28. Sharti ya sita ya swalah: Kufunika viungo visivyotakiwa


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya sita ni kufunika viungo ambavyo havitakiwi kuonekana (´Awrah). Wanachuoni wote wameafikiana juu ya kuharibika kwa swalah ya mwenye kuswali uchi ilihali anaweza kujifunika. Mpaka wa uchi wa mwanaume ni kuanzia kwenye kitovu mpaka kwenye magoti na vivyo hivyo kuhusu mjakazi. Ama mwanamke aliyehuru, mwili wake wote huzingatiwa kuwa ni haramu kuuonesha isipokuwa uso. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا بَنِي آدَمَ خُذُواْ زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

“Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu [mnapoenda] katika kila msikiti.”[1]

Bi maana katika kila swalah.

MAELEZO

Sharti ya sita ya kusihi kwa swalah ni kufunika vile viungo visivyotakikana kuonekana. Kwa  msemo mwingine aswali hali ya kuvifunika.

Wanachuoni wote wameafikiana… – Ibn ´Abdul-Barr (Rahimahu Allaah) amesema:

“Wale ambao wamefanya kufunika viungo visivotakiwa kuonekana ni miongoni mwa faradhi za swalah wamejengea dalili juu ya maafikiano ya kuharibika kwa swalah kwa yule ambaye ataacha nguo yake wazi ilihali ana uwezo wa kufunika na akaswali akiwa uchi.”[2]

Ambaye ataswali akiwa uchi ilihali ni mwenye uwezo wa kufunika viungo vyake visivotakiwa kuonekana basi swalah yake ni yenye kuharibika kwa maafikiano.

Mpaka wa uchi wa mwanaume… – Anatakiwa kufunika kilicho kati ya kitovu na magoti. Zipo ´Awrah aina mbili:

1 – ´Awrah kubwa ambayo ni ile tupu ya mbele na ya nyuma.

2 – ´Awrah nyepesi ambacho ni kile kinachofunikwa mpaka katika magoti. Kunaongezwa juu ya hilo kufunika mabega mawili wakati wa uwezo. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiswali mmoja wenu ndani ya nguo moja ilihali hakuna juu ya mabega yake chochote.”[3]

Kwa hivyo ni lazima mtu wakati wa kuswali afunike mabega yake.

Wanachuoni wametofautiana juu ya kusihi kwa swalah kwa ambaye ameswali na huku mabega yake yako wazi na ana uwezo[4]. Kwa hiyo haitakiwi kwa muislamu kuchukulia wepesi jambo hili na afunike mabega yake wakati anaswali.

Maneno yake:

“… na vivyo hivyo kuhusu mjakazi.”

Mjakazi ana hukumu moja kama mwanamme. Kikomo chake ni kuanzia kwenye kitovu hadi kwenye magoti.

Maneno yake:

“Ama mwanamke aliyehuru, mwili wake wote huzingatiwa kuwa ni haramu kuuonesha isipokuwa uso.”

Halazimiki kufunika uso wake. Baadhi ya wanachuoni wamesema isipokuwa tu kama atakuwa mrembo na anachelea fitina. Katika hali hiyo atalazimika kufunika. Makusudio neno ´mpaka` ni ndani ya swalah. Kuhusu nje ya swalah mwili wake wote hautakiwi kuonekana. Vivyo hivo akiwa ndani ya swalah lakini mbele ya wanaume wa kando naye. Katika hali hiyo afunike uso wake.

Mtoto wa kiume mdogo ambaye hajafikia kiwango cha kupambanua hana ´Awrah. ´Awrah inamuhusu yule mtoto ambaye ameshakuwa na uwezo wa kupambanua ambapo kikomo chake ni miaka saba. Hilo ni kutokana na Hadiyth isemayo:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofikisha miaka saba, wapigeni wanapofikisha miaka kumi na watenganishe baina yao katika malazi.”[5]

Maneno yake:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

خُذُواْ زِينَتَكُمْ

“Chukueni mapambo yenu [mnapoenda]… “

Malengo ya ´mapambo` ni nguo. Hakukusudiwi nguo nzuri. Nguo zimeitwa kuwa ni mapambo kwa sababu zinafunika vile viungo visivotakiwa kuonekana. Hivyo yanampamba mwanadamu. Kufunika viungo hivyo kunampamba. Kule kuacha viungo hivyo wazi kunapingana na jambo hilo. Maneno yake:

عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ

“… katika kila msikiti.”

Bi maana katika kila swalah.

[1] 07:31

[2] al-Istidraak (02/197).

[3] al-Bukhaariy (359) na Muslim (516).

[4] Tazama ”al-Mughniy” (01/338) na ”al-Majmuu´” (03/177).

[5] Abu Daawuud (495) na Ahmad (6756). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (1/266).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 29/12/2021