36. Mambo mawili yaliyopendekezwa kwa ambaye amehudhuria mwaliko


34- Yaliyopendekezwa kwa ambaye amehudhuria mwaliko

 Kuna mambo mawili yaliyopendekezwa kwa ambaye amehudhuria mwaliko

Jambo la kwanza: Du´aa kumuombea yule mwenyeji

1- Amuombee yule mwenyeji baada ya kumaliza kutokana na yaliyokuja kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ni aina mbalimbali:

Ya kwanza: ´Abdullaah bin Bisr ameeleza kwamba baba yake alimtengenezea chakula Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akawa amemwalika na akaitikia. Wakati alipomaliza kula akasema:

اللهم اغفر لهم وارحمهم وبارك لهم فيما رزقتهم

“Ee Allaah! Wasamehe, wahurumie na uwabariki katika kile ulichowaruzuku!”[1]

Ya pili: Miqdaad bin al-Aswad amesimulia kwa kusema: “Nilikwenda mimi na wenzangu wawili kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tukapatwa na njaa kwelikweli ambapo tukawoamba msaada watu lakini hakuna yeyote aliyetukaribisha. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatuchukua na kutupeleka nyumbani kwake ambapo kulikuwa na mbuzi wanne. Akanambia: “Ee Miqdaad! Gawa maziwa kati yetu mara nne.” Nikawa nayagawa kati yetu mara nne ambapo kila mmoja akanywa sehemu yake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukampa sehemu yake. Usiku mmoja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakawia huko nje ambapo nikaanza kujiambia mwenyewe kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekwenda kwa baadhi ya Answaar na amekula mpaka ameshiba na amekunywa mpaka amekata kiu chake – ni kwa nini basi nisinywe sehemu yake? Sikuacha kuendelea kufikiria hivo mpaka nikainuka na kunywa sehemu yake. Halafu nikafunika kikombe chake. Nilipomaliza nikaanza kuwa na wasiwasi nilivyofanya na nikawaza kwamba hivi sasa atakuja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hatokuta kitu. Nikataka kulala; nilikuwa na blanketi la sufi ambapo kila ninavyoivuta kichwani mwangu miguu yangu inabai wazi na nikiivuta miguuni mwangu kichwa changu kinabaki wazi. Sikuweza kupata usingizi na nikawa nikiwaza mambo. Ama wenzangu wawili walikuwa wameshalala. Nilipokuwa katika hali hiyo tahamaki akaingia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akatoa salamu inayosikika na yule aliye macho na wala haiwezi kumuamsha aliyelala. Kisha akaenda msikitini na kuswali. Halafu akakiendea kikombe chake na akakifungua lakini hakuona kitu ambapo akasema: “Ee Allaah! Mlishe yule mwenye kunilisha na mnyweshe yule mwenye kuninywesha.” Nikataka kupata fursa ya du´aa hii ambapo nikachukua blanketi langu na kulivaa kiunoni, nikachukua kisu kikubwa na kuwaendea wale mbuzi na kuanza kuwakagua kutazama ni yupi katika wao aliyenona zaidi ili nipate kumchinjia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini mikono yangu haikupita kwenye chuchu za mbuzi yeyote isipokuwa nilimuona kuwa amejaa maziwa. Nikachukua chombo cha wakeze Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambacho hawakuweza kufikiria kuwa kitajaa maziwa na nikaanza kukamua maziwa mpaka yakajaa. Halafu nikamwendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akasema: “Je, wewe hukunywa kinywaji chako usiku huu, ee Miqdaad?” Nikasema: “Nilikunywa, ee Mtume wa Allaah!” Akainua kichwa chake kunitazama na kusema: “Umefanya mambo mabaya, ee Miqdaad. Lete khabari!” Nikasema: “Kunywa kwanza ndio ndio kutakuja khabari.” Akanywa mpaka akakata kiu chake kisha akanipa kikombe nami nikanywa.

Nilipojua kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameshakata kiu chake na kwamba du´aa yake imenigusa mimi, nikaanza kucheka mpaka nikaanguka chini kwa sababu ya kicheko. Akasema: “Kuna nini?” Nikamweleza mambo yalivo. Akasema: “Hii ni baraka iliyotoka mbinguni. Ni kwa nini hukunieleza ili tuweze kuwanywesheleza wenzetu?” Nikasema: “Ninaapa kwa Yule ambaye amekutuma kwa haki, midhali baraka zimekupata wewe na mimi sikufikiria wale waliokosa.”[2]

Ya tatu: Anas au mwengineo amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwatembelea Answaar. Kila alipokuwa akifika nyumbani mwa Answaar basi watoto wa Answaar wanakuja kumzunguka anawaombea du´aa, anawapapasa vichwa vyao na kuwatolea salamu. Siku moja alienda mlangoni mwa Sa´d bin ´Ubaadah na akaomba idhini ya kuingia na kusema: “as-Salaam ´alaykum wa Rahmatullaah” ambapo Sa´d akasema: “wa ´alaykumus-Salaam wa Rahmatullaah” lakini hata hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa hakusikia. Akafanya hivo mara tatu ambapo Sa´d akamuitikia mara tatu lakini hata hivyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusikia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi juu ya salamu tatu ambapo akiruhusiwa, anaingia, vinginevyo anarudi nyuma. Basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amerudi zake ambapo Sa´d akamfuata na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Baba yangu na mama yangu wawe fidia yako. Hakuna salamu yoyote uliyotoa isipokuwa nilikupa idhini na kukuitikia lakini sikutaka usikie kwa sababu nilipenda nikithirishe salamu na baraka kutoka kwako. Kwa hiyo karibu, ee Mtume wa Allaah!” Halafu wakaingia nyumbani kwake na akamkaribisha zabibu amnapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akala na wakati alipomaliza alisema:

