32. Mlango kuhusu maneno Yake (Ta´ala) ”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!” (Aal ´Imraan 03:175)

2-

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّـهَ

”Hakika wanaoamirisha misikiti ya Allaah ni wale wanaomwamini Allaah na siku ya Mwisho na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah na hawamkhofu yeyote isipokuwa Allaah.” (at-Tawbah 09:18)

3-

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ

”Miongoni mwa watu wako wasemao “Tumemwamini Allaah”; lakini wanapofanyiwa maudhi kwa ajili ya Allaah, hufanya mitihani ya watu kama kwamba ni adhabu ya Allaah.” (an-´Ankabuut 29:10)

4- Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika katika udhaifu wa yakini ni kuwaridhisha watu kwa yanayomkasirisha Allaah, kuwasifu kutokana na riziki iliyoruzuku Allaah na kuwasema vibaya kwa kitu ambacho Allaah hakukuruzuku. Hakika riziki ya Allaah hailetwi kwa mbio za mwenye kuipupia na wala haizuiwi kwa chuki za mwenye kuchukia.”[1]

5- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kutaka radhi za Allaah kwa yanayowachukiza watu, basi Allaah atamridhia na pia watu watamridhia. Na yule mwenye kutaka radhi za watu kwa yanayomchukiza Allaah, basi Allaah atamkasirikia na watu pia watamkasirikia.”[2]

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake.

MAELLEZO

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!” (Aal ´Imraan 03:175)

Anachokusudia mwandishi ni kwamba ni wajibu kumuogopa Allaah (Ta´ala) khofu ambayo itamfanya kumtakasia Yeye ´ibaadah, kutekeleza maamrisho aliyomfaradhishia na kusimama katika mipaka Yake. Khofu imegawanyika aina tatu:

1- Kumuogopa Allaah. Hii ndio kubwa na muhimu zaidi. Inamfanya mtu kumtakasia ´ibaadah Yeye pekee. Ni shirki kumtekelezea khofu kama hii mwingine asiyekuwa Allaah. Ni shirki kumuogoa mwingine asije kukudhuru.

2- Khofu inayomfanya mtu kuacha mambo ya wajibu au kufanya mambo ya haramu. Kuwaogopa viumbe. Khofu hii ndio ambayo kwa ajili yake kumeteremshwa maneno Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”

Khofu hii inamfanya mtu kutotoka kwenda katika Jihaad. Ni wajibu kwa mtu asimwogope kiumbe mwenzake. Khofu inayoruhusiwa tu ni ile ambayo inamfanya mtu kuyafanya yale yaliyowekwa na Shari´ah na Allaah na akayaruhusu. Isiwe ni khofu yenye kumfanya akatenda madhambi. Hata hivyo hakuna neno mtu akamwogopa kiumbe katika mambo ya kimaumbile. Hii ni khofu ya kimaumbile. Imewekwa katika Shari´ah mtu akaogopa vitu vyenye kushtua kama kwa mfano akafunga milango ili wezi wasiingie, akabeba silaha dhidi ya mashambulizi ya wanyama wakali au akajitibu dhidi ya maradhi. Mlango huu unahusiana na aina hii ya pili ya khofu. Nayo ndio shaytwaan aliyowafanya waislamu kuwaogopa makafiri katika Uhud na wakabweteka kutotaka kutoka kwenda katika Jihaad. Ndipo Allaah akawakataza  na akawaamrisha kuwa imara ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawafuata makafiri moja kwa moja baada ya vita vya Uhud, lakini hakukutokea vita kwa sababu walikimbia.

3- Khofu ya kimaumbile kama kwa mfano kuwaogopa wanyama wakali, maradhi na mfano wake.

2-

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّـهَ

”Hakika wanaoamirisha misikiti ya Allaah ni wale wanaomwamini Allaah na siku ya Mwisho na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah na hawamkhofu yeyote isipokuwa Allaah.”

Hii ndio khofu aliyowajibisha Allaah. Vilevile khofu ya kimaumbile na ya kawaida inafaa kama tulivyotangulia kusema.

3-

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ فَإِذَا أُوذِيَ فِي اللَّـهِ جَعَلَ فِتْنَةَ النَّاسِ كَعَذَابِ

”Miongoni mwa watu wako wasemao “Tumemwamini Allaah”; lakini wanapofanyiwa maudhi kwa ajili ya Allaah, hufanya mitihani ya watu kama kwamba ni adhabu ya Allaah.”

Hapa wanasemwa vibaya. Baadhi ya watu wanapoudhiwa basi hawawezi kusubiri. Kinyume chake khofu hiyo inawafanya kutendea kazi yale aliyoharamisha Allaah na kuacha kumtii na yale aliyoyaamrisha. Huku ni kusemwa vibaya kwa sababu ni wajibu kumuogopa Allaah. Pindi mtu anapoudhiwa kwa ajili ya Allaah, basi afanye zile sababu zinazoafikiana na Shari´ah na kwenda mahakamani, kumshtakia mtawala na mfano wa hayo.

4- Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika katika udhaifu wa yakini ni kuwaridhisha watu kwa yanayomkasirisha Allaah, kuwasifu kutokana na riziki iliyoruzuku Allaah na kuwasema vibaya kwa kitu ambacho Allaah hakukuruzuku. Hakika riziki ya Allaah hailetwi kwa mbio za mwenye kuipupia na wala haizuiwi kwa chuki za mwenye kuchukia.”

Ni dalili inayoonyesha udhaifu wa imani kumkasirisha Allaah katika mambo yanayowaridhisha watu na kuwashukuru watu juu ya neema uliyotunukiwa na Allaah kupitia wao. Kilicho cha wajibu ni kumshukuru Allaah. Watu wakikufanyia wema washukuru na uwalipe, lakini shukurani zote njema anastahiki Allaah pekee ambaye ndiye kawafanya wakutendee wema. Kwa hivyo ni wajibu kumshukuru Allaah kwanza halafu ndio baadaye uwashukuru viumbe kwa kiasi cha wema wao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiyewashukuru watu hamshukuru Allaah.”

Lakini hata hivyo shukurani kwa Allaah ndio zinatakiwa kuwa kubwa zaidi kwa sababu Yeye ndiye kasababisha na ndiye kawafanya watu kukutendea wema. Hadiyth inasema:

“…  na kuwasema vibaya kwa kitu ambacho Allaah hakukuruzuku.”

Kuwasema vibaya kwa sababu hawakukufanyia kitu ambacho Allaah amekuwa amekuandikia. Ni wajibu kwako kumuomba Allaah katika fadhilah Zake. Ikiwa watu wako na haki yako basi tambua kuwa Allaah hatoipoteza. Utaipata siku ya Qiyaamah. Lakini hata hivyo hii haina maana kwamba hili linazuia mtu kutoomba haki yake, kama vile haki yake ya zakaah ikiwa ni katika wenye kuistahiki kupewa, lakini usiwaseme vibaya kwa sababu hawakukupa kitu. Bali unatakiwa kumsema vibaya yule aliyesemwa vibaya na Allaah na kumsifu yule aliyesifiwa na Allaah. Waseme vibaya kwa sababu hawakutekeleza haki ya Allaah na wanafanya mambo ya haramu, lakini sio kwa sababu hawakukupa. Usiwe ni mwenye kulipiza kisasi juu ya nafsi yako. Hadiyth inasema:

“Hakika riziki ya Allaah hailetwi kwa mbio za mwenye kuipupia na wala haizuiwi kwa chuki za mwenye kuchukia.”

Kile ambacho hukuandikiwa hakipatikani kwa mbio za kukipupia. Bali unachotakiwa wewe ni kufanya sababu. Usipopata kile unachotafuta basi usivunjike moyo. Kadhalika hakuna yeyote awezaye kuzuia kile ambacho Allaah amekwishakuandikia japokuwa watu watachukia.

 5- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kutaka radhi za Allaah kwa yanayowachukiza watu, basi Allaah atamridhia na pia watu watamridhia. Na yule mwenye kutaka radhi za watu kwa yanayomchukiza Allaah, basi Allaah atamkasirikia na watu pia watamkasirikia.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake.

Ni dalili inayoonyesha kuwa ni wajibu kwa muislamu kutafuta radhi za Allaah na kufanya sababu kuzipata. Kwa sababu ukiridhiwa na Allaah basi umepata kheri zote na akikukasirikia basi umepata shari zote. Kumridhisha Allaah haina maana kwamba mtu asifanye zile sababu zitazofanya watu kutomkasirikia. Lakini hayo yasifanywe kwa kumkasirisha Allaah. Lakini kama kuna kitu kinachomkasirisha Allaah basi usikifanye. Katika hali kama hiyo usiwaogope watu, bali mtegemee Allaah. Katika upokezi mwingine kutoka kwa ´Aaishah imekuja:

“Yule mwenye kutaka radhi za Allaah kwa yanayowachukiza watu, basi Allaah atamtosheleza. Na yule mwenye kutaka radhi za watu kwa yanayomchukiza Allaah hatotoshelezwa nao dhidi ya Allaah – yule asiyemsifu atakuja kumsema vibaya.”

[1] at-Twabaraaniy (10514). Imezuliwa kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”adh-Dhwa´iyfah” (1482).

[2] at-Tirmidhiy (2414) na Ibn Hibbaan (276). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (6097).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 108-110
  • Imechapishwa: 23/10/2018