37. Mwenye busara na hasadi


1 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Msichukiane. Msihusudiane. Msipeane migongo. Kuweni waja wa Allaah ndugu.”

2 – Ni lazima kwa mwenye busara kujitenga mbali na hasadi kwa hali zote. Sifa iliyo nyepesi zaidi ya hasadi ni mtu kutoridhia makadirio ya Allaah na kutaka kwake vengine kinyume na vile alivoamua Allaah (Jalla wa ´Alaa) juu ya waja Wake na kutamani neema iondoke kutoka kwa muislamu.

3 – Roho na mwili wa hasidi havipumziki mpaka pale atakapoona neema imeondoka kutoka kwa ndugu yake.

4 – ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

“Hakuna yeyote aliye na neema isipokuwa kuna mwenye kumuhusudu.”

5 – Muhammad bin Siyriyn amesema:

“Sijapatapo kumuhusudu mtu juu ya kitu cha kidunia. Ni vipi nitamuhusudu kwa kitu cha kidunia ikiwa mtu huyo ni katika watu wa Peponi na yeye yuko njiani kuelekea huko Peponi? Ni vipi nitamuhusudu kwa kitu cha kidunia ikiwa mtu huyo ni katika watu wa Motoni na yeye yuko njiani kuelekea huko Motoni?

6 – Hasadi ni miongoni mwa sifa zenye kusemwa vibaya. Kuacha kuwa na hasadi ni miongoni mwa sifa za watukufu. Kila chenye kuwaka moto kinaweza kuzimwa. Isipokuwa moto wa hasadi si wenye kuzimwa.

7 – Hasadi ni msingi wa chuki. Chuki ndio msingi wa shari. Yule apandaye shari moyoni mwake basi utaota mmea mchungu. Ukuaji wake ni chuki na matunda yake ni majuto.

8 – Hasadi ni kule kutamani neema iondoke kutoka kwa mwengine na imwendee yeye. Ama yule mwenye kuona neema kwa nduguye na yeye akatamani ajaaliwe mfano wake pasi na kutaka imwondoke nduguye, hiyo sio hasadi iliyosemwa vibaya na kukatazwa.

9 – Hasadi inakaribia kutokuweko isipokuwa kwa yule ambaye ameitukuza neema ya Allaah juu yake. Kila ambavo Allaah anampa neema ndivo mashahidi wanavyomchukia zaidi.

10 – Muhammad bin Siyriyn amesema:

“Sijapatapo kumuhusudu mtu juu ya kitu cha kidini wala cha kidunia.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 132-135
  • Imechapishwa: 05/08/2021