimahu Allaah):

“Ee Abu ´Abdillaah!

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

Amelingana vipi?”

Akainamisha kichwa chake chini kwa muda fulani na akipigapiga bakora yake kwenye ardhi na huku akianza kutokwa na jasho. Kisha akakiinua, akatupa bakora yake na kusema: “Kulingana kunajulikana. Namna haijulikani. Kuamini hilo ni jambo la lazima na kuulizia juu yake ni Bid´ah. Na mimi sikuoni vyenginevyo isipokuwa ni mzushi.” Kisha akaamrishwa atolewe nje.

Alitokwa na kijasho kwa sababu ya khofu yake kwa Allaah (´Azza wa Jall), kwa sababu swali hilo halimstahikii Allaah. Kulingana kunajulikana maana yake kwamba ni kuwa juu ya ´Arshi. Namna haijulikani bi maana namna yake haijulikani. Salaf na wanachuoni hawakuwa wakiuliza kuhusu namna; walichokuwa wanauliza ni maana yake tu. Mwishowe akasema:

“Na mimi sikuoni vyenginevyo isipokuwa ni mzushi.”

Halafu akaamrisha akatolewa nje. Haya ndio malipo ya yule ambaye ana ujasiri kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na akauliza juu ya mambo yasiyofaa kuulizwa.

[1] 20:05

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 26/07/2021