32. Moja katika madhehebu mabaya mno

Ama kuhusu wale wenye kuonelea kuwa wengine ndio wajinga (Ahl-ut-Tajhiyl) ni wafuasi wengi wa Sunnah na wafuasi wa Salaf.

Mfumo wao ni kwamba wanaonelea kuwa zile Aayah zenye kuzungumzia juu ya sifa hazijulikani na hakuna yeyote anayejua maana yake. Hili linamuhusu hata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile ambaye anatamka Hadiyth zinazozungumzia sifa pasi na kujua maana yake. Pamoja na hivyo wanasema kuwa akili haina nafasi yoyote katika suala hili. Maoni yao yanapelekea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zake na maimamu wa Salaf hawakuwa na elimu juu ya suala hili. Haya ni katika maoni batilifu kabisa.

Mfumo wao juu ya Aayah zinazozungumzia sifa ni kuzipitisha kimatamshi na kuonelea kuwa maana zake hazijulikani. Kuna baadhi yao ambao wanajigonga na kusema:

“Zinatakiwa kupitishwa kidhahiri kama zilivyo pamoja na kuwa zina tafsiri mbali na ile ya dhahiri. Hakuna anayeijua isipokuwa Allaah pekee.”

Huku ni kujigonga kwa wazi kabisa. Ni vipi mtu atazipitisha kwa maana yake ya kidhahiri, ikiwa zina tafsiri mbali na ile ya dhahiri na hakuna aijuaye mwengine asiyekuwa Allaah? Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu mfumo wa watu hawa katika kitabu “al-´Aql wan-Naql”:

“Kwa hivyo inabainika kuwa maoni ya Ahl-ut-Tafwiydhw, ambao wanasema kuwa wanafuata Sunnah na Salaf, ni moja katika maoni mabaya kabisa ya Ahl-ul-Bid´ah wal-Ilhaad.”[1]

[1] (1/121).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 11/05/2020