Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini kuwa al-Masiyh ad-Dajjaal atajitokeza. Kati ya macho yake kumeandikwa “kafiri”. Hadiyth zilizokuja juu ya hilo na kuamini kuwa hilo litakuwepo.

MAELEZO

ad-Dajjaal yuko na jina la “al-Masiyh” kama alivyonalo ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam). ad-Dajjaal anaitwa al-Masiyh ad-Dajjaal na ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Salaam) anaitwa al-Masiyh ´Iysaa bin Maryam.

Ameitwa hivo ima kwa sababu atatembea (يمسح) ulimwenguni kote kwa muda wa masiku maalum aliyopangiwa au kwa sababu jicho lake la upande wa kulia limefutwa  (ممسوح).

Zimekuja Hadiyth nyingi zinazomweleza, kujitokeza kwake na fitina atazokujanazo. Atakuwa na pepo na moto. Kwamba ataiamrisha mbingu iteremshe mvua na ardhi itoe mazao. Atakuwa ni mtihani kwa watu, atawaamrisha wamwamini na kuwaeleza kwamba yeye ndiye mola wao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna Mtume yeyote isipokuwa aliwatahadharisha Ummah wake juu ya ad-Dajjaal. Nitakwelezeni jambo ambalo halikusemwa na Mtume mwingine kabla yangu; yeye ni mwenye chongo. Jicho lake la kulia ni kama zabibu yenye kuhamahama. Hakika bila shaka Mola wenu si mwenye chongo.”[1]

[1] al-Bukhaariy (4403) na Muslim (169).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 125-126
  • Imechapishwa: 24/04/2019