32. Nguzo ya kwanza ya swalah: Kusimama kwa anayeweza

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo ya kwanza ni kusimama kwa mwenye kuweza. Dalili ni Kauli Yake (Ta ´ala):

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

”Zichungeni swalah na khaswa khaswa swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah hali ya kuwa ni wanyenyekevu.”[1]

MAELEZO

Nguzo ya kwanza ya swalah katika nguzo za swalah ya faradhi ni kusimama kwa mwenye kuweza. Endapo mtu ataswali swalah ya faradhi kwa kukaa chini ilihali anaweza kusimama, swalah yake inabatilika na haisihi. Kwa sababu ameacha nguzo miongoni mwa nguzo za swalah ambayo ni kusimama wakati ana uwezo wa kufanya hivo. Lakini ikiwa mtu hawezi basi kunadondoka kusimama na ataswali kwa kuketi chini.

Maneno yake:

Dalili ni Kauli Yake (Ta ´ala):

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

”Zichungeni swalah na khaswa khaswa swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah hali ya kuwa ni wanyenyekevu.”

Imaam al-Qurtwubiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kusimama kwa unyenyekevu – ambayo ni moja katika vigawanyo vyake – na ummah umeafikiana juu ya kwamba kusimama ndani ya swalah ya faradhi ni jambo la lazima kwa kila ambaye ni mzima na muweza ni mamoja anaswali kipekee au ni imamu. Amesmea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imamu amewekwa ili afuatwe. Hivyo basi, akiswali kwa kusimama nanyi swalini kwa kusimama… “

Hadiyth imepokelewa na maimamu[2]. Pia ndio ubainifu wa maneno Yake (Ta´ala):

وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

“… na simameni mbele ya Allaah hali ya kuwa ni wanyenyekevu.”[3]

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia: “Nilikuwa naumwa ugonjwa wa bawasili nikamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akanambia:

“Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, kwa kulalia ubavu.”[4]

Ni ruhusa kuswali swalah iliyopendekezwa kwa kuketi chini. Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hatujui tofauti yoyote juu ya kuswali swalah iliyopendekezwa kwa kuketi chini.”[5]

Lakini hapati thawabu isipokuwa nusu za ambaye amesimama akiwa amefanya hivo pasi na udhuru. al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Imraan bin Huswayn (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Nilimuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) swalah ya mtu hali ya kukaa. Akasema: “Kuswali kwa kusimama ndio bora. Anayeswali kwa kukaa anapata nusu ya thawabu za ambaye ameswali kwa kusimama. Anayeswali kwa kulala anapata nusu ya thawabu za ambaye ameswali kwa kukaa.”[6]

Ambaye ni muweza akiswali swalah iliyopendekezwa kwa kuketi chini, basi hapati isipokuwa nusu ya thawabu. Yule ambaye ni mgonjwa ambapo akaswali kwa kukaa basi anapata thawabu kamilifu. Kwa sababu hicho ndicho anachokiweza.

[1] 02:238

[2] al-Bukhaariy (378) na Muslim (411).

[3] Tafsiyr-ul-Qurtwubiy (03/217-218).

[4] al-Bukhaariy (1117).

[5] al-Mughniy (01/442).

[6] al-Bukhaariy (1115).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 53-55
  • Imechapishwa: 04/01/2022