35. Mwenye busara na upelelezi


1 – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Nakutahadharisheni na dhana kwani hakika dhana ni mazungumzo ya uongo kabisa. Msipelelezi, msiulizieulizie na wala msichukiane. Kuweni waja wa Allaah ndugu.”

2 – al-Hasan al-Baswriyr amesema:

”Usiulizie juu ya kitendo cha ndugu yako kizuri na kiovu. Kufanya hivo ni katika kupeleleza.”

3 – Ni lazima kwa aliye na busara kulazimiana na usalama kwa kuacha kupeleleza juu ya makosa ya watu na badala yake ajishughulishe na kasoro na  nafsi yake mwenyewe. Kwani yule mwenye kujishughulisha na mapungufu yake mwenyewe badala ya mapungufu ya wengine basi ataupumzisha mwili wake na wala hatouchosha moyo wake. Kila pale atakapoona makosa ya nafsi yake basi atayachukulia wepesi makosa mfano wake ya nduguye. Ambaye anajishughulisha na makosa ya wengine badala ya makosa yake mwenyewe, basi moyo wake hushikwa na upofu na mwili wake huchoka na hivyo haitomuwezekania kuacha makosa ya nafsi yake.

4 – ash-Shaybaaniy amesema:

”Imeandikwa katika vitabu vya kale ”Kama unavofanya ndivo nawe utavofanyiwa”.”

5 – Upelelezi ni sampuli fulani ya unafiki na dhana njema ni sampuli fulani ya imani. Mwenye busara anawajengea dhana njema ndugu zake na anajiwekea mwenyewe masononeko na huzuni zake. Mjinga anawajengea dhana mbaya ndugu zake na wala hafikirii kabisa dhambi na huzuni zake.

6 – Dhana mbaya imegawanyika mafungu mawili:

1 – Iliyokatazwa kwa hukumu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2 – Iliyopendekezwa.

Dhana iliyokatazwa ni kuwajengea dhana mbaya waislamu wote.

Dhana iliyopendekezwa ni kama kwa mfano mtu kuwa na dhana mbaya juu ya mtu ambaye kuko kati yao uhasama katika mambo ya dini au ya dunia na hivyo akawa anamukhofu. Katika hali hiyo inamlazimu kutilia dhana mbaya njama na vitimbi vyake ili awe katika hali ya tahadhari.

7 – ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw amesema:

“Imeandikwa katika Tawraat: “Anayekuwa mfanyabiashara basi anakuwa mtenda dhambi. Anayemchimbia shimo rafiki yake basi hutumbukia ndani mwenyewe.”

8 – Ni lazima kwa mwenye busara kutokuwa na tabia na matendo kama ya mjinga. Asipeleleze aibu za watu. Ambaye atafunua aibu za wengine basi husababisha aibu zake naye kufunuliwa. Pengine aibu zake zikafunuliwa kwa sababu tu ameenda kutafuta aibu za wengine. Ni vipi muislamu ataona kuwa ni vyema kumkosoa muislamu mwenzie kwa kitu ambacho yeye mwenyewe yuko nacho?

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 125-128
  • Imechapishwa: 03/08/2021