أكل طعامكم الأبرار وصلت عليكم الملائكة وأفطر عندكم الصائمون

“Wale chakula chenu watu wema, wawaombee du´aa Malaika na wafuturu kwenu waliofunga.”[3]

 Jambo la pili: Kumuombea du´aa bwana harusi na bibi harusi

2- Jambo la pili amuombee du´aa ya kheri na ya baraka yeye bwana harusi na bibi harusi. Kuna Hadiyth juu ya hlo:

Ya kwanza: Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia akisema: “Baba yangu alikufa na akaacha wasichana saba au tisa. Nikamuoa mwanamke ambaye ni mtumzima [mjane]. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanambia: “Umeoa, ee Jaabir?” Nikajibu: “Ndio.” Akasema: “Bikira au mtumzima?” Nikajibu: “Nimeoa mtumzima.” Akasema: “Kwa nini hukuoa msichana ambaye angelicheza na wewe na wewe ukacheza naye na akakuchekesha na wewe ukamchekesha?” Nikamwambia: “´Abdullaah amefariki na ameacha wasichana tisa au saba na mimi sikupenda kuwaletea ambaye  yuko sawa na wao na ndipo nikaoa mwanamke ambaye anaweza kuwasimamia na kuwarekebisha.” Akasema:

بارك الله لك

“Allaah akubariki.”

au aliniombea kheri[4].

Ya pili: Buraydah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Kuna kundi katika Answaar walimwambia ´Aliy: “Wewe uko na Faatwimah” ambapo akamwendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamtolea salamu. Mtume akamwambia: “Unahitajia nini, ee mwana wa Abu Twaalib?” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ametajwa Faatwimah msichana wa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akamwambia: “Karibu na uko miongoni mwa familia” na hakuzidisha juu yake neno. ´Aliy bin Abiy Twaalib akatoka akirudi katika kundi lile la Answaar wakimsubiri na wakamuuliza: “Mambo yamekuwa vipi?” Akajibu: “Sijui, lakini hata hivyo amenambia: “Karibu na uko miongoni mwa familia” Wakasema: “Moja wapo [ya hayo maneno] kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanakutosheleza; amekupa mke na amekukaribisha. Baada ya ´Aliy kumuoa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ee ´Aliy! Ni lazima kwa bwana harusi kufanya karamu ya ndoa.” Sa´d akasema: “Mimi nina kondoo” na kundi katika Answaar wakawa wamekusanya mahindi. Ilipofika usiku wa ndoa, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia: “Usifanye lolote mpaka kwanza ukutane na mimi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaomba maji, akayatawadha kisha akammwagia nayo ´Aliy na kusema: “

اللهم بارك فيهما وبارك لهما في بنائهما

“Ee Allaah! Wabariki wawili hawa na wabariki katika kule kuingiliana kwao.”[5]

Ya tatu: ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza akisema: “Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinioa ambapo mama yangu akaja na kuniingiza katika nyumba. Ndani walikuweko wanawake wa Answaar ambao wakasema:

على الخير والبركة وعلى خير طائر

“[Ndoa iwe] yenye kheri na baraka na iwe fungu lenye kheri.”[6]

Ya nne: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anah) amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimuombea yule mwenye kuoa na kusema:

بارك الله لك وبارك الله عليك وجمع بينكما في وفي رواية: على خير

“Allaah akubariki na abariki juu yako na awajumuishe kati yetu.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

على خير

“Allaah akubariki na abariki juu yako na awajumuishe katika kheri.”[7]

[1] Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (01/158/12-02), Muslim (06/122), Abu Daawuud (02/135), an-Nasaa´iy katika “al-Waliymah” (03/66), at-Tirmidhiy (04/281) ambaye ameisahihisha, al-Bayhaqiy (07/274), Ahmad (04/178-188) na (190) na matamshi ni yake, Ibn as-Sunniy kwa nambari (470), at-Twabaraaniy (01/116/01), Ibn ´Asaakir amepokea kutoka kwake (08/171), (09/02), (01/03) – 02.

[2] Ameipoikea Muslim (06-128-129), Ahmad (02/06), (03) na (04-05), na siyaaq ni yake, Ibn Sa´d (01/183-184). Baadhi yake imepokelewa na at-Tirmidhiy (03/394) na ameisahihisha, al-Harbiy katika “al-Ghariyb” (01/189/05).

[3] Ameipokea Ahmad (03/138), Abu ´Aliy as-Swaffaar katika Hadiyth yake, at-Twahaawiy katika “al-Mushkil” (01/498-499) na ziada ni yake, al-Bayhaqiy (07/287), Ibn ´Asaakir (07/59-60) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh na wengineo.

[4] Ameipokea al-Bukhaariy (09/423) na siyaaq ni yake, Muslim (04/176) na nyongeza ni yake. Katika mlango huu Anas pia amepokea na imekwishatangulia katika masuala ya 16.

[5] Ameipokea Ibn Sa´d (08/20-21), at-Twabaraaniy katika “al-Kubraa” (01/112/01) kwa mlolongo wa wapokezi mzuri, Ibn ´Asaakir (02/88/12). Tayari tumeshatangulia kuizungumzia katika masuala ambayo punde tu yameashiriwa.

[6] Ameipokea al-Bukhaariy (09/182), Muslim (04/141) na al-Bayhaqiy (07/149).

[7] Ameipokea Ibn Sa´iyd al-Mansuur katika “Suniy” yake (522), Abu Daawuud (01/332), at-Tirmidhiy (02/171), Abu ´Aliy at-Twuusiy (01/110) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 167-175
  • Imechapishwa: 27/03/2018