37. Sura ya pili: Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kuhusu majina na sifa za Allaah

2- Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah katika wema waliotangulia na waliowafuata wanamthibitishia majina na sifa za Allaah kama yalivyokuja katika Qur-aan na Sunnah na wanaujenga mfumo wao juu ya kanuni zifuatazo:

1- Wanathibitisha majina na sifa za Allaah kama zilivyokuja katika Qur-aan na Sunnah kwa udhahiri wake na ile maana inayofahamishwa na matamko yake. Hawapindishi maana kuyaondoa kutoka katika udhahiri wake na wala hawapotoshi matamshi yake na dalili zake kutoka mahala pake.

2- Wanayakanushia kufanana na sifa za viumbe. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

3- Hawavuki yale yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah katika kuthibitisha majina na sifa za Allaah. Yale yaliyothibitishwa na Allaah na Mtume Wake katika hayo nao wanayathibitisha. Yale yaliyokanushwa na Allaah na Mtume Wake nao wanayakanusha. Yale ambayo Allaah na Mtume Wake wameyanyamazia nao wanayanyamazia.

4- Wanaona kuwa maandiko ya majina na sifa za Allaah ni katika Aayah zilizo wazi ambazo inafahamika maana yake na kufasiriwa. Sio katika zile Aayah zisizokuwa wazi. Hawategemezi maana yake, kama wanavyowanasibishia jambo hilo wale wanaowasemea uongo au hawakujua mfumo wao kutoka kwa baadhi ya watunzi na waandishi wa vitabu wa kisasa.

5- Wanategemeza namna ya sifa kwa Allaah (Ta´ala) na wala hawazipekui.

[1] 42:11

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 68
  • Imechapishwa: 02/03/2020