130- Zayd bin Khaalid al-Juhaniy (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituswalisha Swalah ya Subh Hudaybiyah [baada ya usiku ulionyesha]. Wakati alipomaliza aliwageukia watu na kusema: ”Mnajua nini amesema Mola Wenu?” Wakasema: ”Allaah na Mtume Wake ndiyo wenye kujua zaidi.” Akasema: ”Baadhi ya waja wangu wameamka hali ya kuwa ni waumini na wengine makafiri. Waliosema: ”Tumenyeshelezewa kwa sababu ya fadhila na Rahmah za Allaah” wananiamini Mimi na wanakanusha nyota. Ama wale waliosema: ”Tumenyeshelezewa kwa sababu ya nyota kadhaa na kadhaa” anaamini nyota na amenikanusha Mimi.”

131- Anas (Radhiya Allaahu ´anhu) amesema:

”Kuna mtu mmoja aliingia Msikitini siku ya Ijumaa wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amesimama na kutoa Khutbah. Akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Mali imeangamia na njia zimekatika. Muombe Allaah Atupe mvua.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyoosha mikono na kuomba kwa kusema:

اللَّهُمَّ أَغِثْنَا، اللهُمَّ أَغِثْنَا

”Ee Allaah! Tupe mvua! Ee Allaah! Tupe mvua!”

Anas anaendelea kusema:

Ninaapa kwa Allaah kulikuwa hakuonekani mawingu wala mawingu yenye kutawanyika mbinguni na kulikuwa hakuna majengo wala nyumba kati yetu na Sal´[1]. Ghafla mawingu yakaanza kujitokeza nyuma yake. Wakati yalipokusanyika katikati ya mbingu yakasambaa. Kukaanza kunyesha. Ninaapa kwa Allaah hatukuona jua wiki nzima. Ijumaa kukaingia mtu kwenye mlango ule wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa amesimama na kutoa Khutbah na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Mali imeangamia na njia zimekatika Muombe Allaah aisimamishe.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyanyua mikono na kusema:

اللهُمَّ حَوَالَيْنَا ولا عَلَيْنَا اللهُمَّ عَلَى الآكام والظِّرَابِ وَبُطُونِ الأَودِية وَمَنَابِتِ الشَّجَرِ

”Ee Allaah! [Jaalia inyesheleze] kwetu wala isiwe dhidi yetu. Ee Allaah! [Jaalia inyesheleze] kwenye vichaka, milima, mabonde na kwenye mizizi ya miti.”

Mvua ikasimama na jua likachomoza.

[1] Ni mlima mmoja katika kaskazini mwa al-Madiynah.

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah§
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 88-90
  • Imechapishwa: 21/03/2017