24. Ngawira ya kwanza katika Uislamu


Baada ya hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtuma ´Abdullaah bin Jahsh bin as-Asdiy na Muhaajiruun wengine saba. Akamwandikia barua na akamuamrisha asiisome mpaka baada ya kusafiri siku mbili na wala asimlazimishe yeyote kwa yale yaliyomo ndani ya barua. Akafanya kama alivyoelekezwa. Wakati alipofungua barua akakuta ndani kuna yafuatayo:

”Wakati utapofungua barua basi aendelea mpaka utapotua katika miti ya mtende ilioko baina ya Makkah na at-Twaaif. Hapo ndipo utawafuatilia Quraysh na utatujulisha kuhusu khabari zao.”

Akasema:

”Nasikiliza na natii.”

Akawaeleza wenzake kuhusu kazi ile na kwamba hakuna yeyote anayelazimishwa; yule mwenye kupenda kufa kama shahidi basi asimame na yule anayechukia mauti arudi nyuma. Akasema:

”Kuhusu mimi nitasimama.”

Walipokuwa njiani  Sa´d bin Abiy Waqqaas na ´Utbah bin Ghazwaan wakapoteza ngamia wao ambaye walikuwa wakipokezana kumpanda. Wakaenda kumtafuta na hivyo wakaja nyuma ya wengine. ´Abdullaah bin Jahsh akaendelea na safari yake mpaka alipofika katika ile mitende. Akapita karibu na msafara wa Quraysh ambao ulikuwa umebeba zabibu, ngozi na bidhaa zengine za biashara kwenye mabegi yao. Katika msafara huo alikuwepo ´Amr bin al-Hadhwramiy, ´Uthmaan na Nawfal watoto wawili wa ´Abdullaah bin al-Mu ghiyrah na al-Hakam bin Kaysaan. Waislamu wakashauriana na kusema:

”Sisi tuko katika siku ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Rajab. Tukiwapiga vita tutakuwa tumejikosesha mwezi mtukufu. Na tukiwaacha usiku huu wataingia Haram.”

Hatimaye wakakubaliana juu ya kuwashambulia. Mmoja wao akamrushia mshale ´Amr bin al-Hadhwramiy na akamuua. ´Uthmaan na al-Hakam wakashikwa mateka. Nawfal akakimbia.

Kisha wakarudi na misafara na mateka wawili. Moja ya tano ikawekwa pembeni. Hiyo ndio ilikuwa ngawira ya kwanza katika Uislamu na sehemu moja ya tano iliyopiganiwa katika Uislamu. Hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza mtu kuuawa katika Uislamu na kadhalika ndio ilikuwa mara ya kwanza mtu kutekwa mateka katika Uislamu. Pamoja na hivyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawakataza ijapokuwa kitendo chao (Radhiya Allaahu ´anhum) kilikuwa kimejengwa juu ya Ijtihaad.

Quraysh wakalikemea jambo hilo kwa ukali kabisa na wakasema:

”Muhammad amehalalisha miezi mitukufu.”

Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ ۖ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ ۖ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللَّـهِ ۚ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ

”Wanakuuliza kuhusu kupigana ndani ya mwezi mtukufu. Sema: “Kupigana ndani yake ni dhambi kubwa, lakini kuzuia njia ya Allaah na kumkufuru Yeye na [kuzuia] al-Masjid al-Haraam na kuwatoa watu wake humo ni dhambi kubwa zaidi mbele ya Allaah. Na kufuru ni mbaya zaidi kuliko kuua.”[1]

Allaah (Subhaanah) akasema kuwa kitendo hicho kilikuwa ni cha makosa kwa sababu mapigano katika miezi mitukufu ni jambo kubwa mbele ya Allaah. Hata hivyo matendo ya washirikina ni makubwa zaidi mbele ya Allaah kuliko kuzuia kutoka katika njia ya Allaah, kumkufuru Yeye na msikiti Mtakatifu na kumfukuza Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake ambao wao ndio wenye kustahiki zaidi msikiti Mtakatifu. Hayo ni makubwa zaidi kuliko kupigana katika mwezi mtakatifu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakubali moja ya tano katika ngawira zile na akachukua fidia kutoka kwa wale mateka wawili.

[1] 02:217

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 44-45
  • Imechapishwa: 26/04/2018