25. Mfano wa aina za uchawi


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Ahmad amesema: “Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: ´Awf ametuhadithia, kutoka kwa Hayyaan bin al-´Alaa´: Qutwn bin Qabiyswah ametuhadithia, kutoka kwa baba yake ambaye amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“´Iyaafah, Twarq na at-Twiyarah ni katika Jibt.”

´Awf amesema:

“´Iyaafah ni kumshtua ndege aruke, Twarq ni misitari inayochorwa katika ardhi na Jibt, al-Hasan amesema, ni nyimbo ya shaytwaan.”[1]

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake pia ana upokezi wenye cheni ya wapokezi ilioungana kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota basi atakuwa amejifunza sehemu katika uchawi. Vile anavyojizidishia hujizidishia.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.

3- an-Nasaa´iy amepokea kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) isemayo:

“Atakayefunga fundo kisha akalipuliza, basi atakuwa amefanya uchawi. Mwenye kufanya uchawi atakuwa ameshirikisha. Atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”[3]

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikwambieni ni nini ´Adhwh? Ni kueneza uvumi baina ya watu.”

Ameipokea Muslim.

5- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika katika ufasaha kuna uchawi.”[4]

MAELEZO

Mwandishi anachotaka ni kutoa baadhi ya mifano ya uchawi ili kumzindua muumini, ajiepushe nao na kujiweka nao mbali. Uchawi unaweza kuitwa kwa njia fulani kwa sababu unadhuru na kukera ijapokuwa uhalisia wa mambo sio uchawi wa aina ya kuwatumia na kuwaabudu mashaytwaan. Hili la pili ni uchawi safi kabisa na lile la kwanza lina athari ya uchawi.

1- Ahmad amesema: “Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: ´Awf ametuhadithia, kutoka kwa Hayyaan bin al-´Alaa´: Qutwn bin Qabiyswah ametuhadithia, kutoka kwa baba yake ambaye amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“´Iyaafah, Twarq na at-Twiyarah ni katika Jibt.”

´Awf amesema:

“´Iyaafah ni kumshtua ndege aruke, Twarq ni misitari inayochorwa katika ardhi na Jibt, al-Hasan amesema, ni nyimbo ya shaytwaan.”

Jibt ni uchawi, kama alivosema ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).

Mambo haya yanaitwa kuwa ni uchawi kwa sababu ya ile shari na ufisadi unaopatikana ndani yake na kwa sababu wafanyayo hayo wakati mwingine wanaweza kudai kujua mambo yaliyofichikana.

´Iyaafah ni kumshtua ndege akaruka, kama alivosema ´Awf. Wanamshtua na wanadai kwamba atawaelekeza juu ya kitu. Wakati fulani huamini mkosi na wakati mwingine wanakuwa na matumaini. Haya ni katika matendo ya kipindi cha kikafiri. Ndege hana kheri wala shari. Haya yanaonyesha ujinga waliokuwa nao watu hawa. Walikuwa wakiamini mkosi kwa jogoo, bundi na wanyama wengine wabaya na wanakuwa na matumaini na kuamini bahati nzuri wanapowaona wanyama wazuri na wanaona kuwa kuna matokeo mazuri.

Twarq ni msitari unachorwa ardhini. Baada ya kuchora wanasema kuwa ni dalili yenye kuonyesha kuwa jambo fulani litatokea. Wakati fulani jambo hilo linaweza kuhusiana na mchezo na wakati mwingine yanaweza kuwa ni mambo ya kiini-macho/mazingaombwe. Uhalisia wa mambo ni kuwatumikia mashaytwaan na kuwatii. Aidha wanadai kwamba wanajua mambo yaliyofichikana. Yote hayo ni uongo usiofidisha kitu.

Jibt ni nyimbo ya shaytwaan.

Twiyarah ni kuamini nuksi kwa kitu cha kuonywa au cha kusikiwa. Kuamini mkosi na nuksi ni haramu na ni shirki ndogo. Inaweza vilevile ikawa shirki kubwa ikiwa mtu ataamini kuwa ndege huyo anaendesha ulimwengu na au uwezo wa kuendesha kitu. Lakini mara nyingi watu huamini mkosi wake tu.

