7- Mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya imani:

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaona kuwa uhakika wa imani ni kuamini kwa moyo, kutamka kwa ulimi na matendo ya viungo. Dalili ya ´Aqiydah yao hii ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Imani ni tanzu sabini na kitu. Ya juu yake ni “Laa ilaaha illa Allaah” na ya chini yake ni kuokota chenye kudhuru kutoka njiani. Hayaa ni tanzu ya imani.”[1]

Kutamka kwa ulimi ni kusema “Laa ilaaha illa Allaah”.

Matendo ya viungo ni kuokota chenye kuudhi kutoka njiani na hayaa ni matendo ya moyo.

Kuhusu kuamini ndani ya moyo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imani ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake, siku ya Mwisho na Qadar kheri na shari yake.”[2]

Vilevile wanaona kuwa imani inapanda na inashuka. Qur-aan imefahamisha juu ya kuzidi kwake. Ulazima wa kiakili unapelekea kwamba kila ambacho imethibiti kuwa kinapanda basi kinashuka pia. Kwani kupanda hakuwezi kupatikana bila ya kupungua:

وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا

“Iwazidishie imani wale walioamini.”[3]

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا

“Inapoteremshwa Suurah, basi miongoni mwao wako wanaosema: “Nani kati yenu imemzidishia [Suurah] hii imani?”[4]

Hapana shaka juu ya hilo.

Tuliposema kuwa imani ni maneno na matendo hapana shaka kwamba maneno yanatofautiana. Mwenye kusema “Subhaan Allaah”, “Alhamdulillaah” na “Allaahu Akbar” mara moja halingani na aliyesema hivo mara nyingi. Kadhalika tunasema kuwa imani ambayo ni kule kuamini kimoyo kunatofautiana nguvu na udhaifu wake. Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي

“Mola wangu nionyeshe vipi Unahuisha wafu? Akasema: “Je, kwani huamini?” Akajibu: “Balaa!  Lakini ili moyo wangu utumainike.”[5]

Kuambiwa hakulingani na mtu kujionea mwenyewe.

Kuna mtu ameelezwa khabari na mtu mmoja. Katika hali hii amejua kitu juu ya khabari hizo. Anapokuja mtu wa pili akamweleza nazo anazidi kuwa na nguvu. Anapokuja mtu wa tatu akamweleza nazo anazidi kuwa na nguvu zaidi na kadhalika.

Kujengea juu ya hayo tunasema kuwa imani inazidi na inapungua kukiwemo imani ya kuamini kimoyo, jambo ambalo analitambua kila mtu ndani ya nafsi yake.

Kuhusu ambao wamepinga juu ya kupanda na kushuka kwake hakika wamekwenda kinyume na Shari´ah na uhakika wa mambo. Hivyo inapanda na inashuka.

Mpaka hapa ndio mwisho. Allaah ndiye muwafikishaji.

Ee Allaah! Msifu na mswalie Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (09) na Muslim (35).

[2] Muslim (08).

[3] 74:31

[4] 09:124

[5] 02:260

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 47-49
  • Imechapishwa: 18/09/2019