3. Fadhila za Tahmiyd, Tahliyl na Tasbiyh


06- Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له ، له الملك وله الحمد ، وهو على كل شيء قدير

“Hakuna mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyekuwa na mshirika. Ana ufalme na himdi na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”

kwa siku mara mia analipwa kuwa ameachia huru watumwa kumi, anaandikiwa thawabu mia na hufutiwa madhambi mia. Anakingwa na Shaytwaan siku iliyobaki mpaka inapofika jioni. Hakuna yeyote anayekuja na kitu bora kuliko yeye isipokuwa mtu aliyesema hayo zaidi yake.”

07- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusema:

سبحان الله وبحمده

“Ametakasika Allaah na himdi zote ni Zake.”

mara mia kwa siku hufutiwa madhambi hata kama yatakuwa ni mengi kama povu la kwenye bahari.”

08- Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna maneno mawili ambayo ni khafifu kwenye ulimi, mazito katika mizani na yanapendwa kwa Ar-Rahmaan:

سُبْحَانَ اللَّهِ ، وبِحَمْدِهِ سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ

”Ametakasika Allaah na himdi zote ni Zake. Ametakasika Allaah Mkuu.”

09- Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kwa mimi kusema:

سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر

“Ametakasika Allaah na himdi zote ni za Allaah na hapana mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Allaah ni Mkubwa.”

inanipendeza zaidi kuliko yote ambayo jua linaangaza juu yake.”

10- Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Maneno ambayo Allaah Hupenda zaidi ni mane. Lolote ambalo utakaloanza nalo hilo halikudhuru:

سبحان الله ، والحمدلله ، ولا إله إلا الله ، والله أكبر

“Ametakasika Allaah, himdi zote ni za Allaah. Hapana mola anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah. Allaah ni Mkubwa.”

11- Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni nani kati yenu anayeshindwa kuchuma kila siku thawabu elfu moja?” Mtu mmoja katika kikao akauliza: “Na ni vipi mmoja kati yetu ataweza kuchuma thawabu elfu moja?” Akasema: “Aseme: “Ametakasika Allaah” mara mia. Hivyo ataandikiwa thawabu elfu moja na atafutiwa madhambi elfu moja.”

12- Mama wa waumini Juwayriyah (Radhiya Allaahu ´anha) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka nyumbani kwake mapema asubuhi baada ya kuswali Swalah ya asubuhi wakati alipokuwa amekaa kwenye msala wake. Wakati kulipopambazuka alikuwa amekaa mahapa pale pale. Akasema: “Hukutoka katika hali hiyo tangu nilipokuacha?” Akajibu: “Hapana.” Hivyo akasema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Nimekariri maneno mane mara tatu baada yako. Lau yangelipimwa pamoja na hayo uliyoyasema basi yangelipima zaidi kuliko hivyo:

سبحان الله عدد خلقه سبحان الله رضا نفسه سبحان الله زنة عرشه سبحان الله مداد كلماته

“Ametakasika Allaah kiasi cha idadi kama ya viumbe Wake. Ametakasika Allaah kama Radhi Zake Mwenyewe. Ametakasika Allaah kama uzito wa ´Arshi Yake. Ametakasika Allaah kama idadi ya Maneno Yake.”

13- Amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia bedui mmoja:

“Sema:

لا إله إلا الله وحده لا شريك له الله أكبر كبيرا والحمد لله كثيرا سبحان الله رب العالمين لا حول ولا قوة إلا بالله العزيز الحكيم

“Hakuna mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mmoja asiyekuwa na mshirika. Allaah ni Mkubwa kweli kweli. Himdi nyingi ni Zake Allaah. Ametakasika Allaah Mola wa walimwengu. Hapana mabadiliko wala uwezo isipokuwa kwa msaada wa Allaah, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima na Mwenye hekima wa yote daima.”

Bedui akasema: “Haya ni kwa Mola Wangu. Ni yepi yangu?” Akajibu: “Sema:

اللهم اغفر لي وارحمني واهدني و عافنى وارزقني

“Ee Allaah! Nisamehe, nirahamu, niongoze, nipe afya na uniruzuku.”

14- Amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nilikutana na Ibraahiym usiku wa Israa´ na Mi´raaj. Akasema: “Ee Muhammad! Wafikishie Ummah wako salamu na waeleze kwamba Pepo ina udongo mzuri na maji matamu na ardhi yake ni bapa na shamba yake ni:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلا إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ

“Ametakasika Allaah, himdi zote ni za Allaah, hakuna mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Allaah ni Mkubwa”.”

15- Amesema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nisikueleze hazina miongoni mwa hazina za Peponi?” Nikasema: “Ndio, ewe Mtume wa Allaah.” Akasema: “Sema:

لا حول ولا قوة إلا بالله

“Hapana mabadiliko wala uwezo kwa msaada wa Allaah.”

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 24-28
  • Imechapishwa: 19/03/2017