Yote haya ni katika mambo ya kipindi cha kikafiri na ni katika mazimwi. Imesemekana vilevile kwamba ni katika sanamu au kitu kisichokuwa na kheri ndani yake. Kinachokusudiwa ni kwamba kuwashtua ndege kwa njia kama hii imekatazwa kwa sababu ni kujifananisha na matendo ya watu wa kipindi cha kikafiri.

Maneno “Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake pia ana upokezi wenye cheni ya wapokezi ilioungana kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunamaanishwa Hadiyth:

“´Iyaafah, Twarq na at-Twiyarah ni katika Jibt.”

Yaliyo baada yake yako kwa Ahmad peke yake.

2- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayejifunza sehemu ya elimu ya nyota basi atakuwa amejifunza sehemu katika uchawi. Vile anavyojizidishia hujizidishia.”

Ni dalili inayothibitisha kwamba elimu ya unajimu unaohusiana na kuathiri katika ulimwengu ni batili. Inahusiana na mtu kuamini tafaasiri juu ya nyota zinamaanisha kufa kwa mtu, kuwa hai kwa mtu, kuondoka utawala wa mtu fulani na mfano wa hayo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Vile anavyojizidishia hujizidishia.”

Bi maana kila anavyojizidishia kujifunza elimu ya unajimu ndivo pia anavyojizidishia uchawi na shari. Kinachokusudiwa hapa ni kwamba nyota zina taathira katika ulimwengu. Ni dhambi kuamini hivo. Hata hivyo ni sawa kufaidika na nyota na sayari ili mtu kujua ni wapi Qiblah kipo na hali ya hewa. Elimu kama hiyo ni katika neema za Allaah.

Miongoni mwa aina za kuamini mikosi za leo ni kutochinja, kutonunua na kutokuoa katika Swafar. Ni kitendo cha kipindi cha kikafiri.

3- an-Nasaa´iy amepokea kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) isemayo:

“Atakayefunga fundo kisha akalipuliza, basi atakuwa amefanya uchawi. Mwenye kufanya uchawi atakuwa ameshirikisha. Atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”

Mwandishi wa kitabu anachotaka ni kutoa baadhi ya mifano ya uchawi kukiwemo kupuliza kwenye fundo. Wachawi hufunga vifundo kisha wanapuliza ndani yake kwa pumzi zao mbaya. Aidha wanashirikiana na kuwatumikia mashaytwaan. Halafu yanatokea baadhi ya malengo yao kwa idhini ya Allaah. Amesema (Subhaanah):

وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ

“Wao hawawezi kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah.” (al-Baqarah 02:102)

Bi maana kwa idhini Yake ya kilimwengu. Ametaja uchawi pale aliposema:

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ

“Na kutokana na uchawi wa wanaopuliza vifundoni.” (al-Falaq 113:04)

Ni wachawi.

Uchawi umegawanyika aina mbili:

1- Uchawi unaokuwa kwa vifundo, kupuliza na madawa ya kudhuru. Haya yapo.

2-  Uchawi unaokuwa kiini-macho na talbisi. Allaah amesema kuhusu wachawi wa Fir´awn:

فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ

”Tahamaki kamba zao na fimbo zao zikaonekana kwake kutokana na uchawi wao kwamba zinakwenda kwa haraka.” (Twaahaa 20:66)

فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ

“Basi walipotupa [fimbo zao] wakayasihiri macho ya watu na wakawatia woga na wakaja na uchawi mkubwa.” (al-A´raaf 07:116)

Allaah amesema kuwa chawi wao ulikuwa mkubwa kutokana na vile ulivyowababaisha watu na kuwachanganya machoni mwao.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufanya uchawi atakuwa ameshirikisha.”

Kwa sababu kufanya uchawi kunakuwa kwa kuwaabudu mashaytwaan na kuwaomba. Kwa ajili hiyo ndio maana amesema:

وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru, wanafundisha watu uchawi na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika [mji wa] Baabil, Haaruut na Maaruut. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme [kumwambia mtu huyo]: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.” (al-Baqarah 02:102)

Ni dalili inayothibitisha kwamba kujifunza uchawi ni ukafiri.

