Bora kwa msafiri ni yeye kufanya kile ambacho ni chepesi zaidi kwake katika kufunga au kula. Mawili hayo yakilingana basi kufunga ndio bora zaidi. Kwa sababu ni kuharakisha zaidi kuitakasa dhimma yake na anapata uchangamfu zaidi pale anapofunga pamoja na watu wengine. Jengine ni kwa sababu ndio kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ambavo Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

“Tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan katika hali ya joto kali kiasi cha kwamba mmoja wetu alikuwa akiweka mikono yake juu ya kichwa chake kutokana na ukali wa joto. Hapakuweko yeyote katika sisi mwenye kufunga isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaah.”

Wakati mwingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mwenye kufungua kwa sababu ya kuchunga hali za Maswahabah zake wakati alipofikiwa na khabari kwamba swawm inawatia uzito. Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka kuelekea Makkah mwaka ulipofunguliwa mji wa Makkah ambapo akafunga mpaka walipofika Kuraa´ al-Ghamiym ambapo watu wakafunga pamoja naye. Akaambiwa kuwa watu swawm imekuwa ngumu kwao na kwamba wanatazama kile unachokifanya. Akaomba chombo cha maji baada ya alasiri akanywa na huku watu wanamtazama.”

Ameipokea Muslim.

Katika Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliuendea mto ambao unanyeshelezewa na maji kutoka mbinguni wakati ambapo watu walikuwa wamefunga katika siku za majira ya joto. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa juu ya nyumbu wake ambapo akasema: “Enyi watu, kunyweni maji!” Wakakataa. Akasema: “Mimi si kama mfano wenu.” Mimi ni mwepesi zaidi kwenu na mimi nimepanda.” Wakakataa. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashuka na kunywa ambapo watu nao wakanywa. Lakini hakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anataka kunywa.”

Ameipokea Ahmad[1].

Ikiwa msafiri kufunga kunamtia uzito basi ale na wala asifunge safarini. Katika Hadiyth ya Jaabir iliotangulia ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipofungua pindi swawm ilipokuwa ngumu kwa watu. Aliambiwa kuwa baadhi ya watu wamefunga ambapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hao ni waasi. Hao ni waasi.”

Ameipokea Muslim.

al-Bukhaariy na Muslim wamepotea kupitia kwa Jaabir ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa safarini ambapo akaona msongamano wa watu na mtu ambaye amefanyiwa kivuli. Akauliza: “Ana nini huyu?” Akaambiwa: “Amefunga.” Ndipo akasema:

“Si katika wema kufunga safarini.”

Msafiri akipata safari katikati ya mchana na ikawa ni ngumu kwake kukamilisha swawm yake basi inafaa kwake kula akishatoka nje ya mji wake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga na watu wakafunga pamoja naye mpaka walipofika maeneo ya Kuraa´ al-Ghamiym. Wakati alipoambiwa kuwa swawm imekuwa ngumu kwa watu akafungua na watu wakafungua pamoja naye.

[1] Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Yamesemwa na mtunzi wa “Fath-ur-Rabbaaniy”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 03/05/2020