28. Sharti ya tano ya swalah: Kuondosha najisi sehemu tatu


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya tano ni kuondosha najisi yote sehemu tatu; kwenye mwili, kwenye nguo na mahali pa kuswalia. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Nguo zako zisafishe.”[1]

MAELEZO

Maneno yake matunzi:

“Miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah ni kuondosha najisi yote sehemu tatu; katika mwili… “

Miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah ni kuondosha najisi yote sehemu tatu; katika mwili. Ni lazima mwili wako uwe msafi. Kukiweko najisi maeneo yoyote katika sehemu hizo swalah yako haisihi. Maneno yake:

“… kwenye nguo… “

Ni lazima nguo unayoswalia iwe safi. Ikiwa ina najisi basi swalah yako haitosihi mpaka uioshe.

Iwapo mtu ataswali katika nguo yenye najisi, ilihali hajui, basi swalah yake ni sahihi. Haya ndio maoni sahihi. Akikumbuka najisi katikati ya swalah basi atavua nguo hiyo ilio na najisi – kama mfano najisi hio iko katika kilemba au kofia – kisha ataendelea kuswali.

Maneno yake:

“… na mahali pa kuswalia.”

Ni lazima pale pahali anaposwalia pawe pasafi. Akiwa anaswali katika ardhi au zulia lenye najisi, basi swalah yake haitosihi.

Maneno yake:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ

“Nguo zako zisafishe.”

Makusudio ya ´nguo` ni matendo. Lakini kutokana na ueneaji wa Aayah kunajumuisha pia kusafisha mavazi.

[1] 74:04

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 29/12/2021