Kubaleghe kunapatikana kwa moja katika mambo matatu yafuatayo:

La kwanza: Kutokwa na manii kwa kuota au kwa njia nyingine. Amesema (Ta´ala):

وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ

“Matoto miongoni mwenu watakapofikia baleghe, basi waombe idhini kama walivyoomba idhini wale wa kabla yao.”[1]

Pia kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Josho la ijumaa ni wajibu kwa kila mwenye kuota.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

La pili: Kuota nywele sehemu za siri. Hayo ni kutokana na maneno ya ´Atwiyyah al-Quradhwiy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Tuliwadhihirisha [mateka] kwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Quraydhwah. Yule ambaye alikuwa ni mwenye kuota au nywele zake sehemu za siri zimekwishaota basi alikuwa anauliwa. Ambaye bado anaachwa.”

Ameipokea Ahmad na an-Nasaa´iy na ni Swahiyh.

La tatu: Kwa kufikisha miaka kumi na tano. ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Nilijidhihirisha kwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku ya Uhud na mimi nilikuwa mtoto wa miaka kumi na nne lakini hakuniidhinisha.”

Bi maana kwenda kupigana.

al-Bayhaqiy na Ibn Hibbaan wamezidisha katika “as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi Swahiyh:

“Hakuona kuwa nimekwishabaleghe. Nilijidhihirisha kwake siku ya [vita vya] Khandak na mimi nilikuwa mtoto wa miaka kumi na tano ambapo akaniidhinisha.”

al-Bayhaqiy na Ibn Hibbaan wamezidisha katika “as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi Swahiyh:

“… na akaona kuwa nimekwishabaleghe.”

Wameipokea wanachuoni.

an-Naafi´iy amesema:

“Nilikwenda kwa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz pindi alikuwa khaliyfah nikampasha khabari ambapo akasema: “Hicho ndio kidhibiti kati ya mdogo na mkubwa. Akawaandikia wafanya kazi wake wawafaradhishie (yaani zawadi) wale ambao wamebaleghe kwa miaka kumi na tano.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Msichana anabaleghe kwa njia ileile anayobaleghe mvulana. Lakini yeye kwake kunazidi jambo la nne ambalo ni hedhi. Pale tu ambapo msichana atapata hedhi basi amekwishabaleghe. Basi kuanzia hapo kalamu kwake itaanza kufanya kazi hata kama hajafikisha miaka kumi.

Kubaleghe kukitokea katikati ya mchana wa Ramadhaan yule mwenye kubaleghe akiwa katika hali ya kufunga basi atakamilisha swawm yake na hapana kitu juu yake. Akiwa hakufunga basi atalazimika kujizuia siku iliobaki. Kwa sababu ameingia katika wale watu ambao wanalazimika kufunga. Halazimiki kulipa siku hiyo kwa sababu hakuwa miongoni mwa watu wanaowajibika kufunga pale alipojizuia.

[1] 24:59

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 22/04/2020