25. Shirki kubwa na yale yanayopelekea kwayo


Shirki ni aina mbili:

1- Shirki kubwa.

2- Shirki ndogo.

Shirki kubwa: Shirki kubwa ni kufanya kitu katika aina za ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah, kama tulivyotangulia kusema. Aina hii inamtoa mtu katika Uislamu. Aina hii inamharamishia mwenye nayo kuingia Peponi na inamdumisha Motoni milele. Aina hii inaharabu matendo yote. Aina hii inahalalisha damu na mali. Shirki hii ni mbaya kwa njia nyingi:

1- Inamfanya yule mwenye nayo kuwa kafiri na mshirikina:

2- Allaah kamharamishia kuingia Peponi, makazi yake ni Motoni  na madhalika hawatopata mwenye kuwanusuru. Amemharamishia bi maana amemzuia kuingia Peponi kabisa. Kwa ajili hii ndio maana amesema:

وَمَأْوَاهُ النَّارُ

“… makazi yake yatakuwa ni Motoni.”

3- Allaah (´Azza wa Jall) kawaharamishia washirikina msamaha. Amesema (Ta´ala):Pindi alipoharamishiwa Pepo Moto ndio ikawa makazi yake milele. Hatotoka humo kabisa.

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.” (an-Nisaa´ 04:48)

Mshirikina akifa katika shirki [kubwa], hakuna matumaini yoyote kwake kupata msamaha wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) midhali hakutubia. Isipokuwa msahama – midhali mtu hakuwahi kutubia – ni kwa madhambi yaliyo chini ya shirki:

وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

”… na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”

Uzinzi, kuiba, kunywa pombe na yasiyokuwa hayo katika mambo ya haramu  na madhambi makubwa. Yote hayo yako chini ya utashi wa Allaah ilimradi hayajafika katika kiwango cha shirki. Akitaka atawasamehe wenye nayo na akitaka atawaadhibu kwa kiasi cha madhambi yao kisha baadaye atawatoa Motoni na kuwaingiza Peponi kutokana na Tawhiyd na imani yao. Hawa ndio wanaitwa wapwekeshaji watenda madhambi. Lakini iwapo hawatosamehewa hawatodumishwa Motoni milele kama watavyodumishwa Motoni milele makafiri, waabudu masanamu na washirikina wengine.

4- Shirki inaharibu matendo yote. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ

“Hakika umeletewa Wahy na kwa wale walio kabla yako [kwamba]: “Ukifanya shirki, bila shaka yataporomoka matendo yako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. Bali Allaah pekee mwabudu na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.” (az-Zumar 39:65-66)

Kwa hili wanasema hakika shirki inaharibu matendo kama jinsi hadathi inavyoharibu twahara. Mtu akitawadha kisha akapatwa na hadathi, twahara yake inaharibika. Kadhalika akishuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah kisha akashirikisha, Tawhiyd yake inabatilika na matendo yake yanabatilika. Kwa sababu shirki inabatilisha matendo kama jinsi hadathi inavyoharibu twahara. Amesema (Ta´ala) pindi alipowataja baadhi ya Mitume katika Suurah “al-An´aam”:

وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ

”… Nuuh tulimhidi hapo kabla, na katika kizazi chake Daawuud na Sulaymaan… “(al-An´aam 06:84)

mpaka aliposema:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”… lau wangemshirikisha bila shaka yangewaharibikia yale waliyokuwa wakitenda.” (al-An´aam 06:88)

Pamoja na kuwa ni Mitume, lakini lau tutakadiria kwamba wangelimshirikisha Allaah matendo yao yangeporomoka. Kama ambavyo Allaah alimwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

“Ukifanya shirki, bila shaka yataporomoka matendo yako.” (az-Zumar 39:65)

“Mwenye kufa naye anamuomba mshirika badala ya Allaah ataingia Motoni”  na mimi[1] nikasema: “Mwenye kufa naye haombi mshirika badala ya Allaah ataingia Peponi.”[2]Mtu haitomfaa ´amali yoyote aliyofanya ikiwa imechanganyika pamoja na shirki au akayafanya baada ya kufanya shirki na asitubie, yote yanaharibika. Kwa sababu shirki inaharibu matendo. Na akifa juu yake anakuwa ni katika watu wa Motoni wataodumishwa humo milele. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

5- Shirki inahalalisha damu ya mshirikina na mali yake na ni wajibu kumpiga vita. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kupigana vita na watu mpaka waseme “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”, watapoitamka basi imesalimika kwangu damu na mali yao isipokuwa kwa haki yake na hesabu yao iko kwa Allaah.”[3]

Haisalimiki mali na damu isipokuwa kwa Tawhiyd. Ama shirki inahalalisha damu na mali kwa kupigwa vita wenye nayo. Hii ndio shirki na zile adhabu zinazopelekea kwayo duniani na Aakhirah. Ni aina nyingi. Kubwa katika hizo ni pamoja vilevile na kumuomba asiyekuwa Allaah, kutaka uokozi kwa asiyekuwa Allaah kwa mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah pekee, kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, kumsujudia asiyekuwa Allaah, kumuwekea nadhiri asiyekuwa Allaah, kurukuu kwa asiyekuwa Allaah na mengineyo. Atakayefanya kitu katika aina za ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah, basi kafanya shirki tena kubwa.

[1] Bi maana mpokezi ambaye ni ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Maneno yake haya yamekuja hali ya kurufaishwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa Jaabir. Ameipokea Muslim (93).

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (4497) na Muslim (92) kupitia kwa ´Abdullaah bin Mas´uud.

[3] Ameipokea Muslim (21) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). al-Bukhaariy (25) na Muslim (22) wamepokea mfano wake kwa kutaja vilevile swalah na zakaah kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 13/07/2018