Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha ´Utbah bin Rabiy´ah, Shaybah bin Rabiy´ah, al-Waliyd bin ´Utbah na Umayyah bin Khalaf wakatupwa kwenye shimo. Usiku akasimama karibu na viwiliwili vyao na akawakaripia. Akasema:

“Ni ndugu wabaya wa Mtume mlioje mlikuwa kwa Mtume wenu. Mlinikadhibisha na wengine wakanisadikisha. Mlininyima nusura ambapo wengine wakanipa nusura. Mlinitoa ambapo wengine wakanikaribisha.”

Akabaki ´Arsah kwa muda wa siku tatu. Halafu akaondoka na mateka na ngawira ambao alikadhibiwa na ´Abdullaah bin Ka´b bin ´Amr an-Najjaariy.

Wakati wa vita vya Badr Allaah akateremsha Suurah “al-Anfaal”. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika Swafraa´ akagawa ngawira kama alivyomwamrisha Allaah (Ta´ala). Akaamrisha an-Nadhr bin al-Haarith akatwe shingo yake baada ya kushikwa mateka. Hilo ni kwa sababu ya uenezaji ufisadi wake mkubwa na kumuudhi kwake sana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akarithiwa na dada yake (kuna maoni mengine yanayosema kwamba msichana wake ndiye aliyemrithi) kwa shairi maarufu iliyotajwa na Ibn Hishaam. Wanadai kwamba wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoyasikia alisema:

“Lau ningeyasikia kabla ya kumuua basi nisingemuua.”[1]

Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofika ´Irq-udh-Dhubyah aliamrisha ´Uqbah bin Abiy Mu´ayt akatwe shingo yake. Yeye pia alikatwa shingo yake baada ya kukamatwa mateka.”

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawataka ushauri Maswahabah wake awafanye nini wale mateka. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) akashauri wauawe. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akashauri waachwe kwa fidia. Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachagua ushauri wa Abu Bakr na akayafanya hayo. Ndipo Allaah (Ta´ala) akateremsha makemeo fulani pale Aliposema:

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

”Haikumpasa Nabii awe ana mateka [na kuwaacha kwa fidia] mpaka apigane na kushinda katika nchini. Mnataka mambo ya dunia na hali Allaah anataka Aakhirah. Allaah ni Mwenye nguvu za kushinda kabisa, Mwenye hekima.”[2]

Muslim amepokea Hadiyth ndefu kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambapo ndani yake amebainisha tukio zima. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafanya ukombozi wao ni elfu nne kwa kila mmoja.

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akarudi al-Madiynah hali ya kuwa ni mshindi na mnusuriwaji. Allaah amelinyanyua neno Lake na akamfanya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa imara na kuitukuza nusura yake. Watu wengi wa al-Madiynah wakaingia katika Uislamu. Hapo ndipo ´Abdullaah bin Abiy Saluul na kundi la wanafiki wakasilimu kwa unafiki.

[1] al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (3/384).

[2] 08:67

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 09/10/2018