26 – Baadhi ya dalili kwamba Sayyid Qutwub amesema kuwa Qur-aan imeumbwa

Baadhi ya dalili ni:

1- Ni mmoja katika wale wenye kuzikanusha sifa za Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hana mafungamano yoyote na Ahl-us-Sunnah katika suala hili. Amekanusha sifa ya Allaah kulingana juu ya ´Arshi[1] na kuja Kwake siku ya Qiyaamah. Isitoshe amekanusha mikono miwili ya Allaah, Kursiy na mahala pa kuweka miguu, au angalau kwa uchache anavitilia shaka, na amekanusha mshiko wa Allaah na unyooshaji Wake [wa mikono] na kwamba ´Iysaa amenyanyuliwa juu mbinguni.

Niliyakusanya maneno na mijadala yake katika kitabu changu “Adhwaa´ Islaamiyyah”. Je, mtu kweli atarajie kutoka kwa mtu kama huyu kuwa atamkaripia yule mwenye kusema kuwa Qur-aan imeumbwa? Je, mtu kweli atarajie kuwa atapita juu ya njia ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na kusema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa na kwamba kusema kuwa Qur-aan imeumbwa ni kufuru au Bid´ah? Kwa ajili hii ndio maana hatukupata neno hata moja kutoka kwake, moja kwa moja au isiyokuwa moja kwa moja, akiashira kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba haikuumbwa.

2- Ana utofauti kwa kuchukua tahadhari iliokuwa kubwa asije kukosolewa. Kwa ajili hiyo ndio maana anatumia ibara zisizokuwa za wazi katika masuala ambayo yeye mwenyewe anajiona kuwa anaenda kinyume na Ahl-us-Sunnah au wanachuoni wengine. Ni watu wengi wasioona hilo. Hakuna wanaolitambua isipokuwa tu wale wenye maarifa na uoni. Kwa njia hiyo anajilinda yeye mwenyewe kutokamana na ukosoaji.

Kwa mfano al-Ikhwaan al-Muslimuun wamesema wazi kuwa wananusuru ujamaa ambao wanaeleza vilevile kuwa ni wa Kiislamu. Wameandika vitabu juu ya mada hiyo na wamepotosha maandiko katika Qur-aan na Sunnah. Ndipo baadhi yao wakaanza kukosoa hili na kuwaita kuwa ni wakomunisti, kama alivyofanya kitu kama hicho Muhammad al-Ghazaaliy katika kitabu “al-Islaam al-Muftaraa ´alayh”. Hilo Sayyid Qutwub akalitambua na akachukua tahadhari kubwa pindi alipoandika kitabu chake “al-´Adaalah al-Ijtimaa´iyyah”. Alikipa kitabu kichwa cha khabari hichi na ndani yake akathibitisha ujamaa kwa njia ya nguvu kabisa. Upande mwingine watu wanafikiria kuwa yote hayo anatumia dalili kwa Qur-aan na Sunnah na misingi ya dini. Hakuna sehemu hata moja, wala kwenye kitabu, ametaja neno “ujamaa” pindi alipokuwa akithibitisha ujamaa, pamoja na kuwa kama alivyosema al-Khaalidiy, anatumia neno “al-Ijtimaa´iyyah” badala ya “Shuyuu´iyyah” (Ukomunisti) na “Ishtiraakiyyah” (Ujamaa). Usistaajabishwe na usulubu huu kwa mwanasiasa ambaye ameutumia uhai wake wote katika siasa.

3- Siwezi kufikiria kuwa Sayyid katika maisha yake yote marefu ya kimasomo na ya kisiasa hakusikia kunazungumziwa fitina kubwa iliyotokea kati ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na Mu´tazilah inapokuja katika Qur-aan na kwamba Ahl-us-Sunnah walisema kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah yaliyoteremshwa hayakuumbwa, Kwake ndiko yalikoanza na Kwake ndiko yatarudi. Mu´tazilah walisema kuwa Qur-aan imeumbwa. Walitumia msaada wa nguvu za mfalme na wakatumia nguvu za makhaliyfah watatu – al-Ma´muun, al-Mu´taswim na al-Waathiq – ili kuwafunga, kuwaua na kuwatimua Ahl-us-Sunnah. Jambo hilo linajulikana vyema mpaka hii leo. Hakuna hata ambaye ana maarifa na elimu chache kuliko Sayyid ni mjinga juu ya hilo.

4- Nimepata namna ambavyo Sayyid Qutwub katika “Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan” na katika vitabu vingine anakanusha kuwa Allaah anazungumza na anaonelea kuwa maneno ya Allaah ni utashi tu. Kwa mfano anasema katika “as-Salaam al-´Aalami wal-Islaam”[2]:

“Kupitia Mungu huyu mmoja ndio ulimwengu ukawa kwa njia moja:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa! – nacho huwa.”[3]

Hakuna ukati kati baina ya utashi wa muumba na kiumbe. Ulimwengu huu hauji kwa njia nyingine kutoka kwa yule Muumbaji mmoja. Inahusiana tu na matakwa ambayo yanaabiriwa na Qur-aan kwa neno “Kuwa”. Matakwa haya yanatosheleza ili ulimwengu utoke kwayo.”

