30. Imani ni maneno na vitendo, inapanda na inashuka

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Imani ni maneno na matendo, inapanda na kushuka. Kama ilivyokuja katika mapokezi:

“Waumini walio na imani kamilifu zaidi ni wale walio na tabia bora zaidi.””[1]

MAELEZO

 Imani ni maneno na matendo na inapanda na inashuka. Tofauti na wanavosema Murji-ah ambao wanaona kuwa haipandi wala haishuki. Wanamaanisha kwamba imani ya waislamu watenda madhambi na imani ya Jibriyl (´alayhis-Salaam) ni sawasawa. Hili ni batili. Kuna dalili zinazoonyesha kuwa imani inapanda na inashuka. Amesema (Ta´ala):

وَيَزْدَادَ الَّذِينَ آمَنُوا إِيمَانًا ۙ وَلَا يَرْتَابَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ

“Iwazidishie imani wale walioamini na wala wasitie shaka wale waliopewa Kitabu.”[2]

وَيَزِيدُ اللَّـهُ الَّذِينَ اهْتَدَوْا هُدًى

“Allaah atawazidishia uongofu wale wenye kushika uongofu.”[3]

Salaf wamethibitisha kwamba chenye kupanda hushuka.

Kitu kinachothibitisha juu ya kutofautiana kwa imani ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu wa Peponi watawatazama watu wa vyumbani kama wanavyozitazama nyota wakati zinapopanda na kushuka kwa sababu ya kutofautiana baina yake.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hizi ni ngazi za Mitume ambazo hazifikiwi na yeyote?” Akajibu: “Sivyo hivyo! Ninaapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake ni watu waliomwamini Allaah na wakawasadikisha Mitume.”[4]

Miongoni mwa mambo yanayofahamisha hivo ni Hadiyth kuhusu uombezi ambapo Allaah (Ta´ala) atawaambia Malaika wake:

“Mtoeni Motoni yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na nusu dinari, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na kokwa ya tende, kisha yule ambaye moyoni mwake kuna imani sawa na dudu mchungu na halafu yule ambaye yuko na imani ya chini chini chini kabisa kuliko dudu mchugu.”[5]

Hii ni dalili juu ya kutofautiana kwa imani na kadhalika ngazi tofauti Peponi.

[1] Abu Daawuud (4682) na at-Tirmidhiy (1162). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[2] 74:31

[3] 19:76

[4] al-Bukhaariy (3256) na Muslim (2831).

[5] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 129-130
  • Imechapishwa: 24/04/2019