33. Allaah alijua yatayotendeka kabla ya kupatikana kwa viumbe

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

29- Hakuna kilichofichikana Kwake kabla Yeye kuwaumba.

30- Aliyajua yale watakayoyatenda kabla ya kuwaumba.

31- Amewaamrisha kumtii Yeye na akawakataza kumuasi.

MAELEZO

Alijua ni mambo yepi yatayotokea kabla ya viumbe kupatikana. Si kwamba hayajui isipokuwa baada ya kutokea Kwake. Alijua ni mambo gani watayoyafanya viumbe kabla ya kuwaumba, alimjua ni nani ambaye atakuwa mtiifu na ni nani ambaye atakuwa ni mtenda madhambi. Amewaamrisha kumtii Yeye na akawakataza kumuasi:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu”[1]

Alianza kuwaumba, kisha akawaamrisha kumwabudu. Hakika Yeye (Subhaanah) amewaamrisha kumtii na kumwabudu. Pamoja na kwamba alitangulia kujua ni kipi kila mmoja atakachofanya. Lakini hata hivyo malipo hayatokani na ule ujuzi; bali malipo yanatokana na matendo. Allaah hamuadhibu mja kutokana na ule ujuzi Wake isipokuwa ni baada ya kutenda ile dhambi. Haadhibu kutokana na ujuzi na makadirio. Kuna tofauti kati ya ujuzi na malipo. Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah akawaamrisha na kuwakataza. Yule ambaye atatii maamrisho na akajiepusha na makatazo atapata malipo. Yule mwenye kwenda kinyume na maamrisho na akayafanya yale aliyokatazwa ataadhibiwa. Mja analipwa kutokana na matendo yake mwenyewe, na si kutokana na matendo ya Allaah (Subhaanah). Mja ndiye mwenye kuswali, mwenye kutoa zakaah, mwenye kuhiji na mwenye kupambana. Matendo yananasibishwa kwa mja na si kwa Allaah isipokuwa kwa njia ya kwamba kayaumba, kayajua, kayakadiria na kuyapanga.

[1] 51:56

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 25/09/2019