Maneno haya yana maana gani? Mtu huzungumza namna hii ikiwa anaamini kuwa Allaah anaongea akitaka na pindi anapotaka?

Anasema katika “Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan”:

“Maneno Yake (Ta´ala) ni utashi/matakwa[4] ambayo ndio kiumbe kikusudiwacho kinapotoka.”

Huu ni ukanushaji wa wazi juu ya maneno ya Allaah ambayo wazi wazi yamethibitishwa na Qur-aan, Sunnah na Salaf. Anasema vilevile katika “Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan”:

“Ulimwengu huu umetoka kutoka kwa Muumbaji Wake kupitia utashi msafi na wenye uwezo “Kuwa!”. Kuuelekeza utashi tu kwenye kiumbe chochote kile inatosha ili kiwepo namna hii, bila ya ukati kati baina ya nguvu na vyenzo.”

Anaposema “bila ya ukati kati” anakanusha maneno ya Allaah.

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ

“Basi alipoufikia aliitwa: “Ee Muusa!”[5]

Sayyid Qutwub amesema katika mnasaba wa Aayah hii:

“Haiwezi kujulikana maneno haya yametoka wapi wala muelekeo wake uko wapi au uhalisia wa sura yake au namna yake au ni vipi Muusa aliyasikia au ni kwa njia gani yalipokewa. Ni katika maamrisho ya Allaah. Tunaamini kuwa yalitokea pasi na kuuliza namna yake ambayo ni jambo lisilowezekana kwa mwanaadamu kulielewa.”

Maandiko haya ni dalili ya wazi ya kwamba Sayyid Qutwun haonelei kuwa Allaah anazungumza na kwamba haumbi kwa neno Lake, kama ilivyo wazi katika Qur-aan na kama ilivyo ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Badala yake anaonelea kuwa Allaah anaumba tu kwa utashi pasi na ukati kati wowote. Ukati kati unaokanushwa hapa ni neno na maneno. Anayesema yote yaliyotangulia anaamini kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah na kwamba haikuumbwa kwa njia ile wanayoamini Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah?

Kujengea yote yaliyotangulia nasema kwa kukata ya kwamba Sayyid Qutwub anaonelea kuwa Qur-aan imeumbwa. Anaposema kuhusu Qur-aan:

“Shani ya miujiza hii ni kama shani ya viumbe vyengine vyote vya Allaah, nayo ni kama uundaji wa Allaah katika kila kitu.”

anamaanisha kuwa Qur-aan imeumbwa. Tamko hili peke yake linatosha mtu kusema kwamba anaonelea kuwa Qur-aan imeumbwa na ili kumkandamiza yule mwenye kumpingia hilo.

Hivi kweli mtu mwenye busara na aliye na inswafu anaweza kuona sababu yoyote ya sawa Shaykh Bakr kusema pindi anaponikaripia kwa kuwa nimesema kuwa Sayyid Qutwub anasema kuwa Qur-aan imeumbwa:

“Ni vipi mtu kwa urahisi anaweza kumtuhumu mtu kwa kufuru hizi?

Ikiwa hukumu yangu imejengwa juu ya dalili hizi zenye nguvu inazingatiwa kuwa ni hukumu nyepesi, sio sahihi kumhukumu yeyote hukumu hii si katika ´Aqiydah wala mengine. Katika hali hii mtu kamwe hawezi kuona kuwa mtu amesimamikiwa na hoja na katika hali hii mabwana wa kisufi na madhehebu batili yangelishinda.

Kuhusu dalili yako kwamba ´Adhwiymah alisema juu ya Qur-aan yale yaliyosemwa na Sayyid Qutwub, ni ajabu sana. Ni nani aliyesema kuwa maneno ya ´Adhwiymah na watu mfano wake ni hoja? Unakumbuka kuwa Shaykh-ul-Islaam anasema kuwa hakuna maneno ya yeyote yanayotumiwa kuwa ni hoja na kwamba badala yake wao wenyewe wanatakwa hoja. Lau ingelikuwa sahihi kutumia hoja kwa maneno ya baadhi ya maimamu, nauliza ni nani ´Adhwiymah mpaka mtu kama wewe uweze kutumia maneno yake. Unajua uongozi wake katika dini? Ni nani aliyechapisha kitabu chake na kuyakubali maneno yake batili yaliyomo humo? Je, ni maimamu wa Uislamu au ni wanafunzi wa Sayyid Qutwub?

[1] Tafsiri yake ya Suurah “Twaa Haa” (04/2328) katika “Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan” alipokuwa akifasiri Aayah ya Allaah (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa Rahmah amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

“Kulingana juu ya ´Arshi ni kinaya ya utawala mkamilifu.”

[2] Uk. 15.

[3] 36:82

[4] Yaani sio maneno.

[5] 20:11