31. Mfano wa jinsi Maswahabah walivyokuwa wakiipa nyongo dunia


183- Kuna mwanachuoni ambaye alitaka kumjaribu ash-Shibliy akamwambia:

“Kwenye ngamia watano kunatolewa wangapi?” Akasema: “Kwa mujibu wa madhehebu yetu au madhehebu yenu?” Akasema: “Kwani mna madhehebu yenye kutofautiana na yetu?” ash-Shibliy akasema: “Ndio.” Mwanachuoni yule akasema: “Yepi?” Akasema: “Kwa mujibu wa madhehebu yenu kwenye ngamia watano kunatolewa kondoo mmoja na kwa mujibu wa madhehebu yetu kunatolewa zote.” Mwanachuoni yule akasema: “Madhehebu haya yana imaam?” ash-Shibliy akasema: “Ndio. Kiongozi wa waumini Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh). Alimpa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mali yake yote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Umewabakizia nini familia yako?” Abu Bakr akajibu: “Allaah na Mtume Wake.”[1]

184- al-Hasan amesema:

“Wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa khalifah alikhutubu akiwa na kikoi na viraka kumi na mbili.”

185- Qataadah amesema:

“Tumefikiwa na khabari ya kwamba ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Lau ningetaka ningekula chakula kizuri kabisa na ningevaa mavazi mazuri kabisa, lakini nimeyabakiza mazuri yangu kwa ajili ya Aakhirah.”

186- Hafsw bin al-´Aasw amesema:

“Nilikula chakula cha mchana na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh); mkate, mafuta, siki, maziwa, vinyama vya kukatwakatwa na chini ya hapo nyama mbichi. Alikuwa akisema: “Usifanye ubakhili kwa ung. Ndio chakula chote.”

187- Ama kuhusu ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´ann), inatosha kuonesha kuipa kwake kisogo dunia alitoa vifaa kuipa jeshi ngamia mia tatu, dinari elfu moja mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaichia nafsi yake ili tu Ummah usije kuingia katika fitina. Alikuwa akiwapa watu chakula cha kifalme ilihali yeye akenda nyumba ala mkate, siki na mafuta.

188- ´Abdullaah bin Shaddaad amesema:

“Nilimuona ´Uthmaan bin ´Afffaan akikhutubu siku ya Ijumaa. Alikuwa amevaa kikoi kinene kutoka Aden ambacho thamani yake ilikuwa dirhamu nne au tano.”

189- al-Hasan amesema:

“Twalhah bin ´Ubaydillaah aliuza ardhi kwa dirhamu 100.000. Pesa zikalala kwake usiku huo na akalala hali ya kuwa ni mwenye wasiwasi kwa sababu ya pesa hizo. Alipoamka zote akawagawia nazo masikini.”

190- Ziyaad bin Hudayr amesema:

“Nilimuona Twalhah bin ´Ubaydillaah akiketi msikitini na kuwagawia watu dirhamu 100.000.”

191- Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) alipokuwa akitaja siku ya Uhud akisema daima:

“Siku nzima ilikuwa ya Twalhah.”

192- az-Zubayr bin al-´Awaam alikuwa na watumwa elfu moja wakimkusanyia kodi ya majengo. Alikuwa akizigawa kila siku na akirudi nyumbani kwake hana kitu.

193- ´Abdur-Rahmaan bin al-´Awf alikuwa ni mmoja katika wale kumi walioahidiwa Pepo. Allaah awawie radhi. Alihajiri mara mbili kwenda Uhabeshi. Alishiriki katika vita vyote. Alisimama imara pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Uhud. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Rakaa´ moja nyuma yake na kusema:

“Hakuna Mtume anayekufa mpaka kwanza aswali nyuma ya mwanaume mwema katika Ummah wake.”

194- ´Abdur-Rahmaah bin al-´Awf alikuwa ni mmoja katika wale kumi waliobashiriwa Pepo na mmoja katika wale sita wa mashauriano walioteuliwa na ´Umar bin al-Khattwaab. Aliacha kuwa khalifah kwa sababu ya kuipa kisogo dunia ili waislamu wamchague yule Allaah aliyewachagulia.

195- Ninaomba kinga kwa Allaah dhidi ya ´Abdur-Rahmaan bin al-´Awf kwamba ataingia Peponi hali ya kutambaa kwa sababu ya pesa zake na utajiri wake[2]. Hivi kweli unafikiria kuwa wa awali aliyetangulia ambaye ni katika wale kumi halafu wale sita ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikufa hali ya kuwa yuko radhi naye, akapigana katika vita vya Badr na alikuwepo katika waliokuwa Hudaybiyah atatambaa? Kinga inatafutwa kwa Allaah! Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ

“Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi na akapigana.” (57:10)

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu chini ya mti.” (48:18)

Zinatosha kuonesha fadhila zake.

[1] at-Tirmidhiy (3920) na al-Haakim (1/414).

[2] Tazama http://wanachuoni.com/content/mwenye-kuzisahihisha-hadiyth-hizi-ni-mwongo

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 116-120
  • Imechapishwa: 18/03/2017