34. Msimamo wa Ahl-ul-Bid´ah juu ya uombezi siku ya Qiyaamah


Uombezi huu unapingwa na Khawaarij, Mu´tazilah, Raafidhwah na wapotevu wengine. Hata hivyo umethibiti katika Qur-aan na Sunnah:

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi isipokuwa kwa yule Aliyemridhia.”[1]

Wao wameshikamana na ule ueneaji wa Aayah zinazowahusu makafiri na sio waumini. Mfano wa Aayah hizo ni:

 أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ

“Toeni katika Tulivyokuruzukuni kabla haijafika Siku ambayo hakutokuweko [wala kukubaliwa] mapatano wala urafiki wala uombezi.”[2]

Kuna Aayah nyingi zinazokanusha uombezi kwa makafiri:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.”[3]

Watu wenye kufuata matamanio wameshikamana na ueneaji wa Aayah hizi na wameacha mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), na kadhalika baadhi ya Aayah za Qur-aan, zinazofahamisha kuwa uombezi utakuwpeo kwa waumini ambao Allaah amewaridhia:

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi isipokuwa kwa yule Aliyemridhia.”

وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ

“Wala hautofaa uombezi mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini.”[4]

Allaah kamwe hatoacha makafiri waombewe na wala hatokubali kabisa yeyote awaombee. Wala hatokubali uombezi wa Ibraahiym kwa baba yake. Pamoja na kuwa Ibraahiym ndiye baba wa Mitume ambaye yuko na hadhi tukufu mbele ya Allaah na alikuwa ni mpenzi Wake wa hali ya juu uombezi wake kwa baba yake hautokubaliwa.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake ndiye ana uombezi maalum kwa Abu Twaalib. Atamuombea ili aondoshwe kwenye rindi la Moto na kuwekwa katika Moto mwepesi. Hata hivyo uombezi wa waombezi hautokubaliwa juu yao:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi hautowafaa uombezi wowote wa waombezi.”

Aayah hii inawahusu makafiri. Kuhusu waumini, Aayah hizi ndizo zinawahusu:

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ

“Ni Malaika wangapi mbinguni hautowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa Amtakaye na Akaridhia.”[5]

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[6]

Uombezi ulioidhiniwa kwa waumini umethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo kama tulivyosema watawaombea waumini ili zinyanyuliwe ngazi zao, wasiingizwe Motoni na ili watoke.

Hii ndio ´Aqiydah wanayoamini Ahl-us-Sunnah na ni msingi mmoja wapo katika misingi yao wanayojipambanua nayo kutokamana na watu wanaofuata matamanio katika Khawaarij, Raafidhwah na wengineo wanaofuata batili. Ni wajibu kwa muumini kuamini na kusadikisha hilo.

[1] 21:28

[2] 02:254

[3] 74:48

[4] 34:23

[5] 53:26

[6] 02:255

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 401-402
  • Imechapishwa: 19/09/2017