Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

 ”Na miongoni mwa ishara Zake ni usiku na mchana, jua na mwezi. Hivyo basi, msisujudie jua na wala mwezi, bali msujudieni Allaah ambaye ameliumba ikiwa Yeye pekee mnamwabudu.” (Fuswswilat 41 : 37)

Vilevile amesema (Ta´ala):

 إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akalingana juu ya ‘Arshi.” (al-A´raaf 07 : 54)

MAELEZO

Dalili – Dalili ya kwamba mchana na usiku, jua na mwezi, ni miongoni mwa alama za Allaah (´Azza wa Jall), ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ

”Na miongoni mwa ishara Zake ni usiku na mchana… “ (Fuswswilat 41 : 37)

Miongoni mwa alama za wazi na bainifu ni usiku na mchana katika dhati yake na katika kupishana kwake. Vilevile Allaah amevifanya ni vyenye kuwanufaisha viumbe na kuzibadilisha hali zao. Kadhalika jua na mwezi katika dhati yavyo, kutembelea kwake na nidhamu yavyo; vinachangia manufaa ya viumbe na kuwakinga na madhara.

Kisha Allaah (Ta´ala) akawakataza viumbe kulisujudia jua na mwezi pasi na kujali ile nafasi kubwa ya vitu hivyo. Kwa sababu vitu hivi havistahiki kuabudiwa kwa kuwa vimeumbwa. Yule anayestahiki kuabudiwa ni Allaah (Ta´ala) ambaye ameviumba.

Vilevile amesema… – Miongoni mwa dalili kwamba Allaah ameumba mbingu na ardhi ni maneno Yake (Ta´ala):

 إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akalingana juu ya ‘Arshi.” (al-A´raaf 07 : 54)

Ndani yake zipo alama za Allaah zifuatazo:

1- Allaah ameumba viumbe hivi vikubwa kwa muda wa siku sita na kama angelitaka angeliviumba kwa papohapo. Badala yake amefungamanisha visababishwaji kutokana na sababu zake mwa mujibu wa vile inavyopelekea hekima Yake.

2- Amelingana juu ya ´Arshi kwa kuweko juu yake ujuu ambao ni maalum na unaolingana na utukufu na ukubwa Wake. Hili linafahamsha ukamilifu wa nguvu na ufalme.

3- Anaufanya usiku kuufunika mchana kama nguo inavyofunika mwangaza wa mchana.

4- Allaah amefanya jua, mwezi na nyota kujisalimisha na amri Yake na anaviamrisha yale anayoyataka kutokana na manufaa ya viumbe.

5- Kuenea kwa nguvu Zake na ukamilifu wa ufalme Wake kwa sababu uumbaji na amri vyote viwili ni Vyake na si vya mwengine.

6- Kuenea kwa uola Wake kwa walimwengu wote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 20/05/2020