33. Kufungua kwa ajili ya mwenyeji wako


31- Kufungua kwa ajili ya yule aliyemwalika

Inafaa kwake kufungua ikiwa ni swawm ya sunnah na khaswa khaswa akimnga´nga´nia yule mwenyeji wake. Kumekuja Hadiyth zifuatazo juu ya hilo:

1- “Mmoja wenu atakapoitwa kwenye chakula basi aitikie; akitaka afungue na akitaka aache [kufungua].”[1]

2- “Anayefunga swawm ya sunnah ni kiongozi juu ya nafsi yake; akitaka atafunga na akitaka atafungua.”[2]

3- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Kuna siku Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia na kusema: “Je, mna kitu?” Nikasema: “Hapana.” Akasema: “Basi mimi nimefunga.” Kisha siku nyingine akanipitia na nilikuwa nimeletewa al-Hays. Basi nikamwekea nayo, kwani alikuwa akipenda al-Hays. Nikasema: Ee Mtume wa Allaah! Tumeletewa al-Hays na nimekugawia baadhi yake.” Akasema: “Niletee nayo, lakini nimekuwa nimeamka na swawm.” Akala kisha akasema:

“Mfano wa swawm ya sunnah ni kama mtu ambaye ametoa swadaqah katika mali yake; akitaka ataitoa na akitaka ataizuia.”[3]

[1] Ameipoikea Muslim na Ahmad (03/392), ´Abd bin Humayd katika “al-Muntakhab” (01/116), at-Twahaawiy katika “al-Mushkil” (04/148). an-Nawawiy amesema:

“Hapa ni pale ambapo ikiwa swawm yake ni ya sunnah na yule mwenyeji wake akaona uzito. Bora katika hali hii afungue.”

Kuna maneno mfano wake katika “al-Fataawaa” (04/143) ya Ibn Taymiyyah.

[2] Ameipokea an-Nasaa´iy katika “al-Bubraa” (02/64), al-Haakim (01/439), al-Bayhaqiy (04/276) kupitia Hadiyth ya Sammaak bin Harb, kutoka kwa Swaalih bin Umm Haaniy aliyepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Haakim amesema:

“Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.”

ad-Dhahabiy ameafikiana naye.

[3] Ameipokea an-Nasaa´iy kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kama ilivyobainishwa katika “al-Irwaaa´” (04/135/636).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 155-158
  • Imechapishwa: 24/03/2018