Cheni ya wapokezi wa Hadiyth hii ni dhaifu kwa sababu al-Hasan ameipokea kutoka kwa Abu Hurayrah. Kundi la wanachuoni wamesema kuwa al-Hasan hakuisikia kutoka kwa Abu Hurayrah. Kwa hivyo Hadityh inakuwa yenye kukatika. Imepokelewa kupitia kwa ´Ubaadah bin Maysarah na ndani yake kuna udhaifu. Lakini Hadiyth ina yenye kuyatia nguvu kwa upande wa maana.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayejifungamanisha na kitu basi huwakilishwa kwacho.”

Mwenye kujifungamanisha na Allaah basi huwakilishwa kwa Allaah kwa msemo mwingine Allaah humtosheleza kutokamana na dhiki zake:

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ

”Je, kwani Allaah si Mwenye kumtosheleza mja Wake?” (az-Zumar 39:36)

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Yeyote anayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.” (at-Twalaaq 65:03)

Na yule mwenye kujifungamanisha na kuutegemea uchawi, hirizi na mashaytwaan basi  Allaah humfungamanishia mambo hayo. Yule atakayemtegemea mwengine asiyekuwa Allaah basi amekhasirika na kuangamia.

4- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikwambieni ni nini ´Adhwh? Ni kueneza uvumi baina ya watu.”

Ameipokea Muslim.

Mtunzi wa “al-Qaamus” amesema:

“´Adwh ni uchawi, uongo na uvumi.”

Ameutaja katika mazingira haya kwa sababu uchawi unapelekea katika uzushi, uongo, talbisi na kughushi kati ya watu.

(Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni kueneza uvumi baina ya watu.”

Uvumi umeitwa hivo kwa sababu unawadhuru watu na unapelekea katika uongo, uzushi na kuharibu kati ya watu. Kwa ajili hii amesema Yahyaa bin Abiy Kathiyr:

“Mvumi na mwongo wanaweza kuharibu kwa saa moja mengi kuliko yale yanayoweza kuharibiwa na mchawi kwa mwaka mmoja.”

Hivo ndivo alivyopokea Ibn ´Abdil-Barr kutoka kwake. Shari yao ni kubwa. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hatoingia Peponi mvumi.”[5]

 5- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika katika ufasaha kuna uchawi.”

Kwa sababu mtu mwenye ufasaha anaweza kuwaroga watu kwa usulubu na ufasaha wake. Huenda akawababaisha. Huenda akawahadaa na wasibainikiwe na ukweli wa mambo. Wengi wanasema kuwa Hadiyth inasifia ufasaha ikiwa inahusiana na haki. Wengine wanasema kuwa ufasaha unasemwa vibaya, kama alivosema Ibn ´Abdil-Barr kutoka kwa baadhi ya wanachuoni. Lakini hata hivyo ufasaha ikiwa unahusiana na haki na kulingania katika Qur-aan na Sunnah basi ni wenye kusifiwa kama ambavyo ni wenye kusemwa vibaya ikiwa utatumiwa katika kuhadaa na kuwababaisha watu. Hadiyth inaweza kuwa na maana zote mbili. Qur-aan na Sunnah vimekuja kwa ubainisho wa wazi na ufasaha katika kubainisha haki na kuwaita watu katika haki hiyo. Kuna mtu aliyekhutubu kwa ufasaha kabisa mbele na wakati wa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz ambapo akasema:

“Huu ni uchawi halali.”

[1] Abu Daawuud (3907), Ahmad (20623), at-Twabaraaniy (941) na al-Bayhaqiy (16292). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf-ul-Jaami´” (8336).

[2] Abu Daawuud (3905), Ibn Maajah (3726), Ahmad (2841) na al-Bayhaqiy (16290). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (11019).

[3] an-Nasaa’iy (4079) na at-Twabaraaniy katika ”al-Awsatw” (1469). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Ghayaat-ul-Maraam” (288).

[4] Muslim (2606).

[5] Muslim (105).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 90-93
  • Imechapishwa: 12/10/2018