24. Maana halisi ya shirki na Radd juu ya tafsiri mbalimbali za kimakosa juu ya shirki


Kuko ambao wanaifasiri shirki kwamba ni kuabudu masanamu peke yake. Kuhusu kuwaabudu mawalii, makaburi, makuba na waja wema wanasema kwamba sio shirki. Wanaita hii kuwa ni Tawassul na kuomba uombezi na mfano wa hayo. Kwa mujibu wao wanaonelea kuwa shirki ni kule kuabudu masanamu peke yake.

Tunawajibu kwa kusema kuabudu masanamu ni aina moja wapo miongoni mwa aina za shirki. Shirki ni kumuomba asiyekuwa Allaah. Ni mamoja liwe sanamu au kitu kingine.

Washirikina walikuwa wakiabudu vitu mbalimbali na haikuwa masanamu peke yake. Miongoni mwao kulikuwa wanaoabudu masanamu. Wako waliokuwa wakiabudu jua na mwezi. Wako waliokuwa wakiabudu mashaytwaan. Wako waliokuwa wakiabudu miti na mawe. Wako waliokuwa wakiwaabudu Malaika. Wako waliokuwa wakimuabudu al-Masiyh na ´Uzayr. Wako waliokuwa wakiwaabudu mawalii na waja wema. Walikuwa ni wenye kutofautiana katika ´ibaadah zao. Si kwamba walikomeka kuyaabudu masaamu peke yake. Masanamu ilikuwa ni aina moja wapo miongoni mwa aina za waungu wao.

Baadhi yao wanasema kuwa shirki ni kuitakidi kuwa kuna mwengine anayeumba, anaruzuku, anayaendesha mambo pamoja na Allaah. Hivyo Ikiwa wewe hauitakidi kwamba kuna yeyote anayeruzuku, anayenufaisha au anayedhuru pamoja na Allaah, basi wewe ni mpwekeshaji. Tunawaambia: haya hayakusemwa na wale washirikina wa mwanzo. Hii ni Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Hawakushirikisha katika uola. Hawakuwa wakiitakidi ya kwamba masanamu yao yanaumba, kuruzuku, kuhuisha, kufisha au kuendesha mambo. Isipokuwa walikuwa wakiyafanya kuwa wakati na kati. Amesema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

”Wanaabudu badala ya Allaah ambao hawawezi kuwadhuru na wala kuwanufaisha na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10:18)

Hawakusema kuwa watu hawa wanaumba na kwamba wanaruzuku. Bali walisema kwamba ni waombezi wao mbele ya Allaah. Kauli hii ni kauli batili. Nayo ni kuikokmeza shirki katika Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Bali shirki ya fedheha ni katika Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Nayo ni kufanya kitu katika aina za ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah (´Azza wa Jall). Hii ndio shirki ambayo Allaah katahadharisha nayo, akawatumiliza Mitume wake kuikemea, na akaweka Jihaad ili kuiondosha. Inahusiana na kushirikisha katika ´ibaadah. Kuhusu shirki katika uola haikuwa katika watu. Hapakuwepo yeyote anayeitakidi kuwa masanamu yanaumba, yanaruzuku, kuhuisha, kufisha na kuendesha mambo. Isipokuwa walikuwa wanasema hawa ni wakati na kati na waombezi wetu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Tafsiri hii ya shirki ni tafsiri batili.

Miongoni mwa watu kuko ambao wanaifasiri shirki ya kuwa ni shirki al-Haakimiyyah. Wanafunika isiyokuwa hiyo. Wanasema Tawhiyd ya kisawasawa ni Tawhiyd-ul-Haakimiyyah na kwamba shirki ni shirki katika al-Haakimiyyah. Tunawajibu kwa kusema: Hii ni aina miongoni mwa shirki. Kwa kuwa kutunga sheria na hukumu ni haki ya Allaah (´Azza wa Jall). Kuhukumu kwa yale aliyoteremsha Allaah ni ´ibaadah. Lakini shirki haikukomeka katika aina hii. Bali shirki ni yenye kuenea kwa yale yote yanayoabudiwa badala ya Allaah (´Azza wa Jalla). Ni mamoja ikawa al-Haakimiyyah au mengineyo, kwa maombi, kwa kuchinja, kwa kuweka nadhiri, kwa kutaka uokozi au kwa mengineyo. Ama kuikomeza katika aina moja na kusema ndio shirki, hili ni kosa na upotevu. Haijuzu kuingia hili katika akili ya mwanafunzi. Isipokuwa kwa watu wenye malengo nyuma ya hilo. Endapo mtu atahukumu kwa Shari´ah na huku akawa anamuomba badala ya Allaah anakuwa mshirikina.

Kwa kifupi ni kwamba ni lazima ijulikane ni nini shirki. Kwa kuwa wanaifasiri kwa zisizokuwa tafsiri zake. Shirki ukiizingatia ndani ya Qur-aan utaona kwamba ni kumfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـه

”Wanaabudu badala ya Allaah ambao hawawezi kuwadhuru na wala kuwanufaisha na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (Yuunus 10:18)

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۖ لَا يَمْلِكُونَ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ

”Sema: “Ombeni wale mnaodai kuwa ni miungu badala ya Allaah, hawamiliki uzito wa atomu mbinguni wala ardhin.”(Sabaa´ 34:22)

Huku ni kushirikisha katika maombi. Kadhalika kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah. Hii pia ni shirki. Amesema (Ta´ala):

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

”Basi swali kwa ajili ya Mola wako na pia chinja [kwa ajili Yake].” (al-Kawthar 108:02)

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ

”Sema: “Hakika swalah yangu, na kuchinja kwangu, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu – hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa.” (al-An´aam 05:162-163)

Kwa hiyo kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah ni shirki. Kuna sampuli nyingi za shirki. Kidhibiti chake ni kwamba yule mwenye kufanya kitu miongoni mwa aina ya ´ibaadah akamfanyia asiyekuwa Allaha huyo ni mshirikina.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 04/07/2018