33. Maana ya mungu


Mungu maana yake ni mwabudiwa. Mwabudiwa anaweza kuabudiwa kwa haki au kwa batili. Chenye kuabudiwa huitwa mungu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) peke yake ndiye anayeabudiwa kwa haki. Waungu wengine wote, kama masanamu, miti, mawe na makaburi, wanaabudiwa kwa batili. Ndio maana shahaadah ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` maana yake ni kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Haitoshi kusema kuwa hapana mwabudiwa isipokuwa Allaah. Kitu hicho ni batili. Kwa sababu hiyo italeta maana kwamba waungu wote wanaoabudiwa ni Allaah. Hayo ndio madhehebu ya watu wenye kuamini Wahdat-ul-Wujuud wanaosema kuwa kila chenye kuabudiwa na kila sanamu ni Allaah. Kwa hivyo ni lazima neno hilo lifungamanishwe kwamba ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)´. Kwa kifungamanishi hichi wanatoka waungu wote wa batili. Amesema (Ta´ala):

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah ndiye wa haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili na kwamba Allaah ndiye Aliye juu kabisa, Mkubwa.”[1]

Allaah pekee ndiye Mungu wa haki. Hakuna mungu mwingine wa haki isipokuwa Yeye tu. Waungu wengine wote ni wa batili. Kwa hivo unaposema kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah basi umethibitisha kuwa Allaah pekee ndiye ambaye anastahiki kuabudiwa na umekanusha ´ibaadah wanazofanyiwa wengine wote. Neno hilo limekusanya kati ya ukanushaji na uthibitishaji. Linakanusha ´ibaadah wanazofanyiwa asiyekuwa Allaah na linathibitisha ´ibaadah kustahiki kufanyiwa Allaah pekee pasi na kuwa na mshirika.

[1] 22:62

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 15/07/2021