Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa kuamini uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na watu wataotoka Motoni baada ya kuungua na kuwa majivu. Watapelekwa kwenye mto karibu na mlango wa Pepo, kama ilivyopokelewa katika upokezi. Yatapitika namna anavyotaka Allaah na kama anavyotaka Allaah. Si vyengine isipokuwa inahusiana na kuamini na kusadikisha hilo.

MAELEZO

Kuamini uombezi ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na ´Aqiydah zao kuamini maombezi yote kwa ujumla na khaswa uombezi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Uombezi umethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) atampa idhini muombezi amuombee wapwekeshaji. Ni lazima sharti mbili hizi zitimie ili kupatikane uombezi.

Kuwaombea wapwekeshaji watenda madhambi ni moja katika misingi ya Ahl-us-Sunnah kama tulivosema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana fungu kubwa la maombezi haya kwa wapwekeshaji watenda madhambi. Alisema:

“Uombezi wangu umefanywa kwa watenda madhambi makubwa katika Ummah wangu.”

Atawaombea wapwekeshaji watenda madhambi. Mitume, Manaii na waja wema waumini pia wataombea.

Allaah atawaondoa watu Motoni watu ambao hawajapatapo kufanya kheri hapa duniani. Kisha watawekwa kwenye mto wa uhai ambapo watachipuka kama inavyochipuka mbegu iliyobebwa na mafuriko[1]. Roho zitarudi kwenye viwiliviwili vyao kisha waingie Peponi. Watapoona neema zinazowasubiri Peponi watadhani kuwa hakuna yeyote ambaye ana neema kama walizonazo.

Uombezi aina hii unapingwa na Mu´tazilah na Khawaarij. Wanajengea uelewa wao juu ya mfumo wao mbovu; kwamba yule ambaye ataingia Motoni hawezi kutoka ndani yake. Wanasema uongo pasi na shaka. Wameuwekea kikomo ukarimu wa Allaah; kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atawapa idhini Mitume, Malaika na waja wema kuombea mpaka Mola aseme:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na nusu dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na kokwa ya tende, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dudu mchungu na halafu yule ambaye yuko na imani ya chini chini chini kabisa kuliko dudu mchugu.”[2]

Haya yanaaminiwa na wale waumini wabora. Kwa hivyo unatakiwa kutambua na kusema kwamba miongoni mwa misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kuthibitisha kwamba Mitume, Malaika na waja wema watawaombea wapwekeshaji watenda madhambi. Walikuwa wakimwabudu Allaah pekee na wakiswali. Kwa msemo mwingine hawakufa katika kufuru kubwa, shirki kubwa na unafiki wa kiitikadi au upindaji mwingine unamtoa mtu nje ya Uislamu. Hawakufa hali ya kuwa ni wenye kuritadi kutoka katika dini. Walikufa hali ya kuwa ni waumini. Hata kama imani yao ina uzito sawa na dudu mchungu basi itakuwa ni sababu tosha kwa idhini ya Allaah waombezi kuwaombea. Hata kama wataadhibiwa kwa madhambi yao ambayo hawakusafishwa nayo duniani au Aakhirah. Watabakiwa wakiwa ni wachafu mpaka wasafishwe na Moto na wawe wasafi. Kwa sababu Pepo ni makazi ya wasafi na hakuna anayeingia ndani yake isipokuwa tu msafi. Na Moto ni makazi ya wachafu na hakuna atakayeingia ndani yake isipokuwa wachafu kama makafiri, wanafiki, washirikina, wapagani na wengineo wenye kuustahiki.

[1] al-Bukhaariy (6560) na Muslim (184).

[2] al-Bukhaariy (7439) na Muslim (183).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 87-88
  • Imechapishwa: 16/10/2019