34. Mwenye hedhi kubaki msikitini akifuatilia darsa

Swali 34: Ni ipi hukumu ya mwanamke mwenye hedhi kubaki katika msikiti Mtakatifu kwa ajili ya kusikiliza Hadiyth na Khutbah ilihali ni mwenye hedhi?

Jibu: Haijuzu kwa mwanamke aliye na hedhi kubaki katika msikiti Mtakatifu wala misikiti mingine. Lakini inafaa kwake kupita msikitini na kuchukua haja yake kutoka humo na mfano wa hayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia ´Aaishah wakati pindi alipomwamrisha kumletea mkeka ambapo akamjibu kwamba mkeka uko msikitini na yeye yuko na hedhi. Akasema:

“Hedhi yako haiko mikononi mwako.”

Hakuna neno mwenye hedhi akipita msikitini wakati huohuo anaamini kuwa damu haitotiririka msikitini. Haijuzu ikiwa anataka kuingia na kuketi chini. Dalili ya hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaamrisha wanawake watoke kwenda katika uwanja wa kuswalia ´iyd; wanawali, wasichana mabikira na wenye hedhi. Licha ya kuwa ameamrisha mwenye hedhi kujiepusha na uwanja wa kuswalia. Hivyo hiyo ikawa ni dalili inayojulisha kuwa haijuzu kwa mwenye hedhi kukaa msikitini kwa ajili ya kusikiliza Khutbah, darsa na Hadiyth.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 31/07/2021