2- ´Ibaadah ina sampuli nyingi na imekusanya aina zote za matendo mema yaliyo dhahiri katika ulimi na kwenye viungo vya mwili na yenye kutoka moyoni kama mfano wa kumtaja Allaah, kusema “Subhaana Allaah, Laa ilaaha illa Allaah”, kusoma Qur-aan, kuswali, kutoa zakaah, kufunga, kuhiji, kupambana Jihaad, kuamrisha mema, kukataza maovu, kuwatendea wema ndugu, mayatima, masikini, wasafiri, kumpenda Allaah na Mtume Wake, kumwogo Allaah na kurejea Kwake, kumtakasia Yeye nia, kusubiri juu ya hukumu Yake, kuridhia mipango Yake, kumtegemea Yeye, kutaraji rehema Zake na kuogopa adhabu Yake. ´Ibaadah ni yenye kuenea katika matendo yote ya muumini midhali atanuia kujikurubisha kwa Allaah au yanayomsaidia na ´ibaadah. Kunaingia mpaka mambo ya kimazowea maadamu atakusudia yampe nguvu katika kumtii Allaah. Kama mfano wa kulala, kula, kunywa, kufanya biashara, kutafuta riziki na kuoa. Mambo haya ya kiada yakiambatana na nia nzuri basi yanageuka kuwa ´ibaadah na mtu analipwa thawabu kwayo. ´Ibaadah si yenye kukomeka peke yake katika zile nembo zinazotambulika.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 57
  • Imechapishwa: 25/02/2020